23. Maisha ya dunia ni kilimo kwa ajili ya Aakhirah

Liwazo lingine, ambalo ni moja wapo ya dawa juu ya huzuni kwa aliyempoteza ndugu yake mpendwa, ni yeye kutambua kuwa dunia ni yenye kuisha na ya kupita. Furaha na maovu yake ni yenye kuondoka. Imeumbwa kwa ajili ya kuondoka na kuharibika. Kila kilichomo ndani yake kinabadilika na kugeuka na baadaye kumalizika, kuondoka na kuteketea. Si vyengine ni shamba kwa ajili ya Aakhirah. Imepokelewa kwamba Abud-Dardaa´ (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Sulaymaan (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa na mtoto wa kiume ambaye amefungamana naye sana. Mtoto yule akafa na akahuzunika huzuni kubwa, jambo ambalo lilionekana katika mahakama na matangamano yake. Ndipo Allaah (Ta´ala) akamtumia Malaika wawili wakiwa katika umbile la mtu. Akasema: “Nyinyi ni kina nani?” Wakasema: “Tumegombana.” Akawaambia waketi katika kikao cha hukumu. Akasema mmoja wao: “Mimi nimepanda mbegu ambapo akaja huyu na kuiharibu.” Sulaymaan (´alayhis-Salaam) akasema: “Anasema nini?” Yule mwingine akasema: “Allaah akutengeneze! Ulipanda katika njia. Wakati nilipotaka kupita, nikitazama upande wa kulia naona kilimo, upande wa kushoto na upande wa mbele yangu. Ndipo nikaamua kupita katikati ya njia. Ndipo ikaharibika mimea yake.” Sulaymaan (´alayhis-Salaam) akasema: “Ni kipi kilichokupelekea kupanda katika njia ya watu?” Ndipo mmoja katika Malaika wale akasema: “Hivi hukujua, ee Sulaymaan, ya kwamba kifo ni njia ya watu? Ni lazima kwa watu wapite njia hiyo.” Ni kama kwamba wakati huo ndio Sulaymaan (´alayhis-Salaam) alifunuliwa kifuniko.”

Hii ni rambirambi nzuri kwa yule ambaye amefikwa na msiba.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin ´Abdillaah bin Naaswir-id-Diyn ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bard-ul-Akbaad ´inda Faqd-il-Awlaad, uk. 102-104
  • Imechapishwa: 21/08/2023