Ni lazima kwako kufanyia kazi Uislamu wote na usichukue baadhi ya sehemu na ukaacha nyingine. Usitendee kazi ´Aqiydah na ukaacha hukumu na matendo. Sambamba na hilo usifanye matendo na hukumu na ukaiacha ´Aqiydah. Bali uchukue Uislamu mzimamzima. Ifanyie kazi ´Aqiydah, matendo, ´ibaadah, jihaad, mkusanyiko, siasa, uchumi na vyenginevyo. Uchukue kwa kila nyanja. Amesema (Subhaanah):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا ادْخُلُوا فِي السِّلْمِ كَافَّةً وَلَا تَتَّبِعُوا خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ ۚ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ

“Enyi mlioamini! Jisalimisheni kikamilifu na wala msifuate hatua za Shaytwaan – hakika yeye kwenu ni adui wa wazi.”[1]

Jopo la Salaf wamesema:

“Maana yake ni kwamba ingia ndani ya Uislamu mzimamzima.”

Maana ya (السلم) ni Uislamu. Kwa sababu ni njia ya usalama na njia ya uokozi duniani na Aakhhirah. Uislamu unalingania katika usalama. Uislamu unalingania kumwaga damu kwa zile hukumu zilizowekwa katika Shari´ah, kisasi na jihaad inayokubalika katika Shari´ah na ya kweli. Ni usalama na Uislamu, amani na usalama. Kwa ajili hiyo amesema (Jalla wa ´Alaa):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا ادْخُلُوا فِي السِّلْمِ كَافَّةً

“Enyi mlioamini! Jisalimisheni kikamilifu… ”

Ingieni katika tanzu zote za imani. Msichukue sehemu na mkaacha sehemu nyingine. Ni lazima kwenu kufanyia kazi Uislamu mzimamzima:

وَلَا تَتَّبِعُوا خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ

”… na wala msifuate hatua za Shaytwaan… ”

Bi maana maasi aliyoharamisha Allaah (´Azza wa Jall). Shaytwaan analingania katika maasi na kuacha dini yote ya Allaah. Yeye ndiye adui mkubwa zaidi. Kwa ajili hiyo ni lazima kwa muislamu kushikamana barabara na Uislamu wote, aamini Uislamu wote, ashikamane na kamba ya Allaah (´Azza wa Jall) na atahadhari na sababu za mfarakano na tofauti katika hali zote. Ni lazima kwako kuhukumu kwa Shari´ah ya Allaah katika mambo ya ´ibaadah, miamala, mambo ya ndoa, mambo ya talaka, mambo ya matumizi, mambo ya unyonyeshaji, katika hali ya usalama na hali ya vita, pamoja na adui na rafiki, mambo ya uhalifu na mengine yote. Ni lazima kuhukumu kwa dini ya Allaah katika kila kitu. Tahadhari usimfanye rafiki na kumpenda ndugu yako kwa sababu tu ameafikiana nawe katika jambo fulani au kumfanya adui na kumchukia kwa sababu ametofautiana nawe katika maoni au suala fulani. Kufanya hivo sio katika uadilifu. Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) walitofautiana katika masuala fulani. Pamoja na hivyo hilo halikuathiri ule usafi wa mioyo waliokuwa nao na halikuathiri katika urafiki na kupendana kwao.

Muumini anatendea kazi Shari´ah ya Allaah, anaamini kwa haki na anaitanguliza mbele kabla ya kila mtu kwa dalili. Hata hivyo hayo hayampelekei kumdhulumu ndugu yake na kutomfanyia uadilifu pindi anapotofautiana naye katika mtazamo katika mambo ya Ijtihaad ambayo wakati mwingine dalili yake inakuwa yenye kufichikana. Vivyo hivyo inahusu katika yale mambo ambayo wakati mwingine kunakuwa na tofauti katika kufasiri andiko lake. Huenda akapewa udhuru. Ni lazima kwako kumnasihi na kumtakia kheri. Hayo yasikupelekei katika uadui na kuleta mpasuko na kummakinisha adui kwako na ndugu yako.

Uislamu ni dini ya uadilifu, dini ya kuhukumu kwa haki na kwa wema na dini ya usawa isipokuwa katika yale mambo yaliyobaguliwa na Allaah (´Azza wa Jall). Uislamu unalingania katika kila kheri, unalingania katika maadili mema, matendo mema, inswafu, uadilifu na kujitenga mbali na kila tabia mbaya. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ اللَّـهَ يَأْمُرُ بِالْعَدْلِ وَالْإِحْسَانِ وَإِيتَاءِ ذِي الْقُرْبَىٰ وَيَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ وَالْبَغْيِ ۚ يَعِظُكُمْ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ

“Hakika Allaah Anaamrishia uadilifu na wemaa na kuwapa [mahitajio na msaada] jamaa wa karibu; na Anakataza machafu na maovu na ukandamizaji. Anakuwaidhini huenda mkapata kukumbuka.”[2]

يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُم مِّن ذَكَرٍ وَأُنثَىٰ وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوبًا وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا ۚ إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّـهِ أَتْقَاكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ

“Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamme na mwanamke na tukakufanyeni kuwa mataifa na makabila ili mtambuane. Hakika aliye mbora zaidi miongoni mwenu mbele ya Allaah ni yule mwenye kumcha Allaah zaidi kati yenu. Hakika Allaah ni Mjuzi, Mwenye khabari za ndani na za nje.”[3]

[1] 02:208

[2] 16:90

[3] 49:13

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Da´wah ilaa Allaah wa Akhlaaq-id-Du´aah, uk. 37-39
  • Imechapishwa: 14/06/2023