24. Majibu kwa njia nyingi kuonyesha kwamba mtu anaweza kukufuru hata kama ametimiza nguzo za Uislamu

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Ukihakikisha ya kwamba wale aliyowapiga vita Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa na akili nzuri na shirki kidogo kuliko watu hawa[1], basi jua kuwa hawa wana shubuha wanazozitaja kwa tulioyataja, na ni katika shubuha zao kubwa, hivyo sikiliza vizuri majibu yake. Wanasema: “Wale ambao Qur-aan iliwateremkia walikuwa hawashuhudii ya kwamba hapana mungu isipokuwa Allaah, walikuwa wanamkadhibisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wanapinga kufufuliwa na wanakadhibisha Qur-aan na kuiona kuwa ni uchawi. Ama sisi tunashuhudia hapana mungu isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, na tunaisadikisha Qur-aan, na tunaamini kufufuliwa, tunaswali na tunafunga. Vipi basi mtatufanya sisi ni kama wao?”

Jibu ni: “Hakuna tofauti baina ya wanachuoni wote, ya kwamba mtu akimsadikisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika kitu na akamkadhibisha katika kitu kingine, ni kafiri ambaye hakuingia katika Uislamu. Hali kadhalika [ni kafiri] iwapo ataamini baadhi ya Qur-aan na akapinga baadhi yake nyingine, kama mwenye kukubali Tawhiyd na akapinga uwajibu wa swalah, au akakubali Tawhiyd na swalah na akakadhibisha uwajibu wa zakaah, au akakubali yote haya na akakadhibisha uwajibu wa swawm, au akakubali yote haya na akakadhibisha uwajibu wa hajj. Katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati watu hawakujisalimisha juu ya hajj, Allah aliteremsha kuhusu wao:

وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلً ¤ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ

”Na kwa ajili ya Allaah ni wajibu kwa watu watekeleze Hajj katika Nyumba hiyo kwa mwenye uwezo wa kuiendea. Na atakayekanusha, basi hakika Allaah ni Mkwasi kwa walimwengu.” (Aal ´Imraan 03 : 97)

Na mwenye kukubali yote haya na akakadhibisha kufufuliwa, anakufuru kwa maafikiano na ni halali damu yake na mali yake. Kama alivyosema (Ta´ala):

إِنَّ الَّذِينَ يَكْفُرُونَ بِاللَّـهِ وَرُسُلِهِ وَيُرِيدُونَ أَن يُفَرِّقُوا بَيْنَ اللَّـهِ وَرُسُلِهِ وَيَقُولُونَ نُؤْمِنُ بِبَعْضٍ وَنَكْفُرُ بِبَعْضٍ وَيُرِيدُونَ أَن يَتَّخِذُوا بَيْنَ ذَٰلِكَ سَبِيلًا أُولَـٰئِكَ هُمُ الْكَافِرُونَ حَقًّا

”Hakika wale wanaomkufuru Allaah na Mitume Yake na wanataka kufarikisha baina ya Allaah na Mitume Wake na wanasema: “Tunaamini baadhi na tunawakanusha baadhi” na wanataka kuchukua njia iliyo kati ya hayo – hao ndio makafiri wa kweli.” (an-Nisaa´ 04 : 150-151)

Ikiwa Allaah ameweka wazi katika Kitabu Chake ya kwamba mwenye kuamini baadhi na akakufuru baadhi, basi ni kafiri wa kweli na kwamba anastahiki alichokitaja, shubuha hii itakuwa imeondoka. Na hiki ni kitu walichosema watu kutoka al-Ahsaa´ katika kitabu chao walichotutumia. Mtu anaweza kusema pia: “Ikiwa unakubali ya kwamba mwenye kumsadikisha Mtume katika kila kitu na akakadhibisha uwajibu wa swalah, ni kafiri ambaye ni halali damu yake kwa maafikiano, hali kadhalika akikubali kila kitu isipokuwa kufufuliwa, hali kadhalika lau atakadhibisha uwajibu wa kufunga swawm ya Ramadhaan, hakanushi isipokuwa haya ilihali mengine yote anayasadikisha – madhehebu mbalimbali wamekubaliana kwa hili na Qur-aan imeliongelea kama tulivyosema – mtu atafahamu ya kwamba Tawhiyd ndio faradhi kubwa aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ni kubwa kuliko swalah, zakaah, swawm na hajj. Vipi itakuwa mtu akikadhibisha kitu katika mambo haya anakufuru – hata kama atayafanyia kazi mambo yote aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – na akikadhibisha Tawhiyd ambayo ndio dini ya Mitume wote asikufuru?” Ametakasika Allaah! Ni ajabu ilioje ya ujinga huu.

