26. Kuwa na msimamo wa kupindukia kwa waja wema ni ukafiri

Kinacholengwa ni kwamba kuwa na msimamo wa kupindukia kwa Malaika, Mtume au Swahabah kama mfano wa ´Aliy, jini, mti, jiwe au sanamu, yote ni kumshirikisha Allaah. Akimuomba badala ya Allaah, akawataka msaada au akawawekea nadhiri ni shirki kubwa. Shaykh Muhammad (Rahimahu Allaah) amesema akiwahoji: Hivi mnadhani kuwa na msimamo wa kuchupa mipaka kwa Taaj, Shamsaan na mfano wao hakudhuru na kuwa na msimamo wa kuchupa mipaka kwa ´Aliy ndio kunadhuru? Huu ni ujinga mkubwa. Ikiwa kuchupa mipaka kwa Taaj hakudhuru basi msimamo wa kuchupa mipaka kwa ´Aliy kuna haki zaidi kutodhuru. ´Aliy ni mbora kuliko Taaj na Shamsaan. Kutokana na kuchupa mipaka huku walizingatiwa wenye kufanya hivo kuwa ni washirikina kama makafiri wenye kustahiki kuuawa. Wale wenye kuchupa mipaka kwa Taaj, Shamsaan, ´Abdul-Qaadir al-Jaylaan, al-Husayn, al-Hasan au Ja´far bin Muhammad wana haki zaidi [ya kukufurishwa]. Kwa sababu ´Aliy ni mbora zaidi kuliko wao. Wale waliochupa mipaka kwa watu hao wana haki zaidi ya kukufurishwa na kustahiki kuuawa.

Vivyo hivyo wale wenye kuchupa mipaka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au Mitume wengine na akawaabudu badala ya Allaah – na wao ni wabora zaidi kuliko ´Aliy – wanakufuru. Wale wenye kumwabudu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Idriys, Muusa, Haaruun au wakamwabudu ´Iysaa ni makafiri. Ni kama manaswara ambao wanamwabudu ´Iysaa pamoja na Allaah na wakawa watu makafiri zaidi. Kadhalika mayahudi ambao wamemwabudu al-´Uzayr ni watu makafiri zaidi.

Kwa hivyo ni wajibu kwa mwanafunzi azindukane na ajifunze kwamba kumfanyia ´ibaadah asiyekuwa Allaah anakuwa amemshirikisha Allaah shirki kubwa. Ni mamoja ´ibaadah hiyo amefanyiwa Mtume, mja mwema, jini, mtu, mti au jiwe. Yote haya ni kumshirikisha Allaah. Ni lazima ´ibaadah afanyiwe Allaah pekee:

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْحَقُّ وَأَنَّ مَا يَدْعُونَ مِن دُونِهِ هُوَ الْبَاطِلُ

“Hivyo ni kwa kuwa Allaah ndiye wa haki na kwamba vile wanavyoomba badala Yake ndiyo batil.”[1]

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ

“Mola wako ameamuru kwamba: “Msiabudu isipokuwa Yeye pekee.”[2]

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا

“Na mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe Yeye na chochote.”[3]

فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ

“Hivyo basi msimfanyie Allaah washirika, na hali ya kuwa nyinyi mnajua.”[4]

[1] 22:62

[2] 17:23

[3] 04:36

[4] 02:22

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 93-94
  • Imechapishwa: 21/10/2021