Swali 22: Kumetokea majadiliano na fitina kati yangu mimi na baadhi ya ndugu zangu waswaliji msikitini kuhusu kuswali Rak´ah mbili wakati wa kuingia msikitini na huku imamu anatoa Khutbah. Natumai kupata fatwa kutoka kwa muheshimiwa juu ya maudhui haya. Je, inafaa au haifai pamoja na kuzingatia kwamba ndugu hao wanaoswali katika msikiti huo wa kale ni wenye kufuata madhehebu ya Imaam Maalik[1]?

Jibu: Sunnah wakati wa kuingia msikiti ni mtu aswali Rak´ah mbili za mamkuzi ya msikiti ijapo imamu anatoa Khutbah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anapoingia mmoja wenu msikitini basi asiketi chini mpaka kwanza aswali Rak´ah mbili.”[2]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim katika “as-Swahiyh” zao.

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atapofika mmoja wenu siku ya ijumaa na imamu anatoa Khutbah, basi arukuu Rak´ah mbili na azifupishe.”[3]

Hili ni andiko la wazi juu ya maudhui haya. Haijuzu kwa yeyote kwenda kinyume nayo.

Pengine Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) hakufikiwa na Sunnah hii. Imethibiti kutoka kwake kwamba amekataza Rak´ah mbili wakati wa Khutbah. Ikisihi Sunnah kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi haifai kwa yeyote kwenda kinyume nayo kwa ajili ya maneno ya mtu yeyote awaye. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

“Enyi walioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi; mkizozana juu ya jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamuamini Allaah na siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri kabisa.”[4]

وَمَا اخْتَلَفْتُمْ فِيهِ مِن شَيْءٍ فَحُكْمُهُ إِلَى اللَّـهِ

”Jambo lolote lile mlilokhitilafiana kwalo, basi hukumu yake ni kwa Allaah.”[5]

Ni jambo linalotambulika kuwa hukumu ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni katika hukumu ya Allaah (´Azza wa Jall). Amesema (Subhaanah):

مَّن يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّـهَ

“Atakayemtii Mtume, basi kwa hakika amemtii Allaah.”[6]

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/388-389).

[2] al-Bukhaariy (425), Muslim (1166) na Ahmad na tamko ni lake.

[3] al-Bukhaariy (1170) na Muslim (875).

[4] 04:59

[5] 42:10

[6] 04:80

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 62-63
  • Imechapishwa: 28/11/2021