26. Hadiyth ”Hakika Allaah ataziweka mbingu kwenye kidole… “

Hadiyth ya kumi na moja

وَالسَّمَاوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ

“… na mbingu zitakunjwa mkononi Mwake wa kuume.”[1]

119 – Abut-Twaahir Ismaa´iyl bin ´Abdir-Rahmaan bin ´Amr al-Farraa’ ametukhabarisha: Imaam Abu Muhammad al-Maqdisiy ametuhadithia: Hibatullaah ad-Daqqaaq ametuhadithia: ´Abdullaah bin ´Aliy ad-Daqqaaq ametuhadithia: ´Aliy bin Muhammad al-Mu-addal ametuhadithia: Muhammad bin ´Amr ar-Razzaaz ametuhadithia: Muhammad bin ´Ubaydillaah ametuhadithia: Luwayn Muhammad ametuhadithia: Shaybaan ametuhadithia, kutoka kwa Mansuur, kutoka kwa Ibraahiym, kutoka kwa ´Abdullaah ambaye ameeleza:

“Mwanachuoni wa kiyahudi alikuja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kusema: “Ee Muhammad! Hakika Allaah ataziweka mbingu kwenye kidole na ardhi kwenye kidole kisha aseme: “Mimi ndiye Mfalme!” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akacheka mpaka magego yake yakaonekana kwa ajili ya kusadikisha maneno ya mwanachuoni wa kiyahudi yule.”[2]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

120 – Kwa al-Bukhaariy imepokelewa kutoka kwa Aadam, kutoka kwa Shaybaan (ambayo imetiliwa nguvu na Jariyr kupitia njia nyingine), kutoka kwa Mansuur ambaye amezidisha:

“… milima na miti kwenye kidole, maji na udongo kwenye kidole na viumbe wengine wote kwenye kidole.”

121 – at-Tirmidhiy amepokea kutoka kwa ´Atwaa’ bin as-Saa-ib, kutoka kwa Abuudh-Dhuhaa, kutoka kwa Ibn ´Abbaas kwa tamko lisemalo:

”Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwambia myahudi mmoja aliyepita karibu naye: ”Ee myahudi, nieleze.” Akasema: ”Ee Abul-Qaasim, itakuweje siku ambayo Allaah ataziweka mbingu kwenye kidole, ardhi kwenye kidole, maji kwenye kidole, milima kwenye kidole na viumbe wengine wote kwenye kidole?”

Abu Ja´far Muhammad bin as-Swalt akaanza kuonyesha kidole chake kidogo mpaka alipofika kwenye kidole gumba.

Ndipo Allaah akateremsha:

وَمَا قَدَرُوا اللَّـهَ حَقَّ قَدْرِهِ وَالْأَرْضُ جَمِيعًا قَبْضَتُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَالسَّمَاوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ ۚ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ

“Hawakumkadiria Allaah vile inavyostahiki kumkadiria na hali ardhi yote itakamatwa mkononi Mwake siku ya Qiyaamah na mbingu zitakunjwa mkononi Mwake wa kuume. Ametakasika na upungufu na yu juu kabisa kuliko yale wanayomshirikisha!”[3]

at-Tirmidhiy amesema:

”Hadiyth ni nzuri, geni na Swahiyh.”[4]

122 – Abu Daawuud as-Sijistaaniy amepokea – nadhani – ni katika kitabu chake ”al-Maraasiyl”: Ibn Muthannaa ametuhadithia: Mu´aadh bin Hishaam ametuhadithia: Baba yangu ametuhadithia, kutoka kwa Qataadah ambaye amesema:

”Tumetajiwa ya kwamba kuna rabi mmoja alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: ”Watakuwa wapi viumbe siku ya Qiyaamah?” Akasema: ”Mbingu zitakuwa kwenye kidole hichi kidogo, ardhi zitakuwa kwenye kidole cha kufuata.” Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Rabi amesema kweli.”

Wapokezi wake ni wenye kuaminika.

[1] 39:67

[2] al-Bukhaariy (1410), Muslim (1014), at-Tirmidhiy (661) na wengineo.

[3] 39:67

[4] al-Jaamiy´ (3240).

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy (afk. 748)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Arba´iyn fiy Swifaati Rabb-il-´Aalamiyn, uk. 123-127
  • Imechapishwa: 09/06/2024