25. Allaah haridhii kushirikishwa hata na Malaika na Mitume wabora sembuse wengine

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

si Malaika aliyekaribu wala Mtume aliyetumwa.

MAELEZO

Si Malaika aliyekaribu… – Ni yule Malaika mbora kama mfano wa Jibriyl (´alayhis-Salaam), wabebaji wa ´Arshi, walio pambizoni mwake na Malaika walio karibu na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Pamoja na ukaribu wa nafasi zao mbele ya Allaah (´Azza wa Jall), ukaribu wa ´ibaadah na nafasi mbele ya Allaah lau kuna yeyote atawashirikisha pamoja na Allaah katika ´ibaadah basi Allaah haridhii kushirikishwa pamoja Naye; si Malaika aliyekaribu wala Mtume aliyetumwa kama mfano wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ´Iysaa, Nuuh, Ibraahiym ambao ndio Mitume bora. Haridhii kushirikishwa na yeyote ingawa ni katika Mitume bora na japokuwa ni katika watu bora. Hayuko radhi kushirikishwa na yeyote katika Malaika wala Mitume. Tusemeje wengineo katika mawalii na waja wema? Wasiokuwa Malaika na Mitume wana haki zaidi ya kutoridhiwa na Allaah kushirikishwa pamoja Naye katika ´ibaadah. Hapa kuna Radd kwa wale wanaodai kwamba eti wanawafanya waja wema na mawalii kuwa ni waombezi mbele ya Allaah ili wawakurubishe mbele ya Allaah. Watu wa kipindi cha kikafiri walisema:

مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ

“Hatuwaabudu isipokuwa ili wapate kutukurubisha kwa Allaah tumkaribie.”[1]

Vinginevyo walikuwa wakiamini kuwa watu hawa hawaumbi, hawaruzuku, hawamiliki kufisha wala kuhuisha wala kukusanya. Walichokusudia ni wawakalie katikati mbele ya Allaah (´Azza wa Jall). Ndio maana wakawafanyia kitu katika ´ibaadah ili wajikurubishe kwao. Wameyachinjia makaburi, wakayawekea nadhiri makaburi, wakawataka uokozi na kuwaita wafu.

[1] 39:03

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 55-56
  • Imechapishwa: 03/12/2020