25. Msafiri anayetaka kuswali nyuma ya mkazi na kinyume chake

Swali 25: Mtu akisafiri na akataka kuswali Dhuhr na mkusanyiko na akamuona mtu ambaye ni mkazi ameshaswali swalah ya Dhuhr – je, mkazi aswali pamoja na msafiri? Je, afupishe swalah pamoja naye au aswali kwa kukamilisha[1]?

Jibu: Mkazi akiswali pamoja na msafiri kwa ajili ya kutafuta fadhilah za mkusanyiko baada ya kuwa mkazi amekwishaswali faradhi yake, basi aswali mfano wa ile swalah ya msafiri ambapo ataswali Rak´ah mbili kwa sababu juu yake itakuwa ni swalah ya sunnah. Lakini mkazi akiswali nyuma ya msafiri swalah ya faradhi, kama vile Dhuhr, ´Aswr na ´Ishaa, basi ataswali Rak´ah nne na hivyo atalazimika kukamilisha swalah yake baada ya msafiri kutoa Tasliym kutoka katika Rak´ah mbili. Ama msafiri akiswali nyuma ya mkazi swalah ya faradhi wote wawili, basi msafiri atalazimika kuikamilisha Rak´ah nne kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. Hilo ni kutokana na yale aliyopokea Imaam Ahmad katika “al-Musnad” yake na Imaam Muslim katika “as-Swahiyh” yake (Rahimahumaa Allaah) kupitia kwa Ibn ´Abbaas aliyeulizwa kuhusu msafiri anayeswali nyuma ya imamu ambaye ni mkazi Rak´ah nne na anaswali pamoja na marafiki zake Rak´ah mbili ambapo akajibu:

“Hivo ndio Sunnah.”

Pia kutokana na ueneaji wa maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Hakika si venginevyo imamu amewekwa ili afuatwe.”[2]

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/260).

[2] al-Bukhaariy (510) na Muslim (1151, 1154).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Musaafir, uk. 40-41
  • Imechapishwa: 09/03/2022