20. Dalili za kwamba haifai kulia baada ya mtu kufa

Kulia ni huruma kwenye mioyo ya waja. Kwa mujibu wa madhehebu ya Ahmad na Abu Haniyfah inajuzu kulia kabla mtu hajakufa na baada ya kufa. Maoni haya yamepokelewa vilevile na Abu Ishaaq ash-Shiyraaziy.

ash-Shaafi´iy na wengine wengi katika madhehebu yake wamechukiza hilo baada ya mtu kufa ilihali wameliruhusu kabla ya roho ya mtu kutoka. Dalili yao kwa hilo ni ile Hadiyth kutoka kwa Jaabir bin ´Atiyk (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimtembelea ´Abdullaah bin Thaabit na kumtazama hali ya kuwa amezimia. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwita, lakini hakumuitikia. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Sisi ni wa Allaah na Kwake ndiko tutarejea”. Wanawake wakaanza kupiga mayowe na kulia ilihali huku Ibn ´Atiyk anawanyamazisha. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Waache. Pindi itapokuwa ni wajibu hawatolia tena.” Wakauliza: “Wajibu ni kitu gani?” Akasema: “Mauti.”

Imepokelewa na Imaam Ahmad, Abu Daawuud, an-Nasaa´iy na Ibn Maajah na matamshi ni ya Abu Daawuud.

Wamesema pia kuwa al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Maiti huadhibiwa kwa kule familia yake kulia kwa ajili yake.”

Wamesema kuwa haya yanapatikana baada ya kufa na kwamba mtu hazingatiwi kuwa ni maiti kabla ya kufa.

Kadhalika imepokelewa kutoka kwa Ibn ´Umar namna ambavyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwasikia wanawake kutoka Banuu ´Abdil-Ashhal wanavyolia kwa wauliwa wao baada ya vita vya Uhud. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Hakuna yeyote anayelia kwa ajili ya Hamzah.” Ndipo wanawake kutoka Answaar wakalia kwa ajili ya Hamzah mbele yake. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaamka na kusema:

“Ole wao! Wanalia hapa. Wanasikitisha! Waombeni warudi. Kuanzia hii leo asiwepo yeyote atayelia kwa ajili ya maiti.”

Imepokelewa na Imaam Ahmad na Ibn Maajah.

Hii ni dalili ya wazi yenye kuonesha ya kwamba ile hali ya kwanza imefutwa. Tofauti kati ya kulia kabla kufa na baada ya kufa ni kuwa kulia kabla ya kufa ni kwa sababu mtu ana matumaini ya kuendelea kueshi. Katika hali hii kulia kwa ajili yake ni hadhari. Ama baada ya kufa kunakuwa hakuna matumaini. Kwa hivyo kunakuwa hakuna manufaa yoyote kwa kule kulia.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 37-38
  • Imechapishwa: 14/10/2016