21. Dalili za kwamba inafaa kulia baada ya mtu kufa

Watu wetu – Hanaabilah – na wale walio na maoni yao ambao wamejuzisha kulia kabla ya kufa na baada yake wametumia hoja kwa maneno ya Jaabir bin Abdillaah (Radhiya Allaahu anhumaa):

“Baba yangu aliuawa siku ya Uhud. Nikawa namuondosha kitambaa usoni mwake na huku nalia. Wakanikataza mbali na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) akawa hanikatazi. Shangazi yangu Faatwimah akaanza kulia. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) akasema: “Sawa ukilia au usilie Malaika watamfunika kwa mbawa zao mpaka mtapomnyanyua.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Ibn Umar amesema:

“Pindi Sa d bin Ubaadah alipozama Mtume (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) alikuja kumtembelea akiwa pamoja na Abdur-Rahmaan bin Awf, Sa d bin Abiy Waqqaas na Abdullaah bin Mas uud. Wakamkuta amezimia. Mtume (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) akauliza: “Amekufa?” Wakasema: “Hapana, ee Mtume wa Allaah.” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) akaanza kulia. Pindi watu walipoona namna Mtume (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) anavyolia nao pia wakaanza kulia. Akasema: “Hamsikii?” Allaah haadhibu kwa machozi ya macho au kwa huzuni wa moyo. Anaadhibu au kurehemu kwa hichi” na akaashiria ulimi.”

Ameipokea al-Bukhaariy na ni matamshi yake.

Usaamah bin Zayd amesema:

“Tulikuwa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) pindi mmoja katika wasichana zake alipomtumia mjumbe kumweleza kuwa mtoto wake amefariki. Akamwambia yule mjumbe: “Rudi umwambie kuwa ni cha Allaah kile Alichokitoa na kukichukua na kila kitu Kwake kina muda maalum. Mwamrishe awe na subira na atarajie malipo kutoka kwa Allaah.” Baada ya hapo yule mjumbe akarudi na kusema: “Ninaapa unatakiwa uje kwake.” Mtume (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) akasimama akiwa pamoja na Sa´d bin ´Ubaadah, Mu´aadh bin Jabal, ´Ubayy bin Ka´b, Zayd bin Thaabit pamoja na mimi. Mtoto mdogo akaja anamkimbilia na moyo wake unagonga utafikiri ni chupa dogo. Machozi yakamlenga. Sa d akamwambia: “Ee Mtume wa Allaah! Ni nini?” Akasema: “Ni huruma ambao Allaah ameuweka kwenye mioyo ya waja. Allaah anawahurumia katika waja Wake wale wenye kuhurumia.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu anh) amesema:

“Tulikuwa katika moja ya mazishi ya wasichana zake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi wa sallam). Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) akakaa karibu na kaburi. Nikaona macho yake yamejaa machozi. Akasema: “Ni nani katika yenu hakufanya jimaa usiku?” Abu Twalhah akasema: “Mimi.” Akasema (Swalla Allaahu alayhi wa sallam): “Muweke ndani ya kaburi lake.”

Ameipokea al-Bukhaariy.

Anas ameeleza pia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) amesema:

“Nilipata mvulana ambaye nilimpa jina la baba yangu Ibraahiym… “

Akaendelea kusimulia Hadiyth mpaka aliposema:

“Baada ya hapo tukamtembelea na Ibraahiym alikuwa katika hali ya umaututi. Macho ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) yakaacha kububujikwa na machozi.” Abdur-Rahmaan bin Awf na Anas wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Hivi unalia na wewe ndiye ulikataza mtu kulia?” Akasema: “Ee mwana wa Awf! Hakika ni huruma na yule asiyehurumia hahurumiwi. Hakika macho hutokwa na machozi na moyo huingiwa na huzuni na wala hatusemi isipokuwa yale yenye kumridhisha Mola wetu. Ee Ibraahiym! Hakika sisi ni wenye kuhuzunika kwa kutengana na wewe.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim. Hapa kuna dalili ya kufaa kulia kabla ya kufa.

