24. Subiri na taraji malipo kutoka kwa Allaah

Miongoni mwa mambo yenye manufaa makubwa na jambo bora zaidi linaloondosha kukata tamaa ni yale yaliyosihi katika Hadiyth ya Usamaah bin Zayd (Radhiya Allaahu ´anhumaa), ambaye amesema:

“Tulikuwa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati mmoja katika wasichana wake alipomtumia mjumbe kumweleza kuwa mtoto wake wa kiume ameaga dunia. Akamwambia yule mjumbe: “Ni Chake Allaah kile alichokichukua na ni Chake alichokitoa na kila kitu Kwake kina muda maalum; basi vuta subira na taraji malipo.” Mjumbe akarudi na kusema: ”Anaapa kwamba unatakiwa kuja.” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasimama akiwa pamoja na Sa´d bin ´Ubaadah, Mu´aadh bin Jabal, Ubayy bin Ka´b, Zayd bin Thaabit na mimi. Mtoto yule mdogo akamnyooshea mkono na moyo wake ukenda mbio kama kwamba ulikuwa kwenye chupa ndogo. Akabubujikwa na machozi. Sa´d akamwambia: ”Ee Mtume wa Allaah! Nini tena?” Akasema: ”Huu ni huruma ambayo Allaah ameiweka ndani ya nyoyo za waja Wake. Hakika hapana vyengine Allaah huwarehemu katika waja Wake wale wenye huruma.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

[1] al-Bukhaariy (1284) na Muslim (923).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin ´Abdillaah bin Naaswir-id-Diyn ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bard-ul-Akbaad ´inda Faqd-il-Awlaad, uk. 104-105
  • Imechapishwa: 22/08/2023