21. Tofauti ya ufalme wa Allaah na wa viumbe

Amesema mtunzi (Rahimahu Allaah):

Sema “Hayakuumbwa… “

Hapa wanaraddiwa Jahmiyyah na wenye kuonelea ´Aqiydah yao.

Amesema mtunzi (Rahimahu Allaah):

“… maneno ya Mfalme Wetu.”

Mfalme ni Allaah (Jalla wa ´Alaa). Yeye ndiye Mfalme. Amesema (Ta´ala):

تَبَارَكَ الَّذِي بِيَدِهِ الْمُلْكُ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

“Amebarikika ambaye mkononi Mwake umo ufalme Naye juu ya kila kitu ni muweza.” (67:01)

قُلِ اللَّـهُمَّ مَالِكَ الْمُلْكِ تُؤْتِي الْمُلْكَ مَن تَشَاءُ وَتَنزِعُ الْمُلْكَ مِمَّن تَشَاءُ وَتُعِزُّ مَن تَشَاءُ وَتُذِلُّ مَن تَشَاءُ ۖ بِيَدِكَ الْخَيْرُ ۖ إِنَّكَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

“Sema: “Ee Allaah Mfalme uliyemiliki ufalme wote! Unampa ufalme umtakaye na unamuondoshea ufalme umtakaye na unamtukuza umtakaye na unamdhalilisha umtakaye – kheri yote imo mkononi mwako.  Hakika Wewe juu ya kila kitu ni muweza.”” (03:26)

Allaah (Jalla wa ´Alaa) Yeye ndiye Mfalme wa wafalme. Kuhusu ufalme wa wanaadamu ufalme wao ni wa muda. Allaah anampa ufalme yule anayemtaka kwa muda kisha baadaye anamnyakua nao na kumpa mwingine tena.

Kuhusu ufalme wenye kuthibiti na wa daima usioondoka ni ufalme wa Allaah (Jalla wa ´Alaa). Pindi kitaposimama Qiyaamah Allaah (Jalla wa ´Alaa) atauliza:

لِّمَنِ الْمُلْكُ الْيَوْمَ

“Ufalme ni wa nani hii leo?”

Hakuna yeyote atayejibu wala kuzungumza. Angelikuweko yeyote aliye na madai angesema kuwa ni yeye. Baada ya hapo Ajijibu Mwenyewe kwa kusema:

لِلَّـهِ الْوَاحِدِ الْقَهَّارِ

“Ni wa Allaah pekee Mmoja, Aliye juu.” (40:16)

Hakuna hata mmoja anayepingana na hili. Ufalme wote ni wa Allaah (Jalla wa ´Alaa). Anampa ufalme yule Amtakaye kwa muda maalum kisha baada ya hapo ima anakufa au anapokonywa kwa mabavu.

Maneno ya mtunzi (Rahimahu Allaah):

“ivyo ndivyo… “

Bi maana ya kwamba Qur-aan sio kiumbe.

Maneno yake mtunzi (Rahimahu Allaah):

“… walivyoamini wachaji Allaah… “

Bi maana ndivyo maimamu wachaji Allaah walivyoitakidi msemo huu.

Maneno yake mtunzi (Rahimahu Allaah):

“… na wakalidhihirisha.”

Wakawadhihirishia watu na wakasema kuwa Qur-aan imeteremshwa na haikuumbwa. Hawakusema kuwa hii ni mitazamo ya wengine na watu waachwe kwa sababu wana uhuru wa kuzungumza na uhuru wa kuwa na maoni mbalimbali. Kinyume chake waliyaweka mambo wazi kwa hali ya juu na wakabishana na kujadili. Vilevile wakatunga na kuandika vitabu kwa ajili ya kuraddi ´Aqiydah hii. Hilo ni kutokana na khatari na aibu yake. ´Aqiydah hii ndani yake kuna kumtia Allaah (´Azza wa Jall) mapungufu. Wanazuoni hawawezi kunyamazia ´Aqiydah hii au wakaichukulia sahali.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 71-72
  • Imechapishwa: 31/12/2023