Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Muhammad bin ´Abdir-Rahmaan al-Adramiy alisema kumwambia mtu ambaye aliongea kwa Bid´ah na akawalingania watu katika Bid´ah hiyo:

“Je, hakuijua Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Abu Bakr, ´Umar na ´Uthman na ´Aliy au hawakuijua? Yule mtu akasema: “Hapana, hawakuijua.” Akamuuliza: “Kitu ambacho hawakukijua watu hawa umekijua wewe?” Mtu yule akasema: “Basi mimi nasema: “Ndio, walikijua.” Akamuuliza: “Je, yawezekana kweli ikawa hawakukiongelea na wala hawakuwalingania watu juu ya kitu hicho?” Mtu yule akasema: “Ndio, yawezekana.” Akamuuliza tena: “Kitu ambacho hakikuwezekana kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na makhaliyfah zake ukakiweza wewe?” Mtu yule akaangushwa. Kiongozi akasema na alikuwepo hapo: “Allaah asimrehemu yule ambaye hakuweza yale ambayo waliweza wao.”[1]

Namna hii ndivyo inavyokuwa kwa yule ambaye hakuweza yale aliyoweza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Maswahabah zake, wale waliowafuata kwa wema, maimamu baada yao na wale wenye msingi madhubuti katika elimu katika kuzisoma Aayah zinazohusu sifa na kusoma maelezo yake na kuzithibitisha kama zilivyokuja – hivyo Allaah asimrehemu mtu huyo.

MAELEZO

Sijaona wasifu wa ad-Adramiy na wale walio pamoja nao na sijui ni aina gani ya Bid´ah iliyokusudiwa. Kilicho muhimu ni sisi kujua hatua za mahojiano haya ili tupate mbinu za namna ya kuhojiana na wapinzani. al-Adramiy (Rahimahu Allaah) katika mahojiano yake haya ameyajengea ngazi mbalimbali ili kila ngazi amwelezee mpinzani wake inayofuata ili amshinde mpinzani wake huyo:

1 – Utambuzi. al-Adramiy aliuliza kama Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na makhaliyfah zake waliijua Bid´ah hiyo? Mzushi yule akasema kuwa hawakuijua. Ukanushaji huu unapelekea kumtusi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na makhaliyfah zake kwa vile walikuwa hawajui mambo muhimu kuhusu dini. Hata hivyo ni hoja dhidi ya mzushi huyo ikiwa walikuwa hawajui. Kwa ajili hiyo ndio maana al-Adramiy akaenda katika hatua inayofuata:

2 – Wewe umejuaje ikiwa wao walikuwa hawajui? Hivi kweli inawezekana Allaah akamficha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Wake na makhaliyfah zake waongofu utambuzi wa kitu kinachohusu Shari´ah na akakufunulia nacho wewe? Mzushi yule akajirudi na badala yake akasema kuwa walikijua. Ndipo akaenda naye katika hatua nyingine:

3 – Ikiwa waliijua inawezekanaje wasiizungumzie na wasiwaite watu kwayo? Mzushi yule akajibu kuwa iliwezekana kwao kunyamaza na kutozungumza. Ndipo al-Adramiy akamwambia: “Kitu ambacho hakikuwezekana kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na makhaliyfah zake ukakiweza wewe?” Mtu yule akaangushwa na akashindwa kujibu. Kwa sababu mlango umeshafungwa mbele yake. Ndipo kiongozi akasahihisha maoni ya al-Adramiy na akaomba du´aa dhidi ambaye hayakumuwezekania yale yaliyowezekana kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na makhaliyfah zake.

Vivyo hivyo kila mtu wa batili katika wazushi na wengineo ni lazima mwisho wao iwe kushindwa kujibu.

[1] Tazama “Siyar A´laam-in-Nubalaa” (11/314) ya Imaam adh-Dhahabiy (Rahimahu Allaah) na “al-Bidaayah wan-Nihaayah” (1/335) ya Imaam Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 44-47
  • Imechapishwa: 17/10/2022