Hadiyth ya tisa

يَوْمَ نَقُولُ لِجَهَنَّمَ هَلِ امْتَلَأْتِ وَتَقُولُ هَلْ مِن مَّزِيدٍ

“Siku Tutakapoiambia Jahannam: “Je, umeshajaa?” Nayo itasema: “Je, hakuna ziada yoyote?”[1]

106 – Nilimsomea Haafidhw Abul-Husayn ´Aliy bin Muhammad al-Yuuniynuy huko Baalbek na Abul-´Abbaas Ahmad bin ´Abdil-Hamiyd al-Maqdisiy huko Dameski: ´Abdullaah bin ´Umar bin ´Aliy al-Baghdaadiy ametuhadithia… Abul-´Abbaas amenizidishia akasema: Muusa bin Shaykh ´Abdul-Qaadir al-Jiyliy ametuhadithia: ´Abdul-Awwal bin ´Iysaa as-Sijziy ametuhadithia: ´Abdur-Rahmaan bin Muhammad ad-Daawuudiy ametuhadithia: Abu Muhammad bin Hammuuyah as-Sarkhasiy ametuhadithia: Ibraahiym bin Khuzaym ash-Shaashiy ametuhadithia: ´Abd bin Humayd ametuhadithia: Yuunus bin Muhammad ametuhadithia: Sufyaan ametuhadithia, kutoka kwa Qataadah: Anas bin Maalik ametuhadithia ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Moto utaendelea kusema:

هَلْ مِن مَّزِيدٍ

“Je, hakuna ziada yoyote?”[2]

mpaka Mola wa utukufu aweke unyayo Wake juu yake ambapo utasema: “Tosha, tosha.”[3]

Hadiyth hii ni Swahiyh. Maswahabah wengi wameisimulia kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), akiwemo Anas, Abu Hurayrah, Hudhayfah bin al-Yamaan na Abu Sa´iyd al-Khudriy. Abu Hurayrah ameipokea kwa tamko lisemalo:

”… mpaka Mola wa utukufu aweke unyayo Wake juu yake… “

Imekuja katika tamko lingine lisemalo:

”… mpaka Mola wa utukufu aweke mguu Wake juu yake… “

Zote hizi zimepokelewa katika ile Swahiyh.

107 –  Ibn ´Abbaas, Ibn Mas´uud, Abu Muusa na Maswahabah wengine wamesema:

al-Kursiy ni mahali pa kuweka miguu Yake (´Azza wa Jall).”[4]

Mfano wa hayo yamepokelewa kutoka kwa Wahb bin Munabbih.

108 – Mujaahid amesema:

”Siku ya Qiyaamah Allaah atasema kumwambia Daawuud: ”Chukua unyayo Wangu.” Hivyo achukue mguu Wake.”

109 – ´Urwah amesema:

”Nilifika kwa ´Abdul-Malik bin Marwan na nikamtajia mwamba ulioko Yerusalemu. Akasema: ”Huo ndio ule mwamba ambao Mwingi wa rehema aliweka juu yake mguu Wake.” Nikasema: ”Allaah ametakasika kutokana na mapungufu! Allaah anasema:

وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ

“Imeenea Kursiy Yake mbingu na ardhi.”[5]

na wewe unasema kuwa Aliweka mguu Wake juu yake. Allaah ametakasika kutokana na mapungufu! Allaah ametueleza kuwa mlima huo atausagasaga.”

110 – as-Suddiy ameeleza kuwa Abu Maalik amesema:

al-Kursiy iko chini ya ´Arshi. Allaah anaweka miguu Yake juu ya al-Kursiy.

111 – al-Athram amesema:

”Nilikuwa katika tukio moja ambalo bwana mmoja anasimulia Hadiyth inayosema kuwa Mwingi wa huruma ataweka mguu Wake juu ya Moto. Kulikuwepo mvulana. Mvulana yule akanigeukia na kusema: ”Hadiyth hii ina tafsiri yake.” Ndipo Abu ´Abdillaah akasema: ”Mtazame! Anasema vilevile kama wanavosema Jahmiyyah.”

112 – al-Marruudhiy amesema:

”Nilimuuliza Abu ´Abdillaah kuhusu Hadiyth:

“Moto utaendelea kusema:

هَلْ مِن مَّزِيدٍ

“Je, hakuna ziada yoyote?”[6]

mpaka Mola wa utukufu aweke unyayo Wake juu yake ambapo utasema: “Tosha, tosha.” Akajibu: “Tunazipitisha kama zilivyokuja.”

Ameipokea Ibn Battwah katika ”al-Ibaanah”.

[1] 50:30

[2] 50:30

[3] al-Bukhaariy (4848), Muslim (2188), Ahmad (3/129), at-Tirmidhiy (3272), an-Nasaa’iy katika ”al-Kubraa” (7719), ad-Daarimiy katika ”ar-Radd ´alaa Bishr al-Mariysiy, uk. 69, al-Bayhaqiy katika ”al-Asmaa’ was-Swifaat”, uk. 348-349, Ibn Khuzaymah katika ”at-Tawhiyd”, uk. 92-93, na Ibn Mandah katika ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah”, uk. 42, ambaye amesema:

”Hadiyth imethibiti kwa maafikiano.”

[4] al-Haakim amesema:

”Swahiyh kwa sharti za al-Bukhaariy na Muslim.” (al-Mustadrak (2/282))

adh-Dhahabiy amesema:

”Wapokezi wake ni wenye kuaminika.” (al-´Uluww, uk. 61)

al-Azhariy amesema:

”Wanazuoni wameafikiana juu ya usahihi wa mapokezi haya.” (Tahdhib-ul-Lughah (10/61))

[5] 2:255

[6] 50:30

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy (afk. 748)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Arba´iyn fiy Swifaati Rabb-il-´Aalamiyn, uk. 110-115
  • Imechapishwa: 09/06/2024