24. Matamshi ya Qur-aan yameumbwa au hayakuumbwa?

Ni lazima kupambanua na kuuliza: nini unachokusudia kwa kusema kuwa matamshi yako ya Qur-aan; unakusudia ule utamkaji na sauti au kile kinachotamkwa? Ikiwa unakusudia kile kinachotamkwa hakikuumbwa. Kile kinachotamkwa ni maneno ya Allaah (Jalla wa ´Alaa). Lakini matamshi ikiwa unakusudia matamshi unayotamka kwa ulimi wako yameumbwa. Ulimi wako umeumbwa. Kadhalika sauti yako imeumbwa. Matamshi yako yameumbwa. Lakini kile chenye kutamkwa hakikuumbwa. Ni lazima kupambanua. Wao wanataka useme kwa jumla ya kwamba matamshi ya Qur-aan ni kiumbe au useme sio kiumbe. Wanaingia kwa hila kama hii. Ni lazima upambanue na uwakatie njia.

Kwa ajili hii ndio maana Ahl-us-Sunnah wanasema kuwa sauti ni ya yule msomaji na maneno ni ya Allaah. Kile chenye kutamkwa ni maneno ya Allaah. Kuhusu matamshi ni maneno yaliyoumbwa. Bi maana sauti yake imeumbwa. Ule utamkaji wake umeumbwa. Kwa ajili hii ndio maana visomo na sauti zinatofautiana. Kuna sauti ambazo ni nzuri na zingine sio nzuri. Kuna sauti ziko vizuri na zingine haziko vizuri. Hii inafahamisha kwamba sauti imeumbwa. Wasomaji wanatafautiana. Kuna ambao wamepewa sauti nzuri na wengine ni kinyume na hivo. Kuhusu maneno ya Allaah (´Azza wa Jall) ni lazima yawe katika upeo wa ukamilifu wa hali ya juu kabisa.

Haikutakikana kuingia katika suala hili. Lakini wao ndio ambao wamewafanya waislamu kuingia katika jambo hili. Hivyo ni lazima kulifichua na kulibainisha. Kwa hakika ni msiba. Lau Allaah asingelitenga maimamu wakalibainisha basi jambo hili lingewatatiza watu wengi. Kwa hivyo kuna madhehebu matatu:

1 – Jahmiyyah wanaosema kuwa Qur-aan imeumbwa.

2 – Wenye kusimama.

3 – Watamkaji wanaosema kuwa matamshi ya Qur-aan yameumbwa au hayakuumbwa. Tunawaambia: ni lazima kupambanua. Ikiwa unakusudia ule utamkaji wa sauti umeumbwa. Lakini ikiwa unakusudia kile kinachotamkwa na kinachosomwa ni maneno ya Allaah hayakuumbwa. Kwa ajili hii ndio maana imekuja katika Hadiyth:

“Ipambeni Qur-aan kwa sauti zenu.”[1]

Inatakikana kwa msomaji aipambe sauti yake kwa Qur-aan. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anapendezwa na sauti nzuri ya Qur-aan. Alikuwa akimsikiza Abu Muusa al-Ash´ariy (Radhiya Allaahu ´anh) pindi alipokuwa akiswali usiku. Allaah alikuwa amemtunuku sauti nzuri. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawa anamsikiliza[2]. Vivyo hivyo alimuamrisha ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amsomee na huku anasikiliza. Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mimi napenda kuisikia kutoka kwa mwengine asiyekuwa mimi.”[3]

Akamsomea mwanzoni mwa Suurah “an-Nisaa´”. Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akipenda sauti nzuri ya Qur-aan. Kuwa na sauti nzuri ni neema kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall).

[1] Abu Daawuud (1468), an-Nasaa´iy (02/179), Ibn Maajah (1342), Ahmad (04/283) na wengineo

[2] al-Bukhaariy (5048) na Muslim (793) na (236).

[3] al-Bukhaariy (4582) na Muslim (800) na (248)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 75-77
  • Imechapishwa: 02/01/2024