Mtu anaweza kusema pia: “Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) waliwapiga vita na Banuu Haniyfah, ilihali walikuwa Waislamu pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wao wanashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, walikuwa wakiadhini na wakiswali.” Akisema: “Walisema: “Musaylamah ni Mtume”, mwambie: “Hili ndilo lililokuwa linatakikana. Ikiwa yule anayempandisha mtu katika daraja ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anakufuru na mali yake inakuwa halali na damu yake, na wala haimfai kitu Shahaadah zake mbili wala swalah, vipi kwa yule mwenye kumpandisha Shamsaan, Yuusuf, Swahabah au Mtume katika daraja ya al-Jabbaar wa mbingu na ardhi? Ametakasika Allaah! Ni Ukubwa ulioje alonao.

كَذَٰلِكَ يَطْبَعُ اللَّـهُ عَلَىٰ قُلُوبِ الَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ

”Hivyo ndivyo Allaah anavyopiga muhuri juu ya nyoyo za wale wasiojua.” (ar-Ruum 30 : 59)

MAELEZO

Shaykh wetu (Rahimahu Allaah) ametaja kwamba washirikina hawa; waabudu makaburi na waabudu mawalii, wana shubuha wanazotumia dhidi ya wale wenye kuwakufurisha na kuhalalisha damu na mali zao, kuwakemea juu ya kumwabudu kwao mwengine asiyekuwa Allaah, kuyaelekea makaburi, mawalii na kuwaomba, wanasema kuwa sisi tumewafananisha na makafiri wa Quraysh na wengineo na tumezihalalisha damu na mali zao ilihali eti wao wanashuhudia ya kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, wanaswali, wanafunga na wanaamini kufufuliwa. Wanahoji ni vipi tutawafanya kama watu wale? Huu ni utata unaofichikana kwa watu wengi. Wajibu uwaambie kwamba ni kweli wao wanashuhudia ya kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, lakini Shari´ah imefahamisha kwamba yule mwenye kupinga chochote chenye kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anakufuru. Haijalishi kitu hata kama atafanya kila kitu katika yale aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtu akikubali Tawhiyd na akapinga uwajibu wa swalah hakufuru? Anakufuru. Akipinga uwajibu wa zakaah, kufunga Ramadhaan, hajj kwa yule mwenye uwezo asiamini kufufuliwa na kukusanywa anakufuru. Haijalishi kitu hata kama anaswali na anafunga. Ikiwa mambo haya yanatambulikana kwetu na kwamba mwenye kuacha mambo haya hali ya kuwa ni mwenye kuyapinga anakufuru, vipi kwa yule mwenye kupinga shahaadah mbili na maana zake na isitohe akaabudu pamoja na Allaah wengine? Ikiwa yule ambaye anamfanya Musaylamah ni Mtume, kama alivyo Muhammad, anakufuru kwa mtazamo wa wote na Maswahabah wakawapiga vita kwa sababu hiyo, ni vipi kwa yule atakayemnyanyua mtu katika ngazi ya Mola (´Azza wa Jall)? Ikiwa yule ambaye atampandisha mtu katika ngazi ya Mtume anakufuru kwa sababu amemfanya kuwa ni Mtume ilihali Muhammad ndiye Mtume wa mwisho, vipi kwa yule mwenye kumnyanyua mtu kama vile Shamsaan, Yuusuf, Ibn ´Alwaan na wengineo katika ngazi ya Allaah (´Azza wa Jall) kwa njia ya kwamba akawa anamuomba, anamtaka msaada, anamuwekea nadhiri na anamchinjia, je, huyu si ana haki zaidi ya kukufuru kuliko wale waliomnyanyua Musaylamah katika ngazi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?

Kadhalika yule mwenye kuwaabudu Malaika au majini na akawaomba msaada atakuwa amewaweka katika ngazi ya Allaah na amewaabudu pamoja na Allaah. Mtu kama huyu anakuwa kafiri. Haijalishi kitu hata kama ataswali, atafunga, atahiji na kufanya nembo zote za Uislamu. Ni kama ambavyo ataswali, atafunga na atafanya kila kitu lakini hata hivyo akakanusha utume wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au akapinga kuwa yeye ndiye Mtume wa mwisho anakufuru. ´Ibaadah hizi alizokubali hazitomnufaisha kitu. Kwa haya inapata kubainika kuwa mwenye kufanya mambo yaliyowekwa katika Shari´ah na akayakubali lakini akafanya kichenguzi, yanabatilika mambo yote haya. Hapa ni pale ambapo atafanya kitenguzi miongoni mwa vichenguzi vya Uislamu. Mwenye kupinga kwamba swalah sio lazima. Mwenye kupinga kwamba zakaah sio lazima. Mwenye kupinga kwamba kufunga Ramadhaan sio lazima. Mwenye kupinga kwamba kuhiji sio lazima. Mwenye kupinga kufufuliwa na kukusanywa. Mwenye kupinga kwamba Muhammad  ndiye Mtume wa mwisho anakufuru kwa mtazamo wa wote. Akipinga Tawhiyd na asiikubali na akamshirikisha Allaah katika ´ibaadah pamoja na wengine, basi ana haki zaidi na zaidi ya kuwa kafiri na hazitomnufaisha kitu ´ibaadah hizo alizokubali na kuzifanya.

