22. Namna ya kufikia subira wakati wa mitihani

Nasema:

Anapata radhi mja anayezipokea neema kwa shukurani

na ana subira katika kipindi kizito – hiyo ndio nusura yake

Ambaye ameridhiwa na Mwingi wa huruma basi huyo ndiye mwenye furaha,

kwa fadhilah za Allaah duniani na Aakhirah

Subira juu ya misiba inahakikishwa kwa njia nyingi. Njia moja wapo ni yule aliyepatwa na msiba kutaraji yale malipo ambayo Allaah amemuahidi juu ya msiba huo.

Njia nyingine ni yeye kutambua kuwa katika kila msiba kuna ambao ni mbaya zaidi. Kwa hivyo yule aliyepatwa na msiba anajiliwaza kwa kuifikiria ile misiba ambayo ni mibaya zaidi kushinda wa kwake. Waumini wanaiona misiba isiyohusiana na dini kuwa ni miepesi na rahisi zaidi. Bwana mmoja alisema kumwambia Sahl bin Sa´d at-Tastariy (Rahimahu Allaah):

“Mwizi aliingia nyumbani kwangu na akaniibia mali yangu.” Sahl akasema: “Mshukuru Allaah (Ta´ala). Ungelifanya nini iwapo shaytwaan angeliingia moyoni mwako na kuiharibu imani yako?”

Imepokelewa jinsi ambavyo mwanamke mmoja wa kiarabu aliwapitia watoto wake wawili wa kiarabu waliouliwa, akamuhimidi Allaah, Mola wa walimwengu, kisha akasema:

Mitihani yote inayompata mtu ni salama

muda wa kuwa hajafanya jambo litalomkutanisha na Allaah Motoni

Njia ya tatu ni mtu atambue kuwa mitihani ni kifutio cha madhambi, muda wa kuwa ni miepesi na yenye kupita. Aidha inazuia adhabu za Aakhirah, licha ya kwamba ni za khatari na zenye kubaki.

Njia ya nne ni yeye atambue kuwa yote hayo yalikuwa tayari yamekwishakadiriwa na hayakwepeki. Mwenye kupewa mtihani, amekwishapata yale aliyokadiriwa na kuepuka shari yake. Miongoni mwa mambo bora yaliyopokelewa juu ya maudhui hayo ni maneno yake ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh):

“Sijapewa mtihani isipokuwa Allaah (´Azza wa Jall) amenitunuku neema nne juu ya jaribio hilo: haukuipata dini yangu, haukuwa mbaya zaidi, haukunikosesha ridhaa yangu na nataraji malipo juu yake.”

Sahl bin Sa´d at-Tastariy (Rahimahu Allaah) amesema:

Nafsi ya mtambuzi imejaa imani na imetulia

imeridhika na kile kilichopangwa na kutarajiwa

inaangaza kwa nuru ya uongofu na yakini

ambapo ikaangaza na baadaye ikatulizana

Nataraji mazuri katika kila maisha yote

ilihali inatamani ukaribu wa Mfalme.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin ´Abdillaah bin Naaswir-id-Diyn ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bard-ul-Akbaad ´inda Faqd-il-Awlaad, uk. 101-102
  • Imechapishwa: 21/08/2023