21. Mgonjwa wa misuli na kipofu anamshukuru Allaah

Abu Bakr Muhammad bin al-Hasan bin Durayd amesema: ´Abdur-Rahmaan ametukhabarisha, kutoka kwa ami yake, kutoka kwa Yuunus,  ambaye ameeleza:

“Wakati ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) alipokuwa nje akitembelea, alikuja bedui mmoja. Akamwambia: “Ee bedui! Umetokea wapi?” Akasema: “Kutokea kwenye amana ya mlima huu.” Akasema: “Amana yake ni nini?” Akasema: “Mwanangu niliyemzika tangu miaka miwili iliyopita. Mimi namtembelea kila siku na kumuombolezea.” ´Umar akasema: “Nakuomba kwa Allaah unisikilizishe kitu katika hayo.” Akasema:

Ee uliyetoweka ambaye hurudi katika safari yako

Kifo kilimchukua haraka katika udogo wake

Ee kiburudisho cha jicho langu, ulikuwa furaha yangu

usiku kucha na hata saa za usiku

Jicho halioni kitu kinachoishi

isipokuwa kinanikumbusha juu yake

Umekunywa kwenye kikombe ambcho baba yako atakinywa

siku moja, kabla au baadaye, katika utuuzima wake

linawahusu pia viumbe wote

ni mamoja aliyeko mashambani au mijini

Himdi zote ni stahiki ya Allaah, asiyekuwa na mshirika

haya daima aliyajua na kuyakadiria

Kifo kimegawanywa kati ya waja

na hakuna kiumbe yeyote awezaye kuzidisha katika umri wake

´Umar akalia mpaka zikalowa ndevu zake kisha akasema: “Umesema kweli, ee bedui.”

Abul-´Abbaas Ahmad bin Masruuq amesema: Muhammad bin al-Husayn ametuhadithia: Muusa bin ´Iysaa amenihadithia, kutoka kwa al-Waliyd bin Muslim, kutoka kwa Abu ´Umar al-Awzaa´iy:

