21. Washirikina wa kale walikuwa wakishirikisha katika raha tu tofauti na washirikina wa leo

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Akisema: “Kwa hakika hawakukufuru kwa kuwaomba Malaika na Mitume, bali walikufuru waliposema: “Malaika ni mabanati wa Allaah”, sisi hatusemi kuwa ´Abdul-Qaadir ni mtoto wa Allaah wala mwengine yeyote” jibu ni: “Kumnasibishia mtoto Allaah ni kufuru ya kivyake. Allaah (Ta´ala) amesema:

قُلْ هُوَ اللَّـهُ أَحَدٌ اللَّـهُ الصَّمَدُ

“Sema: “Yeye ni Allaah Mmoja pekee, Allaah ambaye ni Mwenye kukusudiwa kwa haja zote.”” (al-Ikhlaasw 112 : 1-2)

Na kwamba Yeye ni Mmoja pekee asiyekuwa na anayelingana Naye, na “asw-Swamad” ni mkusudiwa kwa haja. Atakayepinga haya, atakuwa amekufuru, hata kama hakupinga Suurah.” Allaah (Ta´ala) amesema:

مَا اتَّخَذَ اللَّـهُ مِن وَلَدٍ وَمَا كَانَ مَعَهُ مِنْ إِلَـٰهٍ ۚ إِذًا لَّذَهَبَ كُلُّ إِلَـٰهٍ بِمَا خَلَقَ وَلَعَلَا بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ

“Allaah hakujichukulia mwana yeyote na wala hakukuwa pamoja Naye mwabudiwa yeyote.” (al-Muuminuun 23 : 91)

Katofautisha baina ya sampuli mbili na amefanya yote mawili ni kufuru ya kivyake.

Amesema (Ta´ala):

وَجَعَلُوا لِلَّـهِ شُرَكَاءَ الْجِنَّ وَخَلَقَهُمْ ۖ وَخَرَقُوا لَهُ بَنِينَ وَبَنَاتٍ بِغَيْرِ عِلْمٍ

”Na wamemfanyia Allaah majini kuwa ni washirika Wake – na hali Yeye ndiye Kawaumba – na wakamsingizia kuwa na mabanati na wavulana pasi na ujuzi.” (al-An´aam 06 : 100)

Katofautisha baina ya kufuru hizo mbili. Dalili ya hilo pia ni kwamba waliokufuru kwa kumuomba Laat – pamoja na kuwa ni mtu mwema – hawakumfanya ni mtoto wa Allaah, na wale waliokufuru kwa kuabudu jini, pia hawakumfanya hivo. Hali hadhalika wanachuoni wa madhehebu yote manne wanasema katika: “Mlango: Hukumu ya mwenye kuritadi”, ya kwamba Muislamu akidai ya kwamba Allaah ana mtoto ni murtadi na wanatofautisha baina ya aina hizo mbili – na hili ni jambo liko wazi. Akisema:

أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ

”Tanabahi! Hakika mawalii wa Allaah hakuna khofu juu yao na wala hawatohuzunika.” (Yuunus 10 : 62)

Mwambie: “Hii ni haki, lakini hawaabudiwi. Na sisi hakuna tulichopinga isipokuwa tu kule kuwaabudu kwao pamoja na Allaah na kumshirikisha pamoja Naye. Vinginevyo ni wajibu kwako kuwapenda, kuwafuata na kukubali karama zao. Na wala hawapingi karama za mawalii isipokuwa Ahl-ul-Bid´ah wad-Dhwalaal. Dini ya Allaah iko kati ya mambo mawili, uongofu baina ya upotofu mbili na haki baina ya batili mbili.

Ukishajua kile wanachoita washirikina katika zama zetu hizi “Itikadi” ndio shirki iliyoteremka katika Qur-aan juu yake na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawapiga vita watu kwa ajili yayo, basi ujue kuwa shirki ya watu wa mwanzo ni khafifu kuliko shirki ya watu wa zama zetu kwa mambo mawili.

La kwanza: Watu wa mwanzo walikuwa hawashirikishi na wala hawawaombi Malaika, mawalii na masanamu pamoja na Allaah isipokuwa wakati wa raha. Ama wakati wa shida, walikuwa ni wenye kumtakasia Allaah dini. Kama alivyosema (Ta´ala):

وَإِذَا مَسَّكُمُ الضُّرُّ فِي الْبَحْرِ ضَلَّ مَن تَدْعُونَ إِلَّا إِيَّاهُ ۖ فَلَمَّا نَجَّاكُمْ إِلَى الْبَرِّ أَعْرَضْتُمْ ۚ وَكَانَ الْإِنسَانُ كَفُورًا

“Inapokuguseni dhara baharini hupotea wale mnaowaomba isipokuwa Yeye pekee. Pindi anapokuokoeni katika nchi kavu, mnakengeuka; mtu amekuwa ni mwingi wa kukufuru.” (al-Israa´ 17 : 67)

Na Kauli Yake (Ta´ala):

قُلْ أَرَأَيْتَكُمْ إِنْ أَتَاكُمْ عَذَابُ اللَّـهِ أَوْ أَتَتْكُمُ السَّاعَةُ أَغَيْرَ اللَّـهِ تَدْعُونَ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ بَلْ إِيَّاهُ تَدْعُونَ فَيَكْشِفُ مَا تَدْعُونَ إِلَيْهِ إِن شَاءَ وَتَنسَوْنَ مَا تُشْرِكُونَ

”Sema: “Je mnaonaje ikikufikieni adhabu ya Allaah au ikakufikieni Saa; je, mtamwomba asiyekuwa Allaah mkiwa ni wakweli?” Bali Yeye pekee ndiye mtakayemwomba, kisha atakuondoleeni yale mliyomwomba Akitaka, na mtasahau yale mnayoyashirikisha pamoja Naye.”” (al-An´aam 06 : 40-41)

Na Kauli Yake (Ta´ala):

وَإِذَا مَسَّ الْإِنسَانَ ضُرٌّ دَعَا رَبَّهُ مُنِيبًا إِلَيْهِ ثُمَّ إِذَا خَوَّلَهُ نِعْمَةً مِّنْهُ نَسِيَ مَا كَانَ يَدْعُو إِلَيْهِ مِن قَبْلُ وَجَعَلَ لِلَّـهِ أَندَادًا لِّيُضِلَّ عَن سَبِيلِهِ ۚ قُلْ تَمَتَّعْ بِكُفْرِكَ قَلِيلًا ۖ إِنَّكَ مِنْ أَصْحَابِ النَّارِ

”Na inapomgusa binaadamu dhara, humwomba Mola wake akirudiarudia Kwake hali ya kutubia, kisha Akimtunukia neema kutoka Kwake husahau yale aliyokuwa akimwomba kabla na kumfanyia Allaah washirika ili apotee na Njia Yake. Sema: “Starehe kwa kufuru yako kidogo tu. Hakika wewe ni miongoni mwa watu wa motoni!”” (az-Zumar 39 : 08)

Na Kauli Yake (Ta´ala):

وَإِذَا غَشِيَهُم مَّوْجٌ كَالظُّلَلِ دَعَوُا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ

”Yanapowafunika mawimbi kama vivuli humwomba Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini.” (Luqmaan 31 : 32)

Atakayefahamu masuala haya ambayo Allaah ameyaweka wazi katika Kitabu Chake – nayo ni kwamba washirikina ambao Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwapiga vita walikuwa wakimuomba Allaah (Ta´ala) na wakiwaomba wengine katika raha, ama wakati mgumu na wa shida hawamuombi mwengine isipokuwa Allaah pekee hali ya kuwa hana mshirika na wanawasahau mabwana wao – umembainishia tofauti baina ya watu wa zama zetu na shirki ya watu wa mwanzo. Lakini ni nani ambaye moyo wake unayafahamu mambo haya ufahamu wa ndani kabisa? Allaah ndiye Mwenye kutakwa msaada.

Jambo la pili: Watu wa mwanzo walikuwa wakiomba pamoja na Allaah watu waliokuwa karibu na Allaah. Ima Mitume, mawalii au Malaika. Na wanaomba pia miti au mawe vinavyomtii Allaah na havimuasi. Lakini watu wa zama zetu wanaomba pamoja na Allaah katika mafusaki ya watu. Na wale wanaowaomba ndio wanaowahalalishia maovu kama vile zinaa, kuiba, kuacha swalah na mengineyo. Na yule anayemuamini mtu mwema au kitu kisichoasi, kama mfano wa mti na jiwe, ni uovu kidogo kuliko yule anayemuamini yule anayeshuhudia anafanya madhambi na ufisadi na akathibitisha hilo.

MAELEZO

Kupitia ubainifu huu wa Shaykh Muhammad (Rahimahu Allaah) kuna ubainifu wa wazi wa hali ya juu kwa yule ambaye Allaah anamtakia uongofu katika kubainisha uhakika wa shirki waliyokuwemo wale wa mwanzo na yale waliyomo wale waliokuja nyuma. Hakika wale wa kale ni jambo liko wazi kwamba walikuwa wakishirikisha katika wakati wa raha ambapo wakiwaabudu Mitume, waja wema, miti, mawe na Malaika. Wanapofikwa na matatizo basi wanamtakasia Allaah nia. Hii ndio ilikuwa hali yao, kama alivyobainisha Allaah (Jalla wa ´Alaa) ndani ya Qur-aan:

فَإِذَا رَكِبُوا فِي الْفُلْكِ دَعَوُا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ فَلَمَّا نَجَّاهُمْ إِلَى الْبَرِّ إِذَا هُمْ يُشْرِكُونَ

“Wanapopanda merikebu humwomba Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini, lakini anapowaokoa katika nchikavu, tahamaki hao wanamshirikisha.”[1]

وَإِذَا غَشِيَهُم مَّوْجٌ كَالظُّلَلِ دَعَوُا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ فَلَمَّا نَجَّاهُمْ إِلَى الْبَرِّ فَمِنْهُم مُّقْتَصِدٌ ۚ وَمَا يَجْحَدُ بِآيَاتِنَا إِلَّا كُلُّ خَتَّارٍ كَفُورٍ

”Yanapowafunika mawimbi kama vivuli humwomba Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini. Lakini anapowaokoa katika nchikavu, basi miongoni mwao mwenye kushika mwendo wa wastani. Hawazikanushi alama Zetu isipokuwa kila khayini mkubwa, mwingi wa kukufuru.”[2]

وَإِذَا مَسَّكُمُ الضُّرُّ فِي الْبَحْرِ ضَلَّ مَن تَدْعُونَ إِلَّا إِيَّاهُ

”Inapokuguseni dhara baharini hupotea wale mnaowaomba isipokuwa Yeye pekee.”[3]

Hii ndio ilikuwa hali yao ambapo wakati wa shida wanamtakasia Allaah ´ibaadah. Wanaposukumwa na mawimbi na wakafikwa na majangwa wanamtakasia Allaah. Wanapokuwa na hali nzuri na amani wanamshirikisha Allaah. Ama wale waliokuja nyuma shirki yao inakuwa kipindi chote katika raha na shida. Bali wakati wa matatizo shirki yao inakuwa kubwa zaidi na utawaona wanamwita ´Abdul-Qaadir na Shaykh Ahmad al-Badawiy. Wanafanya hivi wakati wa shida kama kupatwa na mawimbi. Hali ni tofauti na walivokuwa wakifanya washirikina wa kale.

[1] 29:65

[2] 31:32

[3] 17:67

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 73-79
  • Imechapishwa: 20/10/2021