110 – Tambua – Allaah akurehemu – ya kwamba misingi ya Bid´ah ni milango minne. Katika milango hii mine yakatoka matawi sabini na mbili. Halafu baada ya hapo kila Bid´ah katika hizi ikatoa matawi mpaka zote zikafikia maoni elfu  mbili na mia nne. Zote ni upotevu na zote ni Motoni isipokuwa moja tu: ni yule mwenye kuamini yale yaliyomo ndani ya kitabu hichi na akayaamini pasi na kuwa na shaka na wasiwasi ndani ya moyo wake. Huyo ndiye mtu wa Sunnah na ndiye mwenye kuokoka – Allaah akitaka.

111 – Tambua – Allaah akurehemu – lau watu wangelijiepusha na mambo ya kuzua, wasiyavuke na kitu na wasizalishe maneno ambayo hakukupokelewa mapokezi kwayo kutoka kwa Mutme wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala Maswahabah zake, basi kusingelikuwepo Bid´ah yoyote.

112 – Tambua – Allaah akurehemu – ya kwamba hakuna kizuizi kati ya mja na hali yake kama muumini yenye kumfanya kuwa kafiri, isipokuwa ikiwa atakanusha kitu katika yale aliyoteremsha Allaah (Ta´ala), akazidisha au akapunguza katika maneno ya Allaah au akapinga kitu katika aliyosema Allaah (´Azza wa Jall) au kitu katika alichokisema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mche Allaah – Allaah akurehemu –  na kuwa makini na nafsi yako. Tahadhari na kuchupa mipaka katika dini, kwani hakika ni jambo halina lolote kuhusiana na njia ya haki.

113 – Yote niliyokueleza katika kitabu hichi yanatoka kwa Allaah (Ta´ala), kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Maswahabah zake, kutoka kwa wanafunzi wao na kutoka katika karne ya tatu na karne ya nne. Mche Allaah, ee mja wa Allaah! Ni juu yako kusadikisha, kujisalimisha, kutegemeza na kuridhia yaliyomo ndani ya kitabu hichi. Usimfiche muislamu yoyote kitabu hichi. Huenda Allaah akamrudisha aliyechanganyikiwa kutoka katika kuchanganyikiwa kwake, mtu wa Bid´ah kutoka katika Bid´ah zake au mpotevu kutoka katika upotevu wake na akaokoka nacho. Mche Allaah na shikamana na jambo la kwanza na la kale ambalo nimekueleza katika kitabu hichi. Allaah amrehemu mja na awarehemu wazazi wake aliyekisoma kitabu hichi, akakieneza, akakitendea kazi, akalingania kwacho na akakitumia kama hoja. Kwani hakika ni dini ya Allaah na ni dini ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mwenye kuhalalisha kitu chenye kwenda kinyume na yaliyomo ndani ya kitabu hichi, hakika atakuwa si mwenye kumuabudu Allaah kwa dini yoyote. Atakuwa ameyarudisha yote kama mfano wa mtu mwenye kuamini yote aliyosema Allaah (Tabaarak wa Ta´ala), lakini akaitilia shaka herufi moja. Kwa hiyo atakuwa ameyarudisha yote aliyosema Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) na hivyo ni kafiri. Kama ambavyo kushuhudia ya kwamba “hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah” haikubaliwi kwa mwenye kuitamka isipokuwa kwa kuwa na nia ya kweli na kuitakasa yakini, kadhalika Allaah hakubali kitu katika Sunnah ikiwa mtu ataacha baadhi yake. Yule mwenye kuacha kitu katika Sunnah basi atakuwa ameiacha Sunnah yote. Jilazimishe na kukubali na uache ubishi na wingi wa maneno kwa sababu mambo hayo hayana lolote kuhusiana na dini ya Allaah. Mche Allaah, kwani hakika uko katika wakati mbaya kabisa.

114 – Fitina ikitokea basi lazimiana kuwa ndani ya nyumba yako na kimbia palipo jirani na fitina. Tahadhari na ushabiki. Aina zote za vita vya kidunia kati ya waislamu ni fitina. Mche Allaah, hali ya kuwa yupekee pasi na mshirika, na usiviendee, usipigane katika vita hivyo, usiwe upande wa yeyote, usijiunge na yeyote na wala usipende chochote katika mambo hayo, kwa sababu imesemwa:

“Yule mwenye kupenda matendo ya watu – ni mamoja matendo hayo ni kheri au shari – ni kama mfano wa yule aliyefanya.”

Allaah atuwafikishe sisi na nyinyi katika yale anayoyaridhia na atuepushe na kumuasi.

  • Mhusika: Imaam Abu Muhammad al-Hasan bin Khalaf al-Barbahaariy (kfk. 329)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh-us-Sunnah, uk. 106-110
  • Imechapishwa: 23/12/2024