22. Mfano wa vichenguzi vya Uislamu II

Mifano mingine ni amkadhibishe Allaah au amkadhibishe Mtume Wake, amchukie Allaah au amchukie Mtume Wake, achukie kitu miongoni mwa vile alivyokuja navyo Allaah au Mtume Wake, akachukia kushinda kwa dini ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au Uislamu kuwa na nguvu, akafurahishwa na kuporomoka kwa dini ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kudhoofika kwa Uislamu na waislamu, akaona kuwa si lazima kumfuata Mtume, akaona kuwa si lazima kuhukumu kwa Qur-aan na Sunnah za Mtume Wake, akafanya kiburi kumwabudu Allaah nako ni kule kuipokea amri ya Allaah au amri ya Mtume Wake kwa kukataa na kufanya kiburi. Amesema (Ta´ala):

وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ أَبَىٰ وَاسْتَكْبَرَ وَكَانَ مِنَ الْكَافِرِينَ

”Kumbuka Tulipowaambia Malaika: ”Msujudieni Aadam”, wakasujudu isipokuwa Ibliys alikataa na akatakabari na akawa miongoni mwa makafiri.”[1]

وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ ۚإِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ

“Mola wenu amesema: “Niombeni Nitakuitikieni. Hakika wale wanaotakabari na ‘ibaadah Yangu, wataingika Motoni wadhalilike.””[2]

Au akaipuuza dini ya Allaah ambapo hajifunza nayo na wala haifanyii kazi. Amesema (Ta´ala):

وَالَّذِينَ كَفَرُوا عَمَّا أُنذِرُوا مُعْرِضُونَ

“Na wale waliokufuru kwa yale wanayoonywa kwayo ni wenye kukengeuka.”[3]

Au akatilia shaka ukweli wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika yale aliyoeleza, akatilia shaka maelezo ya Allaah, akatilia shaka Qiyaamah, kufufuliwa, Pepo au Moto. Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu watu wa mabustani mawili:

وَمَا أَظُنُّ السَّاعَةَ قَائِمَةً وَلَئِن رُّدِدتُّ إِلَىٰ رَبِّي لَأَجِدَنَّ خَيْرًا مِّنْهَا مُنقَلَبًا قَالَ لَهُ صَاحِبُهُ وَهُوَ يُحَاوِرُهُ أَكَفَرْتَ بِالَّذِي خَلَقَكَ مِن تُرَابٍ ثُمَّ مِن نُّطْفَةٍ ثُمَّ سَوَّاكَ رَجُلًا  لَّـٰكِنَّا هُوَ اللَّـهُ رَبِّي وَلَا أُشْرِكُ بِرَبِّي أَحَدًا

“Sidhani kama haya yatatoweka kamwe na wala sidhani kama Qiyaamah kitasimama na hata kama nitarudishwa kwa Mola wangu, bila shaka nitakuta marejeo bora kuliko haya. Rafiki yake akamwambia na huku anajadiliana naye: “Je, umemkufuru Yule aliyekuumba kutokana na mchanga, kisha kutokana na manii, kisha akakusawazisha kuwa mtu? Lakini Yeye Allaah ndiye Mola wangu na wala sitomshirikisha Mola wangu na yeyote.”[4]

Au akadhihirisha Uislamu kwa mdomo wake na akaficha ukafiri moyoni mwake. Mtu aina hii anakuwa mnafiki. Amesema (Ta´ala):

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ آمَنُوا ثُمَّ كَفَرُوا فَطُبِعَ عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ فَهُمْ لَا يَفْقَهُونَ

“Hayo ni kwa kuwa wao waliamini, kisha wakakufuru, basi ikapigwa chapa juu ya nyoyo zao kwa hiyo hawafahamu.”[5]

Au akaingia katika Uislamu kwa kujionyesha kwa ajili ya dunia, kuchelea kuuliwa, kama ilivyo hali wanafiki.

[1] 02:34

[2] 40:60

[3] 46:03

[4] 18:36-38

[5] 63:03

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Iymaan – Haqiyqatuhu wa Nawaaqidhwuh, uk. 28-29
  • Imechapishwa: 02/05/2023