26. Dalili kwamba Allaah ataonekana Aakhirah

Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

لِّلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَىٰ وَزِيَادَةٌ

“Kwa wale waliofanya mazuri watapata Pepo na zaidi.” (10:26)

Mazuri (الْحُسْنَىٰ) maana yake ni Pepo. Zaidi (زِيَادَةٌ) maana yake ni kuona uso wa Allaah. Hivyo ndivyo ilivyokuja katika “as-Swahiyh” ya Muslim[1].

Amesema (Ta´ala):

لَهُم مَّا يَشَاءُونَ فِيهَا وَلَدَيْنَا مَزِيدٌ

“Watapata humo wayatakayo na Kwetu kuna yaliyo zaidi” (50:35)

Watapata humo wayatakayo kwa maana ya Pepo. Kwetu kuna yaliyo zaidi kwa maana kumuona Allaah (Jalla wa ´Alaa).

Amesema vilevile (Ta´ala):

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاضِرَةٌ إِلَىٰ رَبِّهَا نَاظِرَةٌ

“Kuna nyuso siku hiyo zitanawiri. Zikimtazama Mola wake.” (75:22-23)

Bi maana kwa macho yao. Kwa sababu kuona (النظر) kukifuatiwa na (إِلَىٰ) maana yake ni kuona kwa macho.

Lakini (النظر) ikiwa peke yake maana yake ni kusimama na kusubiri.

Lakini (النظر) ikifuatiwa na (فِي), kama ilivyo katika maneno Yake (Ta´ala):

أَوَلَمْ يَنظُرُوا فِي مَلَكُوتِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ

“Je, hawazingatii (فِي) ufalme wa mbingu na ardhi.” (07:185)

maana yake inakuwa kufikiria na kuzingatia.

Kwa ufupi ni kwamba (النظر) ni kama ifuatavyo:

1 – Ikija peke yake maana yake ni kusubiri.

2 – Ikifuatiwa na (فِي) maana yake ni kufikiria na kuzingatia.

3 – Ikifuatiwa na (إِلَىٰ) maana yake ni kutazama kwa macho.

Hizi ndio kanuni.

Aayah tulionayo imefuatiwa na (إِلَىٰ):

إِلَىٰ رَبِّهَا نَاظِرَةٌ

“… (إِلَىٰ) zikimtazama Mola wake.” (75:22-23)

Maana yake ni kuona kwa macho.

Kuhusu maneno Yake (Ta´ala):

لَّا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الْأَبْصَارَ

“Macho hayamzunguki bali Yeye anayazunguka macho yote.” (06:103)

Kuzunguka haina maana ya kuona. Wewe unaweza kukiona na kukitazama kitu lakini usikidiriki kwa maana usikizunguki. Huwezi kukizunguka chenye kuonwa kwa kila pande ingawa unakiona. Waumini watamuona Mola Wao siku ya Qiyaamah lakini pamoja na hivyo hawatomzunguka. Kwa msemo mwingine hawatomzunguka utukufu Wake  (Jalla wa ´Alaa) na hawamzingiri kielimu. Wewe unaliona jua lakini huwezi kulizunguka kutokana na ukali na miale yake. Hili ni kuhusu kiumbe. Vipi kuhusu Muumbaji (Subhaanahu wa Ta´ala)? Kukanushwa uzingirwaji sio kukanushwa kuonekana. Uhakika wa mambo ni kwamba wamesema kukanushwa uzingirwaji kunafahamisha ya kwamba Ataonekana lakini hata hivyo hatodirikiwa. Kwa maana nyingine hatozungukwa (Subhaanahu wa Ta´ala).

Kuhusu maneno ya Allaah kumwambia Muusa:

لَن تَرَانِي

“(لَن) hutoniona!” (07:143)

Haina maana ya makanusho ya milele. Maneno Yake:

لَن تَرَانِي

“(لَن) hutoniona!”

Bi maana duniani. Dalili ya hilo ni kwamba Kuonekana kumethibiti Aakhirah.

Wasomi wa lugha wanasema kuwa neno (لَن) sio la makanusho ya milele. Bali ni la makanusho ya muda fulani.

Maneno yake mtunzi (Rahimahu Allaah):

“Allaah atajidhihirisha… ”

Bi maana atajionyesha (Subhaanahu wa Ta´ala). Atajiondoshea pazia (Jalla wa ´Alaa).

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kama ambavyo mwezi mwandamo haufichi.”

Haya yamechukuliwa kutoka katika maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika nyinyi mtamuona Mola wenu kama mnavyouona mwezi mwandamo huu katika usiku wa m´garo.”[2]

Usiku wa mng´aro ni usiku wa tarehe kumi na tano au kumi na nne. Ni usiku ambao mwezi unakuwa mkubwa kwelikweli. Kwa kuwa mwezi mwanzoni mwa mwezi unakuwa dhaifu. Halafu baada ya hapo unakuwa mkubwa zaidi na zaidi mpaka unatimia katika zile nyusiku za mng´aro. Kisha unapungua tena na kuwa mwembamba. Amesema (Ta´ala):

وَالْقَمَرَ قَدَّرْنَاهُ مَنَازِلَ حَتَّىٰ عَادَ كَالْعُرْجُونِ الْقَدِيمِ

“Mwezi Tumeukadiria vituo mpaka ukarudi [mwembamba] kama kwamba karara la shina la mtende lililopinda la zamani.” (36:39)

[1] Muslim (181) na (297)

[2] al-Bukhaariy (7439) na Muslim (183) na (302)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 80-82
  • Imechapishwa: 08/01/2024