Anas (Radhiya Allaahu anh) amesema vilevile:

“Zayd alishika bendera akauawa. Baada ya hapo ikashika Abdullaah bin Rawaahah akauawa. Baada ya hapo ikashika Ja far akauawa na macho ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) yakabubujikwa na machozi. Baada ya hapo ikashika Khaalid bin Waliyd pasi na amri yake na akashinda.”

Ameipokea al-Bukhaariy.

Ibn Abbaas (Radhiya Allaahu anhumaa) amesema:

“Msichana wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi wa sallam), Zaynab, alifariki na wanawake wakaanza kulia. Umar akaanza kuwapiga kwa bakora yake. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) akamshika mkono na kumwambia: “Tulia, ee Umar! Ninakutahadharisheni wanawake na mayowe yenu ya shaytwaan!” Kisha akasema (Swalla Allaahu alayhi wa sallam): “Ama kile kinachotoka kwenye macho na moyo kinatoka kwa Allaah ( Azza wa Jall) na huruma. Na kile chenye kutoka kwenye mkono na ulimi ni kutoka kwa shaytwaan.”

Ameipokea Imaam Ahmad.

Aaishah (Radhiya Allaahu anhaa) ameeleza kuwa pindi Sa d bin Mu aadh alipofariki Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) na Abu Bakr na Umar (Radhiya Allaahu anhumaa) walimjia. Aaishah amesema:

“Ninaapa kwa Yule ambaye moyo wangu uko mkononi Mwake! Niliweza kutafautisha kati ya kilio cha Abu Bakr na kilio cha Umar ilihali nilikuwa chumbani mwangu.”

Ameipokea Ahmad.

Asmaa bint Yaziyd amesema:

“Pindi mtoto wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) Ibraahiym alipofariki Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) alilia.”

Ameipokea Ibn Maajah.

Imaam Ahmad amepokea vilevile kutoka kwa Ibn Abbaas (Radhiya Allaahu anhumaa) ambaye amesema:

“Pindi msichana wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) Ruqayyah, alipofariki alisema: “Jiunge na wawakilishi wetu wema Uthmaan bin Madh uun.” Wanawake wakalia mpaka Umar akawapiga kwa bakora yake. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) akasema. “Waache walie. Ninakutahadharisheni wanawake na mayowe ya shaytwaan!” Kisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) akasema: “Ama kile kinachotoka kwenye macho na moyo kinatoka kwa Allaah ( Azza wa Jall) na huruma. Na kile chenye kutoka kwenye mkono na ulimi ni kutoka kwa shaytwaan.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) akakaa chini pembezoni na kaburi. Karibu yake alikuwepo Faatwimah akilia. Akampangusa macho yake kwa kitambara chake kwa sababu alikuwa akimuonea huruma.”

Katika Hadiyth hizo mbili kuhusu kufa kwa Zaynab na Ruqayyah kumethibiti kulia baada ya kufa. Kuna mapokezi mengi juu ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) alitembelea kaburi la mama yake na akalia na akawafanya wengine vilevile waliokuwepo pale kulia. Imesihi pia kuwa (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) alimbusu maiti Uthmaan bin Madh uun mpaka machozi yakamtiririka usoni mwake. Kisa cha Ja far na Abdullaah bin Rawaahaan kimeshatangulia.

Kadhalika imesihi kwamba Abu Bakr asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu anh) alimbusu Mtume (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) baada ya kufa kwake na akalia na akawafanya wengine pia wakaanza kulia. Aliy (Radhiya Allaahu anh) pia alilia baada ya Mtume (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) kufa.

Hadiyth zote hizi zinafahamisha kuwa inajuzu kulia kabla na baada ya mtu kufa na kwamba haichukukizwa kabisa.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 38-41
  • Imechapishwa: 14/10/2016