Ni lazima kwa mfungaji ajiepushe na uongo, usengenyi na matusi. Akimtusi mtu basi amjibu kwa kumwambia kuwa amefunga. Baadhi ya watu pengine wakawa na urahisi wa kuacha chakula na kinywaji. Lakini pengine isiwe rahisi kuachana na yale waliyoyazowea katika kuongea na kutenda vitu vibaya. Kwa ajili hiyo baadhi ya Salaf wamesema:

“Funga sahali ni kuacha chakula na kinywaji.”

Kwa hivyo ni lazima kwa muislamu kumcha Allaah, kumwogopa na kuhudhurisha ukubwa wa Mola wake na kwamba anamuona katika kila kipindi na katika kila hali. Matokeo yake aichunge swawm yake kutokamana na vifunguzi na vitu vyenye kuipunguza ili funga yake iwe sahihi.

Mfungaji anatakiwa kujishughulisha na kumtaja Allaah, kusoma Qur-aan na kuswali kwa wingi swalah zilizopendekezwa. Salaf walipokuwa wanafunga basi hukaa misikitini na wakisema kuwa wanahifadhi swawm zao na hawamsengenyi yeyote. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule asiyeacha maneno ya uongo, kuyatendea kazi na ujinga, basi Allaah hana haja kwa yeye kuacha chakula na kinywaji chake.”[1]

Hilo ni kwa sababu kunakamilika kumwabudu Allaah kwa kuacha matamanio haya yaliyoruhusiwa katika kipindi kisichokuwa cha funga isipokuwa baada ya kujikurubisha Kwake kwa kuacha yale ambayo Allaah amemuharimishia katika kila hali ambavyo ni uongo, dhuluma na kuwashambulia watu katika damu, mali na heshima zao. Abu Hurayrah amepokea kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Mfungaji yuko katika ´ibaadah muda wa kuwa hajamsengenya au akamuudhi muislamu.”[2]

Anas amesema:

“Hakufunga yule ambaye kazi yake ni kula nyama za watu.”[3]

Mfungaji huacha mambo yaliyokuwa halali kwake katika kipindi ambacho hakikuwa cha yeye kufunga. Kwa hivyo ana haki zaidi ya kuacha yale mambo ambayo si halali kwake katika kipindi chote ili aingie miongoni mwa wale wenye kufunga kikweli.

[1] al-Bukhaariy (1903).

[2] ad-Daylamiy (01/302). Pia ameipokea Ibn Abiy Shaybah kutoka katika maneno ya Abul-´Aaliyah (8889).

[3] Ibn Abiy Shaybah kupitia kwa Anas kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) (8890).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mulakhasw al-Fiqh (01/386)
  • Imechapishwa: 05/04/2021