21. Dalili kwamba anayemtii Mtume, ataingia Peponi, na anayemuasi Motoni

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

إِنَّا أَرْسَلْنَا إِلَيْكُمْ رَسُولًا شَاهِدًا عَلَيْكُمْ كَمَا أَرْسَلْنَا إِلَىٰ فِرْعَوْنَ رَسُولًا فَعَصَىٰ فِرْعَوْنُ الرَّسُولَ فَأَخَذْنَاهُ أَخْذًا وَبِيلًا

“Hakika Sisi Tumekutumieni Mtume awe ni shahidi juu yenu, kama Tulivyotuma kwa Fir’awn Mtume. Lakini Fir’awn alimuasi huyo Mtume, Tukamuadhibu adhabu kali sana.”[1]

MAELEZO

Dalili ya kumtumiliza Mtume ni maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّا أَرْسَلْنَا إِلَيْكُمْ رَسُولًا شَاهِدًا عَلَيْكُمْ كَمَا أَرْسَلْنَا إِلَىٰ فِرْعَوْنَ رَسُولًا فَعَصَىٰ فِرْعَوْنُ الرَّسُولَ فَأَخَذْنَاهُ أَخْذًا وَبِيلًا

“Hakika Sisi Tumekutumieni Mtume awe ni shahidi juu yenu, kama Tulivyotuma kwa Fir’awn Mtume. Lakini Fir’awn alimuasi huyo Mtume, Tukamuadhibu adhabu kali sana.”

Sisi hapa dhamiri inarudi kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Hii ni dhamiri ya kujitukuza Mwenyewe kwa sababu Yeye ni mtukufu (Subhaanahu wa Ta´ala).

Tulimtuma – Pia hii ni dhamiri ya utukufu. Maana yake ni kwamba tumemtumiliza na kumfunulia Wahy.

Kwenu – Enyi majini na watu. Wanazungumzishwa watu wote. Kwa sababu ujumbe wa Mtume huyu ni wenye kumgusa kila mtu mpaka pale Qiyaamah kitaposimama.

Mtume – Ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Awe ni shahidi juu yenu – Bi maana mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´al) siku ya Qiyaamah. Kwani amekufikishieni ujumbe wa Allaah na amesimamisha hoja dhidi yenu. Amesema (Ta´ala):

رُّسُلًا مُّبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ لِئَلَّا يَكُونَ لِلنَّاسِ عَلَى اللَّـهِ حُجَّةٌ بَعْدَ الرُّسُلِ

“Mitume ni wabashiriaji na waonyaji ili pasikuweko kutoka kwa watu hoja yoyote juu ya Allaah baada ya kuletwa Mitume hao.”[2]

Hakuna yeyote siku ya Qiyaamah atasema kuwa hakujua kuwa ameumbwa kwa sababu ya ´ibaadah, hakujua ni yale yanayompasa na ni yepi yaliyo ya haramu kwake. Hawezi kuyasema haya. Kwa sababu Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) wamewafikishia. Ummah huu wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) utatoa ushahidi dhidi yao. Amesema (Ta´ala):

وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَاكُمْ أُمَّةً وَسَطًا لِّتَكُونُوا شُهَدَاءَ

“Namna hiyo Tumekufanyeni ummah bora na adilifu ili muwe mashahidi.”[3]

Ummah huu utatoa ushahidi dhidi ya nyumati zilizotangulia siku ya Qiyaamah kwamba Mitume walifikisha ujumbe wa Allaah kutokana na yale watayosoma ndani ya Qur-aan. Allaah ametusimulia visa vya nyumati zilizotangulia, Mitume na waliyowaambia nyumati zao. Yote haya tumeyajua kupitia Kitabu cha Allaah (´Azza wa Jall) ambacho hakiingiliwi na batili mbele yake wala nyuma yake – bali ni uteremsho kutoka kwa Mwingi wa hekima, Anayestahiki kuhimidiwa.

Na ili Mtume awe Mtume awe… Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) awe ni shahidi juu yenu enyi Ummah wa Muhammad. Atatoa ushahidi juu yenu kwamba alikusimamishieni hoja, akawafikishia ujumbe na akawanasihini kwa ajili ya Allaah. Kwa hivyo hakuna yeyote ambaye yuko na hoja siku ya Qiyaamah na akasema kuwa hakufikishiwa kitu na kwamba hakujiwa na mwonyaji. Mpaka makafiri watakubali kutupwa ndani ya Moto. Amesema (Ta´ala):

كُلَّمَا أُلْقِيَ فِيهَا فَوْجٌ سَأَلَهُمْ خَزَنَتُهَا أَلَمْ يَأْتِكُمْ نَذِيرٌ قَالُوا بَلَىٰ قَدْ جَاءَنَا نَذِيرٌ فَكَذَّبْنَا وَقُلْنَا مَا نَزَّلَ اللَّـهُ مِن شَيْءٍ إِنْ أَنتُمْ إِلَّا فِي ضَلَالٍ كَبِيرٍ

“Kila wanapotupwa ndani yake kundi, basi walinzi wake watawauliza: “Je, hajakufikieni mwonyaji yeyote?” Watasema: “Bali ndio! Hakika alitujia mwonyaji, hata hivyo tulikadhibisha na tukasema: “Allaah hakuteremsha kitu chochote; nyinyi si chochote isipokuwa mumo katika upotevu mkubwa.”[4]

Walikuwa wakiwaambia Mitume kwamba wako kwenye upotevu na hivyo wanawakadhibisha na kuwatia upotofuni Mitume. Hii ndio hoja ya kutumilizwa Mitume: wasimamishe hoja juu ya waja na kumwongoza yule ambaye Allaah amemtakia uongofu. Allaah anamwongoza amtakaye kupitia Mitume na anamsimamishia hoja yule anayefanya ukaidi, akakanusha na akakufuru.

[1] 73:15-16

[2] 04:165

[3] 02:143

[4] 67:08-09

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 48-50
  • Imechapishwa: 02/12/2020