Kwa sababu ´ibaadah ya kumwabudu Allaah haiwi ´ibaadah isipokuwa pale ambapo mtu atajiepusha na Twaaghuut, ambayo ni shirki. Amesema (Ta´ala):

فَمَن يَكْفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤْمِن بِاللَّـهِ فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَىٰ لَا انفِصَامَ لَهَا

“Basi atakayemkanusha Twaaghuut na akamuamini Allaah, hakika atakuwa ameshikilia imara kishikilio madhubuti kisichovunjika.”[1]

Kumwamini Allaah hakutoshi isipokuwa pamoja na kukufuru Twaaghuut. Vinginevyo washirikina wanamwamini Allaah lakini hata hivyo wanamshirikisha:

مَا يُؤْمِنُ أَكْثَرُهُم بِاللَّـهِ إِلَّا وَهُم مُّشْرِكُونَ

“Wengi kati yao hawamuamini Allaah isipokuwa wao ni wenye kufanya shirki.”[2]

Amebainisha (Subhaanah) kwamba wanamwamini Allaah lakini hata hivyo wanaiharibu kwa kumshirikisha Allaah. Hii ndio maana ya maneno ya Shaykh:

“Yule mwenye kumwabudu Allaah na akamtii Mtume haifai akamshirikisha Allaah na chochote. Hakika Allaah Haridhii kushirikishwa pamoja Naye yeyote katika ´ibaadah Yake.”

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika yale aliyopokea kutoka kwa Mola Wake (´Azza wa Jall). Allaah (Ta´ala) amesema:

“Hakika Mimi ni Mwenye kujitosheleza kutohitajia washirika. Hivyo basi yule atakayefanya kitendo akanishirikisha Mimi pamoja na mwingine, basi nitamwacha yeye na shirki yake.”[3]

Wako watu ambao wanaswali, wanashuhudia kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, wanayafanya hayo kwa wingi, wanafunga na wanahiji. Lakini wanayaomba makaburi, wanamwabudu al-Hasan, al-Husayn, al-Badawiy na wengineo. Isitoshe wanawataka uokozi wafu. Watu hawa ´ibaadah yao ni batili. Kwa sababu wanamshirikisha Allaah (´Azza wa Jall) na wanaichanganya ´ibaadah yao na shirki. Matendo yao ni batili na yenye kuporomoka mpaka pale watapompwekesha Allaah (´Azza wa Jall), wamtakasie ´ibaadah na waache kuabudu wengine asiyekuwa Yeye. Vinginevyo hawako juu ya lolote. Ni lazima kuzinduka kwa hilo. Allaah hayuko radhi kushirikishwa pamoja Naye katika ´ibaadah Yake yeyote awaye. Hayuko radhi kushirikiana na yeyote yule awaye. Haifai kwa yeyote kusema kwamba yeye anawafanya mawalii na waja wema wazuri kuwa ni waombezi, kwamba yeye hayaabudu masanamu na mizimu, kama ilivyokuwa katika kipindi cha kikafiri, na kwamba yeye anawafanya watu hao kuwa ni waombezi. Tunamwambia: hayo ndio maneno ya watu wa kipindi cha kikafiri ambao walijifanyia waombezi mbele ya Allaah kwa sababu eti ni waja wema na mawalii katika mawalii wa Allaah, jambo ambalo Allaah hayuko radhi nalo.

[1] 02:256

[2] 12:106

[3] Muslim (2985).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 54-55
  • Imechapishwa: 03/12/2020