23. Allaah haridhii kushirikishwa pamoja Naye yeyote katika ´ibaadah Yake

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

La pili: Hakika Allaah haridhii kushirikishwa pamoja Naye yeyote katika ´ibaadah Yake;

MAELEZO

Suala hili limefungamana na suala la kwanza. Kwa sababu suala la kwanza linabainisha ulazima wa kumwabudu Allaah na kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hiyo ndio maana ya kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah.

Suala la pili ni kwamba ´ibaadah ikichanganyikana na shirki haikubaliwi. Ni lazima ´ibaadah iwe imefanywa kwa ajili ya kutafuta uso wa Allaah (´Azza wa Jall) pekee. Kwa hiyo yule mwenye kumwabudu Allaah na wakati huohuo akamwabudu mwengine basi ´ibaadah yake ni batili. Upatikani wake ni sawa na ukosekanaji wake. Kwa sababu ´ibaadah hainufaishi isipokuwa pamoja na Ikhlaasw na Tawhiyd. Ikichanganyikana na shirki basi inaharibika. Amesema (Ta´ala):

وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ

“Hakika umefunuliwa Wahy na kwa wale walio kabla yako kwamba: “Ukifanya shirki bila shaka yataporomoka matendo yako na hakika utakuwa miongoni mwa waliokhasirika.”[1]

وَلَوْ أَشْرَكُوا لَحَبِطَ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Lau wangemshirikisha bila shaka yangeporomoka yale waliyokuwa wakitenda.”[2]

´Ibaadah haiitwi ´ibaadah isipokuwa ikiambatana na  Tawhiyd kama ambavo swalah haiitwi kuwa ni swalah isipokuwa ikiambatana na twahara. Shirki ikichanganyikana na ´ibaadah inaiharibu. Ni kama ambavo twahara ikichanganyikana na moja katika vichenguzi vya wudhuu´ basi inaiharibu na kuibatilisha. Kwa ajili hiyo ndio maana utaona Allaah katika Aayah nyingi anakusanya kati ya amri ya kumwabudu Yeye na makatazo ya shirki. Amesema (Ta´ala):

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا

“Mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe Yeye na chochote.”[3]

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamuabudu Allaah pekee hali ya kumtakasia yeye dini, wenye kupondoka kwenye haki na kuiacha batili.”[4]

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ

“Hatukutuma kabla yako Mtume yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: “Hakika hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Mimi; hivyo basi niabuduni.”[5]

Maneno Yake (Ta´ala):

لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ

“Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Mimi; hivyo basi niabuduni.”

kuna amri mbili:

1- Kuna makanusho ya shirki.

2- Kuna kumthibitishia ´ibaadah Allaah (Ta´ala).

Amesema (Ta´ala):

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ

“Mola wako ameamuru kwamba: “Msiabudu yeyote isipokuwa Yeye pekee.”[6]

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

”Hakika Tulituma katika kila ummah Mtume kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na Twaaghuut [waungu batili].”[7]

Kumeambatanishwa kati ya kumwabudu Allaah na kuepuka Twaaghuut.

[1] 39:65

[2] 06:88

[3] 04:36

[4] 98:05

[5] 21:25

[6] 17:23

[7] 16:36

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 52-54
  • Imechapishwa: 02/12/2020