25. Majibu kwa njia nyingi kuonyesha kwamba mtu anaweza kukufuru hata kama ametimiza nguzo za Uislamu II

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Yaweza kusemwa pia: “Wale ambao ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) aliwaua kwa kuwaunguza moto, wote walikuwa wakidai Uislamu. Walikuwa ni katika wafuasi wa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) na walisoma elimu kutoka kwa Maswahabah, lakini walimuamini ´Aliy kama ilivyokuwa inaaminiwa kwa Yuusuf, Shamsaan na mfano wao. Vipi walikubaliana Maswahabah kuwapiga vita na kuwaona kuwa ni makafiri? Je, unaafikiri ya kwamba Maswahabah wanawakufurisha Waislamu au mnadhani ya kwamba kuwa na imani kwa Taaj na mfano wake haidhuru na kuwa na imani kwa ´Aliy bin Abiy Twaalib ndio kunakufurisha?”

MAELEZO

Mtunzi wa kitabu Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) anabainisha kwa mifano hii ujinga wa wajinga katika kuwakufurisha waabudu makaburi na waabudu mawalii. Kwa sababu kulikuwepo kundi katika zama zake ambalo lilikuwa likijinasibisha katika elimu na kwamba wao ni waislamu. Pamoja na haya walikuwa wakiwaabudu kundi la makafiri kama vile Taaj, Yuusuf na Shamsaan. Walikuwa wakichupa mipaka kwao na wakidai kuwa na sifa za kiungu na wakiona kuwa haidhuru kufanya hivo kwa sababu ni waja wema, wakifanya Tabarruk kwa waja wema na wakiwaomba. Ndipo Shaykh (Rahimahu Allaah) akawabainishia kuwa imani hii ndio kufuru kubwa. Ikiwa imani waliokuwa nayo watu juu ya al-Laat, al-´Uzzaa, Manaat, Malaika na Mitume kabla ya kuja Uislamu iliwakufurisha, basi ni vivyo hivyo juu ya watu hawa ambao wana imani juu ya Yuusuf, Shamsaan, Taaj na wengineo inawakufurisha. Hakuna tofauti juu ya hayo. Kumfanyia ´ibaadah asiyekuwa Allaah ni kumshirikisha Allaah. Ni mamoja yule anayeabudiwa ni sanamu, walii, jini, Malaika au wengineo. Sababu na hukumu ni kule kumfanyia ´ibaadah asiyekuwa Allaah. Hii ndio sababu. Mwenye kumfanyia ´ibaadah asiyekuwa Allaah – haijalishi kitu ni nani – basi amefanya shirki kubwa. Amesema (Jalla wa ´Alaa):

فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Hivyo basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.”[1]

وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ

“Hakika umefunuliwa Wahy na kwa wale walio kabla yako kwamba: “Ukifanya shirki bila shaka yataporomoka matendo yako na hakika utakuwa miongoni mwa waliokhasirika.”[2]

إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ

“Hakika yule atakayemshirikisha Allaah, basi hakika Allaah atamharamishia Pepo na makazi yake yatakuwa ni motoni – na madhalimu hawatopata yeyote mwenye kuwanusuru.”[3]

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa lakini anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”[4]

Ni dalili inayofahamisha kuwa washirikina hawatosamehewa, matendo yao yameharibika na Pepo imeharamishwa kwa mshirikina. Ni mamoja huyo mwenye kuabudiwa pamoja na Allaah ni jini, walii, Malaika, mwezi, jua, sanamu, mti au vyenginevyo. Hukumu ni yenye kuenea. Kwa sababu vyote hivo ni batili, kama alivosema Allaah (´Azza wa Jall) ndani ya Qur-aan:

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْحَقُّ وَأَنَّ مَا يَدْعُونَ مِن دُونِهِ هُوَ الْبَاطِلُ وَأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْعَلِيُّ الْكَبِيرُ

“Hivyo ni kwa kuwa Allaah ndiye wa haki na kwamba vile wanavyoomba badala Yake ndiyo batili na kwamba Allaah ndiye Aliye juu kabisa, Mkubwa.”[5]

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ

“Mola wako ameamuru kwamba: “Msiabudu isipokuwa Yeye pekee.”[6]

وَإِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ ۖ لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الرَّحْمَـٰنُ الرَّحِيمُ

“Mungu wenu ni Mungu mmoja pekee; hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye, Mwingi wa huruma, Mwenye kurehemu.”[7]

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ

“Basi elewa kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na omba msamaha kwa dhambi zako.”[8]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaambia watu wakati alipotumwa:

“Enyi watu! Semeni ´hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah` mtafaulu.”

Hivi ndivo alivowaamrisha watamke shahaadah. Wakilitamka kwa ukweli linabomoa shirki na wanakuwa waislamu kwa kitendo hicho. Kuhusu ambao watalitamka na wakati huohuo wanawaabudu wasiokuwa Allaah halitomnufaisha kama wanafiki, mayahudi na wengineo ambao wanalitamka na wakati huohuo wanaabudu wengine wasiokuwa Allaah. Vivyo hivyo wale ambao wamechupa mipaka kwa Allaah na wakamwabudu yeye badala ya Allaah walikuwa washirikina. Pamoja na haya walikuwa wakitamka shahaadah na wakiishi katika zama za Maswahabah na wakisema kuwa ni waislamu. Wakati walipochupa mipaka juu ya ´Aliy, wakasema kuwa yeye ndiye Allaah, wakamuomba yeye badala ya Allaah na wakamfanya kuwa ni mungu pamoja na Allaah wakakufuru. ´Aliy mwenyewe ndiye aliwapiga vita. Maswahabah wote waliafikiana juu ya kuwaua. Bali (Radhiya Allaahu ´anh) hakuwaua kwa upanga. Aliwachimbia shimo chini kisha akawaingiza ndani yake na kuwachoma kwa moto kutokana na (Radhiya Allaahu ´anh) alivyokuwa amewakasirikia. Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Lau angeliwaua kwa upanga ingelikuwa ni yenye kupendeza zaidi kwangu. Kwa sababu hakuna yeyote anaadhibu kwa moto isipokuwa Allaah pekee.”

Alifanya hivo kutokana na ukali wa hasira juu yao ndipo akawachoma kwa moto. Kutokana na ukafiri wao mkubwa mpaka wakamfanya yeye kuwa ndiye mungu. Walisema:

“Wewe ndiye.”

Bi maana Allaah. Matokeo yake wakamuomba, wakachupa mipaka kwake na wakadai kuwa ndiye mungu anayestahiki kuabudiwa. Hivo ndivo wanavofanya Raafidhwah hii leo kwa ´Aliy, al-Hasan na al-Husayn ambapo wanawaomba, wanawataka msaada na wanawawekea nadhiri, matendo ambayo ni shirki kubwa. Raafidhwah ndio warithi wa wachupaji hawa katika Imaamiyyah na wengineo ambao wamevuka mipaka kwa ´Aliy na kwa watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hawa ndio warithi wao, kama itavyokuja kuhusu Banuu ´Ubayd al-Qaddaas.

[1] 72:18

[2] 39:65

[3] 05:72

[4] 04:48

[5] 22:62

[6] 17:23

[7] 02:163

[8] 47:19

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 91-93
  • Imechapishwa: 21/10/2021