21. Kuswali Rak´ah mbili baada ya adhaana ya kwanza ya ijumaa

Swali 21: Naona katikati ya swalah ya ijumaa katika misikiti miwili Mitakatifu baadhi ya watu wanasimama kwa ajili ya kuswali Rak´ah mbili baada ya muadhini kumaliza kutoa adhaana ya kwanza. Nataraji kutoka kwa muheshimiwa kubainisha haki juu ya kitendo hichi. Allaah akujaze kheri na aurefushe umri wako katika kumtii[1].

Jibu: Sitambui katika dalili za Shari´ah yanayofahamisha juu ya kupendekeza kwa Rak´ah mbili hizi. Kwa sababu adhaana iliyotajwa ilianzishwa na ´Uthmaan bin ´Affaan (Radhiya Allaahu ´anh) wakati wa uongozi wake pindi watu walipokuwa wengi Madiynah. Alicholenga ni kuwazindua kwamba siku ya leo ni ya ijumaa na Maswahabah wakamfata katika jambo hilo. Miongoni mwao ni ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh). Jambo likatulia juu ya kwamba ni Sunnah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Lazimianeni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu. Ziumeni kwa magego yenu.”[2]

Baadhi ya wanazuoni wameona kuwa Rak´ah mbili hizi baada ya adhaana zimesuniwa kutokana na kuenea kwa maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kati ya kila adhaana mbili kuna swalah. Kati ya kila adhaana mbili kuna swalah.” Kisha mara ya tatu akasema: “Kwa anayetaka.”[3]

Inavyonidhihirikia ni kwamba adhaana iliyotajwa haingii katika hilo. Kwa sababu makusudio ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliposema “adhaana mbili” ni adhaana na Iqaamah tukiondosha siku ya ijumaa. Kuhusu siku ya ijumaa imewekwa katika Shari´ah kwa watu kujiandaa kusikiliza Khutbah baada ya adhaana.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/390-391).

[2] Abu Daawuud (4607).

[3] al-Bukhaariy (588, 591) na tamko ni lake na Muslim (1384).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 61-62
  • Imechapishwa: 28/11/2021