Ambaye atakula ndani ya Ramadhaan kutokana na sababu inayokubalika katika dini (kama mfano wa zile nyudhuru za kidini ambazo zinamhalalishia yeye kula) au kwa sababu za haramu (kama mfano wa ambaye anaiharibu funga yake kwa kufanya jimaa au kitu kingine), basi atalazimika kulipa. Amesema (Ta´ala):

فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Akamilishe idadi katika siku nyinginezo.”[1]

Inapendekeza kuharakisha kulipa kwa ajili ya kutakasa dhimma yake. Pia inapendeza mtu alipe kwa kufuatanisha. Kwani kulipa kunasimulia kutekeleza. Asipolipa papohapo basi anatakiwa kuazimia kufanya hivo. Inafaa kwake kuchelewesha kwa sababu wakati wake ni wenye wasaa. Kila jambo la wajibu ambao umewekewa muda wenye wasaa inafaa kulichelewesha sambamba na kuliazimia. Aidha inafaa kufunga masiku mbalimbali. Lakini kusipobaki kufika kwa Sha´baan isipokuwa kwa kiwango cha yale masiku anayodaiwa, basi katika hali hiyo analazimika kuyafululiza yote kutokana na ufinyu wa wakati. Haijuzu kuchelewesha mpaka kukaingia Ramadhaan nyingine pasi udhuru. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Nilikuwa nikidaiwa funga ya Ramadhaan na siwezi kuilipa isipokuwa ndani ya Sha´baan. Hili ni kutokana na ile nafasi yangu kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”[2]

Hiyo imejulisha kuwa wakati wa kulipa ni wenye wasaa mpaka pale kutapobaki katika Sha´baan isipokuwa kile kiwango cha masiku anayodaiwa. Hapo atalazimika kuyafunga kabla ya kuingiliwa na Ramadhaan mpya.

[1] 02:184

[2] al-Bukhaariy (1950) na Muslim (2682).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mulakhasw al-Fiqh (01/387-388)
  • Imechapishwa: 05/04/2021