5- Kufa akiwa ni mwenye kupambana katika njia ya Allaah. Kutokana na hilo kuna Hadiyth zifuatazo:

A- “Mnazingatia kufa shahidi ni kitu gani?” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Yule mwenye kuuliwa katika njia ya Allaah ndiye shahidi.” Akasema: “Basi mashahidi katika Ummah wangu ni wachache.” Wakasema: “Ni wepi, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Mwenye kuuliwa katika njia ya Allaah ni shahidi, mwenye kufa katika njia ya Allaah ni shahidi, mwenye kufa kwa maradhi ya tauni ni shahidi, mwenye kufa kwa maradhi ya tumbo[1] na mwenye kuzama ndani ya maji ni shahidi.”

Ameipokea Muslim (06/51) na Ahmad (02/522) kupitia kwa Abu Hurayrah.

Katika maudhui haya ipo Hadiyth kutoka kwa ´Umar iliyopokelewa na al-Haakim (02/109) na al-Bayhaqiy.

B- “Yule mwenye kutoka katika njia ya Allaah ambapo akafa, akauawa au akakanyagwa na farasi au ngamia wake au akagonjwa na mdundu mwenye sumu au akafa juu ya kitanda chake kwa balaa lolote alilolitaka Allaah, basi huyo ni shahidi na yuko na Pepo.”

Ameipokea Abu Daawuud (01/391), al-Haakim (02/78), al-Bayhaqiy (09/166) kupitia kwa Abu Maalik al-Ash´ariy. Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Haakim. Mambo yalivyo ni kwamba ni nzuri tu. Kisha nikabainikiwa na sababu ya kosa hili. Hakika si vinginevyo ni Hadiyth dhaifu. Anayetaka maelezo zaidi arejee katika “adh-Dhwa´iyfah” (5360).

[1] Bi maana ni yale maradhi ambayo yanamfanya mtu tumbo lake likavimba. Imesemekana vilevile kwamba ni maradhi ya tumbo la kuharisha. Imesemekana vilevile kwamba ni yule mwenye kuhisi maumivu tumboni.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 51
  • Imechapishwa: 30/01/2020