“Nilitoka kwa lengo la kulinda mipaka ya nchi mpaka nilipokuwa ´Ariysh Misri, ambapo nikamuona kipofu chini ya mwavuli. Mikono na miguu yake ilikuwa imening´inia bila uhai. Akisema: “Himdi zote njema ni Zako, ee Mola na mlinzi Wangu. Ee Allaah! Hakika mimi nakuhimidi himdi nyingi ambazo zinawaenea viumbe Wako wote, kama fadhilah Yako juu ya viumbe Wako wengine wote. Kwani hakika umenifadhilisha juu ya wengine wengi Uliyowaumba.” Nikafikiria kumuuliza kama anajua jambo hilo au anazumgumza namna hiyo tu kwa ajili ya msukumo fulani. Nikamsogelea na kumtolea salamu. Akaniitikia salamu yangu. Nikamwambia: “Allaah akurehemu! Nataka kukuuliza jambo. Utanieleza?” Akasema: “Ikiwa nalijua, basi nitakujibu.” Nikasema: “Allaah akurehemu! Unamuhimidi Yeye juu ya neema gani? Huoni nini Amekufanyia?” Akajibu, ndio. Akasema: “Naapa kwa Allaah! Iwapo Allaah atanimiminia moto ukanichoma, akaiamrisha milima inisagesage, akaziamrisha bahari zinizamishe na akaziamrisha ardhi zikanifunika, basi hakuna ambacho kingezidi kwake isipokuwa tu kumpenda na kumshukuru. Naweza kukuomba mahitaji fulani unitekelezee?” Nikasema: “Ndio, niombe unachotaka.” Akasema: “Mwanangu alikuwa daima akinikumbusha nyakati za swalah na akinilisha wakati wa kufungua kwangu swawm. Nimemkosa tangu jana.  Unaweza kunitafutia naye?” Nikafikiria kujikurubisha kwa Allaah (´Azza wa Jall) kwa kitendo hichi, nikatoka na kuanza kumtafuta. Nilipofika katika baadhi ya matuta ya mchanga, nikamuona mnyamamkali akimla yule mvulana. Nikasema:  “Hakika sisi ni wa Allaah na Kwake ndiko tutarejea”. Nini nitamweleza mja huyu mwema juu ya mtoto wake? Mwishowe nikarudi kwake nikamtolea salamu. Akanirudishia salamu. Nikasema: “Allaah akurehemu! Nataka kukuuliza kitu. Utanieleza?” Akasema: “Ikiwa nalijua, basi nitakujibu.” Nikasema: “Wewe ni mtukufu na umekurubishwa zaidi mbele ya Allaah (´Azza wa Jall) kumshinda Nabii wa Allaah Ayyuub (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?” Akasema: “Nabii wa Allaah Ayyuub (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye mtukufu na mwenye ngazi ya juu zaidi mbele ya Allaah kuliko mimi.” Nikasema: “Allaah alimpa mtihani na akasubiri. Hali iliendelea kuwa nzito mpaka watu wake wa karibu wakamtelekeza. Akawa ni kicheko kwa wapita njia. Tambua kuwa mwanao, ambaye ulinieleza na ukaniomba nikutafutie, ameliwa na myamamkali. Allaah akufanyie makubwa malipo yako juu yake.” Akasema: “Himdi zote njema ni za Allaah ambaye hakunifanya kuhisi huzuniko lolote la kidunia. Kisha akashusha pumzi na akaanguka kifudifudi. Nikakaa kitambo fulani halafu nikamtikisa. Akawa amekufa. Nikasema: “Hakika sisi ni wa Allaah na Kwake ndiko tutarejea”. Nifanye nini juu yake? Ni nani ambaye atanisaidia kumuosha na kumvika sanda, kuchimba kaburi lake na kumzika? Nilipokuwa katika hali hiyo nikaona msafara unaoelekea katika mipaka ya nchi. Nikawapungia mkono ambapo wakabadili njia kuelekea kwangu. Wakaegesha juu yangu na wakasema: “ Wewe ni nani na ni nini hiki?” Nikawaeleza yaliyotokea. Wakashuka chini, wakawafunga vipando vya wanyama wao na kunisaidia kumuosha bwana yule kwa maji ya bahari. Tukamvisha sanda kwa nguo waliokuwa nayo. Kisha nikatangulia mbele na tukamswalia swalah ya jeneza. Hatimaye tukamzika chini ya mwavuli wake. Nikakaa karibu na kaburi lake hali ya kuliwazika naye. Nikisoma Qur-aan kwa muda wakati wa usiku ambapo nikachukuliwa na usingizi. Nikamuona rafiki yangu akiwa katika maumbile mazuri kabisa na mavazi mazuri kabisa. Alikuwa katika bustani ya kijani, amevaa mavazi ya kijani, ambapo amesimama na akisoma Qur-aan. Nikawambia: “Wewe sio rafiki yangu?” Akasema: “Ndio.” Nikasema: “Ni kipi kilichokufanya uwe hicho ninachokiona?” Akasema: “Mimi nimejiunga pamoja na wale wenye kusubiri kwa ajili ya Allaah (´Azza wa Jall) na nimepata ngazi ambayo haipatikani isipokuwa kwa kuwa na subira wakati wa majanga na kushukuru katika kipindi cha raha.” Baada ya hapo nikaamka.”

Neema hizi mbili ni kubwa mno: kuwa na subira wakati wa mitihani na kushukuru katika kipindi cha raha. Anayetunukiwa mawili hayo basi hakika ametunukiwa kheri kubwa. Yule anayeyatendea kazi basi hakika amefuzu thawabu kubwa na anapata radhi za Mola mwingi wa rehema.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin ´Abdillaah bin Naaswir-id-Diyn ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bard-ul-Akbaad ´inda Faqd-il-Awlaad, uk. 97-101
  • Imechapishwa: 21/08/2023