22. Adhabu ya wenye kumuasi Muhammad ni kubwa zaidi kuliko ya watu wa Muusa

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Amesema (Ta´ala):

إِنَّا أَرْسَلْنَا إِلَيْكُمْ رَسُولًا شَاهِدًا عَلَيْكُمْ كَمَا أَرْسَلْنَا إِلَىٰ فِرْعَوْنَ رَسُولًا فَعَصَىٰ فِرْعَوْنُ الرَّسُولَ فَأَخَذْنَاهُ أَخْذًا وَبِيلًا

“Hakika Sisi Tumekutumieni Mtume awe ni shahidi juu yenu, kama Tulivyotuma kwa Fir’awn Mtume. Lakini Fir’awn alimuasi huyo Mtume, Tukamuadhibu adhabu kali sana.”[1]

Mtume ni Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Fir´awn alikuwa ni mfalme mjeuri huko Misri ambaye alidai kuwa ni mola. Fir´awn ilikuwa ni jina la utani la kila mfalme Misri alikuwa akiitwa Fir´awn. Makusudio hapa ni yule Fir´awn aliyedai kuwa ni mola:

فأَنَا رَبُّكُمُ الْأَعْلَىٰ

“Mimi ni mola wenu mkuu.”[2]

Fir’awn alimuasi huyo Mtume – Bi maana Muusa. Alimkufuru Muusa, kama Allaah alivyotusimulia ndani ya Kitabu Chake yaliyopitika kati ya Muusa na Fir´awn na yalivyoishilia mambo ya Fir´awn na watu wake.

Tukamuadhibu – Fir´awn akaadhibiwa ambapo Allaah akamzamisha yeye na watu wake ndani ya maji kisha akawaingiza Motoni:

مِّمَّا خَطِيئَاتِهِمْ أُغْرِقُوا فَأُدْخِلُوا نَارًا

“Kutokana na hatia zao basi walizamishwa kisha wakaingizwa Motoni.”[3]

Akaingia Motoni kwenye tabaka la chini kabisa. Amesema (Ta´ala):

النَّارُ يُعْرَضُونَ عَلَيْهَا غُدُوًّا وَعَشِيًّا

“Moto unadhihirishwa kwao asubuhi na jioni… ”

Hali hii ni ndani ya kaburi kabla ya Aakhirah. Wanaonyeshwa Motoni asubuhi na jioni mpaka Qiyaamah kisimame. Hii ni dalili juu ya adhabu ya ndani ya kaburi:

وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ أَدْخِلُوا آلَ فِرْعَوْنَ أَشَدَّ الْعَذَابِ

“… na Siku itakayosimama Saa [kutasemwa]: “Waingizeni watu wa Fir’awn katika adhabu kali kabisa.”[4]

Hizi ni adhabu tatu:

1- Allaah aliwazamisha na akawatokomeza mpaka wa mwisho wao kwa mkupuko mmoja.

2- Wanaadhibiwa ndani ya kaburi mpaka kisimame Qiyaamah.

3- Watapofufuliwa siku ya Qiyaamah wataingia adhabu kali zaidi.

Vivyo hivyo wale wenye kumuasi Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mwisho wao  ni mbaya zaidi kuliko mwisho wa watu wa Fir´awn. Kwa sababu Muhammad ndiye Mtume bora. Kwa hivyo yule mwenye kumuasi adhabu yake itakuwa kubwa zaidi.

Adhabu kali sana – Isiyokuwa na huruma:

وَكَذَٰلِكَ أَخْذُ رَبِّكَ إِذَا أَخَذَ الْقُرَىٰ وَهِيَ ظَالِمَةٌ ۚ إِنَّ أَخْذَهُ أَلِيمٌ شَدِيدٌ

“Vivyo hivyo mkamato wa Mola wako unavyokuwa anapokamata miji na huku ikifanya dhuluma – hakika mkamato Wake unaumiza vikali.”[5]

Aayah hizi ni dalili juu ya neema za Allaah juu yetu kwa kututumia Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwamba lengo la kumtuma Kwake ni ili atubainishie ´ibaadah. Kwa hiyo yule mwenye kumtii, ataingia Peponi, na yule mweye kuwasi ataingia Motoni kama ambavo watu wa Fir´awn waliingia Motoni kwa sababu ya kumwasi kwao Mtume wao Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Vivyo hivyo maadui wa Mitume ndio mwenendo na njia yao.

[1] 73:15-16

[2] 79:24

[3] 71:25

[4] 40:46

[5] 11:102

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 48-50
  • Imechapishwa: 02/12/2020