24. Kitu cha kwanza ambacho tutafanyiwa hesabu kwacho

109 – Wakiy´ ametuhadithia: al-A´mash ametueleza, kutoka[1] kwa Sulaymaan bin Maysarah na al-Mughiyrah bin Shibl, kutoka kwa Twaariq bin Shihaab al-Ahmasiy, kutoka kwa Salmaan, ambaye amesema:

”Mfano wa swalah tano ni kama vile mishale ya ngawira. Yule anayepiga kwa minne ni bora kuliko anayepiga kwa mitatu. Yule anayepiga kwa mitatu ni bora kuliko anayepiga kwa mishale miwili. Anayepiga kwa mishale miwili ni bora kuliko anayepiga kwa mshale mmoja. Allaah hamfanyi yule ambaye ana mshale ndani ya Uislamu kuwa sawa na ambaye hana mshale.”

110 – Ibn Fudhwayl ametukhabarisha, kutoka kwa Layth[2], kutoka kwa ´Amr bin Murrah, kutoka kwa al-Baraa’, ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Kishikilio imara zaidi cha Uislamu ni kupenda kwa ajili ya Allaah na kuchukia kwa ajili ya Allaah.”

111 – Ibn Numayr ametuhadithia, kutoka kwa Maalik bin Mighwal, kutoka kwa Zubayd, kutoka kwa Mujaahid, ambaye amesema:

”Kishikilio imara zaidi cha Uislamu ni kupenda kwa ajili ya Allaah na kuchukia kwa ajili ya Allaah.”

112 – Yaziyd bin Haaruun ametuhadithia: Daawuud bin Abiy Hind ametueleza, kutoka kwa Zuraarah bin Awfaa, kutoka kwa Tamiym ad-Daariy, ambaye amesema:

”Kitu cha kwanza atachofanyiwa kwacho hesabu mja siku ya Qiyaamah ni swalah ya faradhi. Ima awe ameitimiza na vinginevyo kutasemwa: ”Tazameni kama yuko na swalah za kujitolea.” Hivyo swalah ya faradhi ikamilishwe na swalah zake za kujitolea. Na isipokamilishwa swalah ya faradhi yake na asiwe na swalah za kujitolea, basi atashikwa viungo vyake na kutupwa Motoni.”[3]

113 – Hushaym ametukhabarisha mfano wa Hadiyth ya Yaziyd: Daawuud ametueleza, kutoka kwa Zuraarah, kutoka kwa Tamiym, isipokuwa yeye hakutaja ”basi atashikwa viungo vyake na kutupwa Motoni.”[4]

[1] Imekuja katika ile ya asili ”na Sulaymaan”. Masahihishwo yamefanywa baada ya ”al-Muswannaf” na vitabu vya nyasifu. Sulaymaan huyu ni mwaminifu. Wapokezi wengine ni waaminifu na ni wanamme wa Muslim. Cheni ya wapokezi kwenda mpaka kwa Salmaan ni Swahiyh.

[2] Alikuwa anaitwa Layth bin Abiy Sulaym na alikuwa dhaifu. Ahmad (4/286) ameipokea kupitia njia nyingine, kutoka kwa ´Amr bin Murrah, kutoka kwa Mu´aawiyah bin Suwayd bin Muqrin, kutoka kwa al-Baraa’.

[3] Cheni ya wapokezi ni Swahiyh.

[4] Cheni ya wapokezi ni Swahiyh. Hammaad bin Salamah ameipokea kutoka kwa Abu Daawuud bin Abiy Hind, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye amesema:

”Kitu cha kwanza ambacho mja atafanyiwa hesabu kwacho siku ya Qiyaamah ni swalah yake. Ikiwa ameikamilisha, basi itaandikwa kama imekamilika. Na kama hakuikamilisha, basi Allaah atawaambia Malaika wake: ”Tazameni kama mja Wangu yuko na swalah za kujitolea mkamilishe kwazo kile alichopoteza katika swalah yake ya faradhi.” Kisha kufuatie zakaah. Halafu kufuatie matendo mengine kama hivo.”

Ameipokea Ibn Maajah (1426) na Ahmad (4/103). Cheni ya wapokezi ni Swahiyh.

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiy Shaybah al-Kuufiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 42
  • Imechapishwa: 16/07/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy