25. Kunyanyua mikono katika du´aa ya Qunuut

Swali: Imepokelewa du´aa katika swalah ya Witr:

اللهم اهدِنا فيمَن هديت وعافنا فيمن عافيت وتولنا فيمن توليت وبارك لنا فيما أعطيت وقِنا شر ما قضيت [ف]انك تقضي ولا يقضى عليك [و]اٍنه لا يذل مَن واليت [ولا يعزُ من عاديت]تباركت ربنا وتعاليت لا منجا منك إلا إليك

“Ee Allaah! Niongoze pamoja na Uliowaongoza, nisalimishe pamoja na Uliowasalimisha na nilinde pamoja na Uliowalinda. Tubariki katika kile Ulichotupa na tukinge na shari ya Uliyotuhukumia. Kwani hakika Wewe unahukumu wala huhukumiwi. Hakika hadhaliliki Uliyemlinda, na wala hatukuki Uliyemfanya adui. Umebarikika, ee Mola wetu, na umetukuka. Hakuna mahali pa kuokoka kwengine isipokuwa Kwako.”[1]

Je, mikono inyanyuliwe juu wakati wa kuomba du´aa? Ni yepi yaliyothibiti kutoka kwa mwekaji Shari´ah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?

Jibu: Kunyanyua mikono miwili katika hali ya kuomba du´aa katika du´aa ya Qunuut na nyenginezo ni Sunnah iliyothibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Isipokuwa zile hali ambazo kumepokelewa dalili ya kutonyanyua mikono kama vile baada ya kumaliza zile swalah tano. Kabla ya kutoa salamu au baada ya kutoa salamu hakunyanyuliwi mikono. Vivyo hivyo katika Khutbah ya ijumaa na Khutbah ya ´iyd mbili haifai kwa Khatwiyb kunyanyua mikono yake wakati anapoomba du´aa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa hanyanyui mikono katika Khutbah hizo isipokuwa anapoomba du´aa ya kuteremshiwa mvua. Hapo ndipo alikuwa akinyanyua mikono yake anapoomba du´aa ya kuteremshiwa mvua. Hali kadhalika maamuma wanatakiwa kunyanyua mikono yao pindi imamu anaponyanyua mikono yake katika du´aa ya kuomba kuteremshiwa mvua.

´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz

Swaalih al-Fawzaan

´Abdul-´Aziyz Aalish-Shaykh

Bakr Abu Zayd

[1] Ahmad (1727), Abu Daawuud (1425) na an-Nasaa’iy (1745). Cheni ya wapokezi ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Qiyaam Ramadhwaan, uk. 31-32”.

  • Mhusika: al-Lajnah ad-Daaimah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Swalaat-it-Taraawiyh, uk. 27
  • Imechapishwa: 17/04/2022