22. Kutochukua msimamo wowote juu ya Qur-aan – shaytwaan bubu

Imaam Ibn Abiy Daawuud (Rahimahu Allaah) amesema:

ولا تكُ في القرآن بالوقف قائلاً

04 – Usichukue msimamo wa kusita juu ya Qur-aan

كما قال أتْباعٌ لجهمٍ وأسجحُوا

     kama walivyosema wafuasi wa Jahmiy na wakazembea

MAELEZO

Miongoni mwa Jahmiyyah kuna ambao wanasema waziwazi kwamba Qur-aan imeumbwa. Hawa ni wale viongozi wa Jahmiyyah.

Miongoni wao kuna wengine wanasema kuwa hawasemi kuwa imeumbwa wala haikuumbwa. Wanasema kuwa wanachukua msimamo wa kusimama. Huyu ni shaytwaan bubu. Akisimama watu watafikiria kuwa Qur-aan ni kiumbe. Ni lazima kubainisha. Wakisema kuwa imeumbwa basi usinyamaze. Maana yake ni kwamba unawasapoti lakini hata hivyo huweki wazi. Kwa hivyo haijuzu kusimama katika jambo hili. Hii ni ´Aqiydah ya wasimamaji ambao hawasemi kuwa Qur-aan imeumbwa wala haikuumbwa. Hili maana yake ni kuficha kubainisha haki na ni jambo linatoa ishara kwamba maoni ya Jahmiyyah ni sahihi kwa sababu mtu huyu hakuwaraddi, hakuwafedhehesha na kuwafichua.

Ambaye anatia shaka kama Qur-aan ni kiumbe au sio kiumbe na badala yake akaamua kusimama, huyu ni Jahmiy. Vinginevyo kama asingelikuwa mtu Jahmiy angesema kwa kinywa kipana. Lakini anajificha kwa kunyamaza.

Uhakika wa mambo ni kuwa huyu ni mbaya zaidi kuliko Jahmiyyah. Kwa sababu wao wameweka wazi na ´Aqiydah yao ikajulikana. Kuhusu mtu huyu anataka kuwapaka watu mchanga wa machoni na kuonesha kuwa ni mnyenyekevu na mchaji zaidi na kwamba eti hawezi kuzungumzia mambo haya. Haifai kusimama. Ni lazima kusema kwa kinywa kipana na kubatilisha ´Aqiydah hii.

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kama walivyosema na wakazembea.”

Amewafanya kuwa na wao ni katika wafuasi wa Jahmiyyah. Kwa sababu lau wasingelikuwa ni katika wafuasi wa Jahmiyyah wasingesimama. Kinyume chake wangeliwaraddi na wakasema waziwazi jambo hilo.

Jahmiyyah walipoona kuwa watu hawakubaliani na ´Aqiydah yao ndio wakakimbia katika hila hii. Lengo ilikuwa wafiche batili yao nyuma yake. Kwa ajili hii pindi Imaam Ahmad alipoulizwa juu ya msimamo wa kusimama akasema yafuatayo:

“Lau hili lingelikuwa kabla ya Jahmiyyah kusema waliyoyasema tungekuwa tunasimama. Lakini baada ya wao kusema maneno yao ya aibu, ni lazima kusema wazi kwa kinywa kipana juu ya ubatilifu wake na kuyaraddi.”

Haya ni maana ya aliyoyasema Imaam Ahmad kuhusu masuala ya kusimama kwamba Qur-aan imeumbwa.

Maneno yake mtunzi (Rahimahu Allaah):

“… na wakazembea.”

Bi maana kufanya wepesi na kulainisha. Wakazembea.

Katika baadhi ya vitabu imekuja:

“… na wakasamehe.”

Bi maana wakasamehe hili. Ni mamoja walizembea au walisamehe maana yake ni kwamba hawakukemea. Badala yake ni kwamba walilainisha pamoja na Jahmiyyah na hawakuwakemea. Walichukua msimamo wa kusimama katika suala hili.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 73-74
  • Imechapishwa: 31/12/2023