25. Kutofautiana kwa watu juu ya Kuonekana kwa Allaah

Imaam Ibn Abiy Daawuud (Rahimahu Allaah) amesema:

وقل يتجلى الله للخلقِ جهرةً

Sema “Allaah atajidhihirisha kwa viumbe waziwazi

كما البدر لا يخفى وربك أوضحُ

    kama ambavyo mwezi mwandamo haufichi – basi na Mola wako ataonekana kwa uwazi zaidi”

MAELEZO

Hili ni suala la Kuonekana kwa Allaah (´Azza wa Jall). Je, viumbe watamuona Allaah au hawatomuona? Jahmiyyah na Mu´tazilah wote wanapinga Kuonekana. Wanasema kuwa Allaah hatoonekana. Hoja yao ni kwamba viwiliwili ndivyo huonekana na wanasema kuwa Allaah hana kiwiliwili. Hivyo hatoonekana. Wanapinga Kuonekana kabisa, si duniani wala Aakhirah. Tunamuomba Allaah usalama.

Kuna wengine wanaosema kuwa Allaah anaonekana duniani na Aakhirah. Hii ni ´Aqiydah ya baadhi ya Suufiyyah.

Maoni ya tatu – na haya ndio maoni ya watu wa haki – ni kwamba Allaah (´Azza wa Jall) ataonekana Aakhirah. Watu wa Peponi watamuona. Kumethibiti Hadiyth tele juu ya hilo zilizopokelewa kwa mapokezi mengi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kuhusu duniani hatoonekana. Watu hawawezi kumuona Allaah duniani. Pindi Muusa (´alayhis-Salaam) alipomuomba kumuona Allaah (Subhaanah) hapa duniani kwa kusema:

قَالَ رَبِّ أَرِنِي أَنظُرْ إِلَيْكَ ۚ قَالَ لَن تَرَانِي وَلَـٰكِنِ انظُرْ إِلَى الْجَبَلِ فَإِنِ اسْتَقَرَّ مَكَانَهُ فَسَوْفَ تَرَانِي ۚ فَلَمَّا تَجَلَّىٰ رَبُّهُ لِلْجَبَلِ جَعَلَهُ دَكًّا وَخَرَّ مُوسَىٰ صَعِقًا ۚ فَلَمَّا أَفَاقَ قَالَ سُبْحَانَكَ تُبْتُ إِلَيْكَ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُؤْمِنِينَ

“Akasema: “Mola wangu! Nionyeshe ili nikutazame.” Akasema: “Hutoniona! Lakini tazama jabali, likitulia mahali pake, basi utaniona.” Basi Mola wako alipojidhihirisha katika jabali akalifanya livurugike kuwa vumbi na Muusa akaanguka hali ya kuzimia. Alipozindukana akasema: “Utakasifu ni Wako! Nimetubu Kwako nami ni wa kwanza wa wanaoamini.”” (07:143)

Mlima ulipasuka na ukageuka udongo kutokana na ukubwa wa Allaah (´Azza wa Jall). Ni vipi binaadamu ataweza kumuona Allaah? Hili ni kuhusiana na duniani.

Kuhusu Aakhirah Allaah atawapa nguvu watu wa Peponi ambazo kwazo wataweza kumuona Allaah (´Azza wa Jall). Huku ni kuwakirimu. Pindi walipomuamini duniani pasi na kumuona ndipo Allaah akawakirimu na akajionyesha kwao Peponi ili waburudike na kule kumuona. Qur-aan na Sunnah iliyopokelewa kwa mapokezi mengi imefahamisha hivyo.

Lakini makafiri ilipokuwa hawakumuamini duniani ndipo Allaah akawazuia kumuona siku ya Qiyaamah. Amesema (Ta´ala):

كَلَّا إِنَّهُمْ عَن رَّبِّهِمْ يَوْمَئِذٍ لَّمَحْجُوبُونَ

“Hapana! Hakika wao siku hiyo watawekewa kizuizi [wasimuone] Mola wao.” (83:15)

Ikiwa makafiri wao watazuiawa na kumuona Mola wao basi mtu anapata kufahamu kupitia hili ya kwamba waumini hawatozuiwa na kumuona Mola wao. Vinginevyo makafiri na waumini wangalikuwa sawa Aakhirah. Allaah ametafautisha kati yao. Amewakirimu waumini kwa kujionyesha kwao (Subhaanahu wa Ta´ala) kama inavyolingana na utukufu Wake. Watamuona waziwazi kwa macho yao na hawatosongamana katika kumuona. Bi maana hawatokuwa na msongamano katika kumuona. Watamuona waziwazi kwa macho yao kama wanavyoliona jua waziwazi pasi na mawingu na kama wanavyouona mwezi mg´aro. Haya ni mashabihisho ya maono na sio ya kitachoonwa. Hivyo ndivyo zimesihi Hadiyth kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Haya ndio madhehebu ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah kuhusu Kuonekana kwa Allaah (´Azza wa Jall).

Jambo muhimu analotakiwa mwanafunzi kushikamana nalo ni kumdhukuru Allaah (´Azza wa Jall) katika kila hali na kila wakati.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 78-79
  • Imechapishwa: 02/01/2024