22. Kuoanisha baina ya dalili zinazokataza kulia na zinazojuzisha kulia baada ya mtu kufa

Kuhusu yale waliyotaja watu wa ash-Shaafi´iy na wale wengine waliosema kuwa imechukizwa kulia baada ya kufa na kutumia dalili kwa zile Hadiyth zilizotajwa, zote zinatakiwa kufasiriwa kuwa ni kulia kulikoambatana na maobolezo. Hilo linatiliwa nguvu na Hadiyth “Hakika maiti anaadhibiwa kwa familia yake kumlilia” na katika matamshi mengine imekuja “Hakika maiti anaadhibiwa kwa familia yake kumlilia… “

Kuhusu madai ya kwamba Hadiyth ya Hamzah imefuta kulia kunakoruhusiwa baada ya wauliwaji wa vita vya Uhud, sio sahihi. Kwa kuwa Hadiyth nyingi zinazoruhusu kulia baada ya kufa zimejitokeza baada ya vita vya Uhud. Miongoni mwazo ni Hadiyth ya Abu Hurayrah. Alisilimu katika mwaka wa saba. Kadhalika kulia kwa ajili ya Zaynab ambaye alikufa mwaka wa nane. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alilia kwenye kaburi la mama yake mwaka ulipotekwa mjia wa Makkah.

Ama kuhusiana na hoja yao kwamba inajuzu tu kulia kabla ya kufa kama hadhari, ikiwa mtu analia kabla ya kufa kwa sababu ya huzuni basi baada ya kufa huzuni wake unakuwa mkubwa zaidi. Kwa sababu kabla ya kufa mtu daima anaweza kuwa na matumaini ya kuendelea kuishi. Ama baada ya kufa matumaini yote yameondoka. Hapo kunaliliwa kwa ajili ya mfarakano usiorudi maishani katika dunia. Hii ndio maana ya maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika macho hutokwa na machozi na moyo huingiwa na huzuni na wala hatusemi isipokuwa yale yenye kumridhisha Mola wetu.”

Kadhalika al-Bukhaariy amepokea kwamba ´Umar amesema:

“Waache walie kwa ajili ya Abu Salmaan midhali udongo hauwekwi kichwani wala hakupigwi kelele.”

Baadhi ya wanachuoni wanasema kulia kulikopokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ambako amekuruhusu na amekupendekeza ni kulia kunakopelekea kutoa machozi na moyo kuwa mlaini na wenye huruma na kulia ambako (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekukataza ni kulia kwa mayowe na kuomboleza. Kinachotilia nguvu haya ni maneno yake ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ama kile kinachotoka kwenye macho na moyo kinatoka kwa Allaah ( Azza wa Jall) na huruma. Na kile chenye kutoka kwenye mkono na ulimi ni kutoka kwa shaytwaan.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 41-42
  • Imechapishwa: 14/10/2016