24. Mlinganizi anatakiwa kukemea ushabiki wa madhehebu

Kwa kumalizia ni kwamba ni lazima kwa mlinganizi wa Kiislamu kulingania katika Uislamu wote na asifarikishe kati ya watu na asifanye ushabiki  na kasumba kwa madhehebu fulani pasi na mengine, kabila fulani pasi na nyingine, Shaykh lake, raisi wake au mtu mwingine. Bali lengo lake liwe kuithibitisha haki na kuiweka wazi na kuwafanya watu wanyooke juu yake ijapo itaenda kinyume na maoni ya fulani.

Walipozuka watu ambao wanafanya ushabiki kwa madhehebu fulani na wanasema kuwa madhehebu fulani ni bora kuliko madhehebu fulani ndipo kukatokea mfarakano na ikhtilafu. Jambo hilo limewapelekea baadhi ya watu kutoswali pamoja na wale wasiokuwa katika madhehebu yake. Ikapelekea ambaye ni Shaafi´iy aswali nyuma ya Hanafiy, Hanafiy haswali nyuma ya Maalikiy wala nyumba na Hanbaliy. Hivi ndivo ilivyotokea kwa baadhi ya wapetukaji mpaka na washabiki. Haya ni majanga na ni kufuata nyayo za shatwaan. Maimamu ni maimamu wa uongofu: Shaafi´iy, Maalik, Ahmad, Abu Haniyfah, al-Awzaa´iy, Ishaaq bin Raahuuyah na mfano wao. Wote hawa ni maimamu wa uongofu na walinganizi wa haki. Waliwalingania watu katika dini ya Allaah na wakawaelekeza katika haki. Hata hivyo kulitokea masuala kadhaa kati yao ambayo walitofautiana kwa sababu ya dalili kujificha kwa baadhi yao. Wale miongoni mwao ambao walijitahidi wakapatia wanapata thawabu mara mbili na wale miongoni mwao ambao walijitahidi wakakosea wanapata thawabu mara moja. Kwa hivyo ni lazima kwako kutambua hadhi na ubora wao, uwatakie rehema na utambue kuwa ni maimamu wa Uislamu na walinganizi wa uongofu. Lakini hilo lisikupelekei kufanya ushabiki na ufuataji wa upofu mpaka ukaona kuwa madhehebu fulani ni aula zaidi kuisibu haki kwa kila hali na kwamba hayakosei. Hili ni kosa. Ni lazima kwako kuitendea kazi haki na kuifuata haki pindi dalili yake inapodhihiri ijapo itaenda kinyume na fulani na fulani. Ni lazima usifanye ushabiki na ukafuata ufuataji wa upofu. Bali unatakiwa kutambua ubora na nafasi ya maimamu. Lakini pamoja na hivo jifanyie mikakati nafsi yako na dini yako na uipokee na kuiridhia haki na uelekeze kwa haki pindi unapoombwa nayo. Sambamba na hayo unatakiwa kumcha Allaah na kumchunga (Jalla wa ´Alaa), ifanyie uadilifu nafsi yako na kuamini kuwa haki ni moja na kwamba wenye kujitahidi wakipatia basi wanapata ujira mara mbili na wakikosea wanapata ujira mara moja. Nakusudia wale wenye kujitahidi Ahl-us-Sunnah na wanazuoni wenye imani na uongofu. Hivyo ndivo yalivyosihi maelezo kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Da´wah ilaa Allaah wa Akhlaaq-id-Du´aah, uk. 39-41
  • Imechapishwa: 14/06/2023