26. Bora kwa msafiri ni yeye kukamilisha au kufupisha?

Swali 26: Msafiri amewahi faradhi nyumbani kwa wakazi na yeye ndiye anastahiki zaidi kuwa imamu – je, awaswalishe swalah ya mkazi au ya msafiri[1]?

Jibu: Sunnah ni yeye kuwaswalisha swalah ya msafiri. Atakapotoa salamu basi wao watasimama na kukamilisha kivyao. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipowaswalisha watu wa Makkah mwaka wa Ufunguzi aliwaswalisha swalah ya msafiri na akawaamrisha wakamilishe swalah zao. Akiswali kikamilifu ni sahihi ijapo bora ni kutofanya hivo.

Imethibiti kutoka kwa ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba alikuwa akiwaswalisha watu kwa kukamilisha katika hajj katika ile miaka ya mwishomwisho ya uongozi wake. Vilevile imethibiti kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ya kuwa alikuwa akiwaswalisha watu kwa kukamilisha safarini na akisema:

“Hakunipi ugumu.”

Lakini bora ni vile alivofanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu yeye ndiye mwekaji Shari´ah aliyefunzwa kutoka kwa Mola Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/260).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Musaafir, uk. 41-42
  • Imechapishwa: 09/03/2022