20. Watoto waliowatangulia wakubwa katika safu wana haki zaidi

Swali 20: Baadhi ya watoto wanakuja mapema siku ya ijumaa. Baadaye wanakuja watu ambao ni wakubwa zaidi kuliko wao ambapo wanawasimamisha na wanaketi maeneo yao. Wanajengea hoja kwa maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Wawe nyuma yangu kati yenu wakomavu na wenye akili.”

Je, kufanya hivi kunafaa[1]?

Jibu: Haya yanasemwa na baadhi ya wanazuoni ambao wanaona bora kwa watoto wapange safu nyuma ya wanamme. Maoni haya yanatakiwa kutazamwa vizuri. Maoni sahihi zaidi ni kwamba wakitangulia mbele basi haifai kuwarudisha nyuma. Wakitangulia katika safu ya kwanza au katika safu ya pili basi asiwasimamishe ambaye amekuja baada yao. Kwa sababu wametangulia katika haki ambayo haikutanguliwa na wengine. Kwa hivyo haijuzu kuwarudisha nyuma kutokana na kuenea kwa Hadiyth juu ya hilo. Kuwarudisha nyuma ni kuwakimbiza mbali na swalah na kuikimbilia. Kwa hivyo si sawa kufanya hivo.

Lakini endapo watu watakusanyika kama kwa mfano wamefika kutoka safarini au wamekusanyika kutokana na sababu nyingine, basi wanamme watapanga safu mwanzo kisha wafuatiwe na watoto halafu waje wanawake ikitokea hali hiyo hali ya kuwa wamekusanyika. Kuhusu kuwaondosha kutoka katika safu na wakaketi mahali pao wakubwa ambao wamekuja baada yao haijuzu kufanya hivo kutokana na tulivyotaja. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Wawe nyuma yangu kati yenu wakomavu na wenye akili.”

Makusudio yake ni kuwahimiza wakomavu kuharakia swalah na wawe mbele za watu. Hiyo haina maana kwamba ya kuwarudisha nyuma ambao wamewatangulia eti kwa sababu yao wao. Kwa sababu hayo yanakwenda kinyume na dalili za Shari´ah tulizotaja.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/408-409).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 59-60
  • Imechapishwa: 28/11/2021