23. Kinachofanya msibiwaji kukosa malipo yake

Msibiwaji anatakiwa kuhadhari kwelikweli kusema kitu katika mnasaba wa msiba na wakati wa kulia kwake kwa kitu kitachosababisha kuharibu malipo yake na kumkasirisha Mola wake. Jambo hilo linaweza kwa mfano akaonelea kuwa amedhulumiwa. Allaah (Ta´ala) ni mwadilifu na wala hadhulumu. Ni mjuzi na wala hakosei na wala sio mjinga wa kutokijua kitu. Ni mwenye hekima na matendo Yake yote ni yenye hekima na yenye manufaa. Hafanyi kitu isipokuwa kwa hekima. Kila kile anachokitoa (Subhaanah) ni Chake na ni Chake vilevile kile anachokichukua. Hatoulizwa kwa yale anayoyafanya na wao wataulizwa. Anafanya alitakalo. Yeye ni muweza wa kila jambo. Uumbaji na maamrisho ni Yake.

Mwenye kusibiwa anatakiwa kusema yale yenye kumridhisha Mola wake na kufanya matendo Yake yaongezeke. Ibn Abiy-Dunyaa amepokea kwa mlolongo wa wapokezi wake kutoka kwa Yuunus bin Muhammad al-Makkiy ambaye amesema:

“Kuna mwanaume mmoja kutoka Twaa-if alipanda mpando. Ulipokuwa mkubwa ukashikwa na ugonjwa na ukaunguwa. Tukaenda kumliwaza. Akalia na kusema: “Ninaapa kwa Allaah ya kwamba silii kwa sababu yake. Ninalia kwa sababu nimemsikia Allaah (Ta´ala) akisema:

مَثَلُ مَا يُنفِقُونَ فِي هَـٰذِهِ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا كَمَثَلِ رِيحٍ فِيهَا صِرٌّ أَصَابَتْ حَرْثَ قَوْمٍ ظَلَمُوا أَنفُسَهُمْ فَأَهْلَكَتْهُ ۚ وَمَا ظَلَمَهُمُ اللَّـهُ وَلَـٰكِنْ أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ

“Mfano wa vile wanavyovitoa katika uhai wao huu wa duniani ni kama mfano wa upepo ndani yake mna baridi ya barafu, ukasibu shamba lilolimwa la watu waliojidhulumu nafsi zao ukaliangamiza. Allaah Hakuwadhulumu lakini wamejidhulumu nafsi zao.” (03:117)

Ninachelea nisije kuwa miongoni mwa watu hawa. Hilo ndilo lililoniliza.”

Mja ahadhari asiombe dhidi ya nafsi yake. Pindi Abu Salamah alipofariki Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema:

“Msiombe dhidi ya nafsi zenu isipokuwa tu kheri. Kwani hakika Malaika huitikia “Aamiyn” kwa yale mnayoyasema.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 42-44
  • Imechapishwa: 14/10/2016