Ni kama ambavyo Maswahabah waliwapiga vita Banuu Haniyfah ilihali wanaswali, wanafunga, wanashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, lakini wakamsadikisha Musaylamah kuwa ni Mtume. Matokeo yake wakakufuru kwa sababu hiyo. Vivyo hivyo yule mwenye kusadikisha Twulayhah al-Asadiy kuwa ni Mtume, al-Aswad al-´Ansiy huko Yemen au Mukhtaar bin Abiy ´Ubaydah ath-Thaqafiy wakati walipodai utume wakakufuru. Waislamu waliwapiga vita. Kutokana na haya inapata kutambulika kuwa yule mwenye kufanya moja katika vichenguzi vya Uislamu basi matendo yake yote yanabatilika. Amesema (Jalla wa ´Alaa):

إِنَّ الَّذِينَ يَكْفُرُونَ بِاللَّـهِ وَرُسُلِهِ وَيُرِيدُونَ أَن يُفَرِّقُوا بَيْنَ اللَّـهِ وَرُسُلِهِ وَيَقُولُونَ نُؤْمِنُ بِبَعْضٍ وَنَكْفُرُ بِبَعْضٍ وَيُرِيدُونَ أَن يَتَّخِذُوا بَيْنَ ذَٰلِكَ سَبِيلًاا

”Hakika wale wanaomkufuru Allaah na Mitume Yake na wanataka kufarikisha baina ya Allaah na Mitume Wake na wanasema: “Tunaamini baadhi na tunawakanusha baadhi” na wanataka kuchukua njia iliyo kati ya hayo… “

Allaah akasema:

أُولَـٰئِكَ هُمُ الْكَافِرُونَ حَقًّا

“Hao ndio makafiri wa kweli.”[2]

Walipotenganisha akaeleza kuwa ni makafiri wa kikweli. Kwa sababu wamewaamini baadhi na wakawakufuru wengine. Kwa mfano wakapatikana watu wenye kusema kuwa wao wanamwamini Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), lakini wakasema kuwa hawaamini kufufuliwa na kukusanywa, hawaamini Pepo, Moto, uwajibu wa swalah, zakaah au uwajibu wa kufunga Ramadhaan. Yote haya ni kuritadi kutoka nje ya Uislamu na kuukufuru. Haijashi kitu hata kama watafanya yenye kulingana na hayo katika mambo mengine ya Uislamu. Kitenguzi kimoja kinatosha kubatilisha yale waliyomo. Kadhalika iwapo watakubali kila kitu lakini wakamtukana Allaah, wakamtukana Mtume, wakaiponda dini au wakacheza shere na dini wanakufuru na ´ibaadah hizo wanazofanya hazitowafaa. Yote haya kwa sababu wamefanya kitenguzi. Amesema (Ta´ala):

وَيُرِيدُونَ أَن يَتَّخِذُوا بَيْنَ ذَٰلِكَ سَبِيلًا

“Wanataka kuchukua njia iliyo baina ya hayo.”

Haya ya kuwaamini baadhi na kuwakufuru wengine ndio yaliyowakafirisha na kuyaporomosha matendo yao. Miongoni mwa hayo ni maneno ya Allaah (Jalla wa ´Alaa):

قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Sema:  Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake?”  Msitoe udhuru; mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.”[3]

Amewakufurisha kwa kucheza kwao shere. Haijashi kitu hata kama wanaswali na wanafunga. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwenye kubadilisha dini yake muueni.”[4]

Kubadilisha dini kwa kufanya moja katika vitenguzi vya Uislamu ni kubadilisha dini. Kwa ajili hii wanachuoni katika madhehebu yote wametenga mlango kuhusu hukumu ya mwenye kuritadi na wakasema kuwa ni yule muislamu mwenye kukufuru baada ya Uislamu wake. Bi maana kwa kufanya moja katika vichenguzi.

[1] Washirikina wa leo.

[2] 04:151

[3] 09:65-66

[4] al-Bukhaariy (2016).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 85-90
  • Imechapishwa: 21/10/2021