114 – Yaziyd bin Haaruun ametuhadithia: Abu Ma´shar ametueleza, kutoka kwa Muhammad Swaalih al-Answaariy, ambaye amesema:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikutana na ´Awf bin Maalik akasema: ”Umeamkaje, ee ´Awf bin Maalik?” Akasema: ”Nimeamka hali ya kuwa ni muumini wa kweli.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Hakika kila msemo una uhakika wake; ni upi uhakika wa hilo?” Akasema: ”Ee Mtume wa Allaah! Nimeyatupilia mbali maisha ya dunia. Ninakesha usiku na nashinda mchana wenye joto nikiwa na kiu. Ni kama kwamba natazama ´Arshi ya Mola wangu. Ni kana kwamba nawatazama watu wa Peponi wakitembeleana humo. Ni kama kwamba nawatazama watu wa Motoni wakipiga makelele na kulia humo.” Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Umejua, basi lazimiana!”[1]

115 – Ibn Numayr ametuhadithia: Maalik bin Mighwal ametueleza, kutoka kwa Zubayd, ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Umeamkaje, ee Haarith bin Maalik?” Akasema: ”Nimeamka hali ya kuwa ni muumini.” Akasema: ”Hakika kila msemo una uhakika wake.” Akasema: ”Nimeamka hali ya kuyatupilia mbali maisha ya dunia. Ninakesha usiku na nashinda mchana nikiwa na kiu. Ni kama kwamba natazama ´Arshi ya Mola wangu, iliyowekwa kwa ajili ya hesabu. Ni kana kwamba nawatazama watu wa Peponi wakitembeleana Peponi. Ni kama kwamba nasikia mayowe ya watu wa Motoni.” Ndipo akasema: ”Mja ambaye Allaah ameing´arisha imani ndani ya moyo wake” au ”Umejua, basi lazimiana!”[2]

116 – Abu Usaamah ametuhadithia, kutoka kwa Muusa bin Muslim: Ibn Saabitw ametueleza na akasema:

”Mara fulani ´Abdullaah bin Rawaahah alikuwa akiwashika mkono marafiki zake na akiwaambia: ”Hebu njooni tuamini kitambo. Njooni tumtaje Allaah na tuzidishe imani zetu.  Hebu njooni tumtaje Allaah kwa kumtii, ili Apate kututaja kwa kutusamehe.”[3]

[1] Dhaifu na kuna Swahabah anayekosekana katika cheni ya wapokezi. Muhammad bin Swaalih al-Answaariy at-Tammaar al-Madaniy alikuwa ni mwanafunzi wa wanafunzi wa Maswahabah. Alikuwa ni mkweli mwenye kukosea, kama ilivyo katika “at-Taqriyb”. Abu Ma´shar Najiyd bin ´Abdir-Rahmaan alikuwa ni dhaifu.

[2] Iko namna hii katika ile ya asili. Katika ”al-Muswannaf” (01/188) imekuja ”Mja ambaye imani imeng´aa ndani ya moyo wake. Ukishajua, basi lazimiana.”

Kuna wapokezi wengi wanakosekana mfululizo. Zubayd alikuwa katika watu wa tabaka la sita ambaye hakukutana na yeyote katika Maswahabah, kama ilivyo katika ”at-Taqriyb” ya Haafidhw. Hata hivyo imepokelewa ikiwa ni pamoja na ´Abd bin Humayd, at-Twabaraaniy na Abu Nu´aym kwa cheni ya wapokezi yenye kuungana kutoka kwa al-Haarith bin Maalik, lakini kwa cheni ya wapokezi dhaifu. Kisha ikapokelewa kupitia njia zingine ambapo baadhi yake kuna Swahabah anayekosekana na zingine cheni yake imeungana. Hakuna nafasi ya kulichambua hilo hapa na hivi sasa.

[3] Cheni ya wapokezi ni dhaifu kwa sababu Ibn Saabitw, ambaye anaitwa ´Abdur-Rahmaan, hakuwahi kukutana na Ibn Rawaahah (Radhiya Allaahu ´anh), ambaye alikufa hali ya kuwa ni shahidi katika vita vya Mu´tah wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiy Shaybah al-Kuufiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 43-44
  • Imechapishwa: 17/07/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy