Inastahiki kwa mwanafunzi popote alipo azingatie Kitabu cha Allaah na ajaalie kule kukizingatia ni miongoni mwa hamu yake kubwa na ni miongoni mwa kazi yake kubwa. Aidha akitilie umuhimu mkamilifu kule kukisoma na kuzingatia zile maana tukufu zilizomo ndani yake na hoja zinazong´aa juu ya usahihi wa yale waliyokuja nayo Mitume, ukweli wa yale yaliyofahamishwa na Qur-aan na ubatilifu wa yale yanayosemwa na watu waovu popote wanapokuwa na vovyote watavokuwa.

Ambaye ataizingatia Qur-aan hali ya kuwa ni mwenye kutaka uongofu Allaah atamtukuza, atampa uelewa na atamfikisha kwenye malengo yake. Amesema (Subhaanah):

إِنَّ هَـٰذَا الْقُرْآنَ يَهْدِي لِلَّتِي هِيَ أَقْوَمُ

“Hakika hii Qur-aan inaongoza katika yaliyonyooka kabisa.”[1]

قُلْ هُوَ لِلَّذِينَ آمَنُوا هُدًى وَشِفَاءٌ

“Sema: “Hiyo ni kwa walioamini ni mwongozo na shifaa.””[2]

Vivyo hivyo Sunnah zilizotakasika muumini akizizingatia na akazingatia misimamo yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pamoja na maadui na wapinzani wake Makkah na Madiynah basi atajua haki na atatambua kuwa watu wa haki ni wenye kunusuriwa na wenye kupewa mtihani. Yule ambaye atakosa nusura duniani basi hatokosa malipo na badali Aakhirah. Amesema (´Azza wa Jall):

إِنَّا لَنَنصُرُ رُسُلَنَا وَالَّذِينَ آمَنُوا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيَوْمَ يَقُومُ الْأَشْهَادُ يَوْمَ لَا يَنفَعُ الظَّالِمِينَ مَعْذِرَتُهُمْ ۖ وَلَهُمُ اللَّعْنَةُ وَلَهُمْ سُوءُ الدَّارِ

“Hakika Sisi tutawanusuru Mitume Wetu na wale walioamini katika uhai wa dunia na siku watakayosimama mashahidi. Siku hazitowafaa madhalimu nyudhuru zao na watapata laana na watapata makazi mabaya.”[3]

Allaah (Subhaanah) amewaahidi nusura wale watendaji duniani na thawabu huko Aakhirah. Amesema (´Azza wa Jall):

وَلَيَنصُرَنَّ اللَّـهُ مَن يَنصُرُهُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَقَوِيٌّ عَزِيزٌ الَّذِينَ إِن مَّكَّنَّاهُمْ فِي الْأَرْضِ أَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ وَأَمَرُوا بِالْمَعْرُوفِ وَنَهَوْا عَنِ الْمُنكَرِ ۗ وَلِلَّـهِ عَاقِبَةُ الْأُمُورِ

“Bila shaka Allaah atamnusuru yule mwenye kuinusuru dini Yake – hakika Allaah ni Mwenye nguvu asiyeshindikana – ambao Tukiwamakinisha katika ardhi husimamisha swalah na hutoa zakaah na huamrisha mema na hukataza maovu. Kwa Allaah pekee ndio hatima ya mambo yote.”[4]

Katika Aayah hizi mbili Allaah amewaahidi wale wenye kuitendea kazi haki, wanasimamisha swalah na wanatoa zakaah kuwapa wale wenye kustahiki. Aidha wanaamrisha mema na wanakataza maovu. Amewaahidi (´Azza wa Jall) nusura. Ni nusura ilioenea ulimwenguni na kumakinishwa ndani yake. Pia watapata nusura na radhi kutoka kwa Allaah (Subhaanah) siku ya Qiyaamah. Katika haya kuna utukufu kwa waumini na udhalilifu kwa makafiri. Waumini watafuzu kwa Pepo na makafiri watakabiliwa na fedheha na majuto. Moto ndio utakuwa mahali pao na mapumziko yao. Amesema (Subhaanah) juu ya maana hii:

وَعَدَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَلَيُمَكِّنَنَّ لَهُمْ دِينَهُمُ الَّذِي ارْتَضَىٰ لَهُمْ وَلَيُبَدِّلَنَّهُم مِّن بَعْدِ خَوْفِهِمْ أَمْنًا ۚ يَعْبُدُونَنِي لَا يُشْرِكُونَ بِي شَيْئًا

“Allaah amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na wakatenda mema kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi – kama alivyowafanya makhalifa wale waliokuwa kabla yao – na atawamakinishia dini yao aliyowaridhia na atawabadilishia amani badala ya khofu yao – [kwa sharti] wananiabudu Mimi na hawanishirikishi na chochote.”[5]

Zipo Aayah nyingi zenye maana kama hii.

[1] 17:09

[2] 41:44

[3] 40:51-52

[4] 22:40-41

[5] 24:55

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahamiyyat-ul-´Ilm https://binbaz.org.sa/discussions/33/اهمية-العلم-في-محاربة-الافكار-الهدامة
  • Imechapishwa: 18/05/2022