Uislamu umekuja kuhifadhi mali na kuichuma kwa njia zinazokubalika katika Shari´ah zilizosalimika kutokamana na dhuluma, ulaghai, ribaa, kuwadhulumu watu na kuwashambulia. Ni kama ambavo Uislamu umekuja vilevile kuheshimu umiliki wa mtu mmojammoja na wa jamii nzima. Kwa hiyo Uislamu uko kati na kati baina ya nidhamu mbili, uchumi mbili na kati ya njia mbili za kilaghai. Matokeo yake Uislamu ukahalalisha mali, ukalingania kwayo na ukaita kuichuma kwa njia za busara. Mtu anayafanya yote hayo na wakati huohuo hayamshughulishi kutokamana na kumtii Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kutekeleza yale ambayo Allaah amemuwajibishia. Amesema (´Azza wa Jall):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَأْكُلُوا أَمْوَالَكُم بَيْنَكُم بِالْبَاطِلِ

”Enyi walioamini! Msiliane mali zenu kwa batili.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kila muislamu juu ya muislamu mwenzie ni haramu; damu yake, mali yake na heshima yake.”[2]

“Zindukeni! Hakika damu yenu, mali yenu na heshima yenu juu yenu ni haramu kama ilivyo utukufu wa siku yenu hii na katika mwezi wenu huu na katika nchi yenu hii.”[3]

“Mmoja wenu kuchukua kamba yake, alete mzigo wa kuni mgongoni kwake, auuze, kwa huo, Allaah ahifadhie heshima yake, kufanya hivo ni bora kwake kuliko kuombaomba watu ambapo watampa au watamnyima.”[4]

Aliulizwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni pato gani bora zaidi. Akajibu:

“Kazi ya mtu kwa mikono yake na kila uuzaji unaokubaliwa.”[5]

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mtu hajapato kula chakula kilicho bora kama kula kwa kazi itokanayo na mikono yake. Mtume wa Allaah Daawuud alikuwa anakula kwa kazi itokanayo na mikono yake.”[6]

Haya yanatubainishia kuwa nidhamu ya Uislamu juu ya mali inatokana na nidhamu ya kati na kati. Uislamu hauna rasilimali ya kikatili inayotoka nchi za magharibi na wafuasi wake wala haitokani na wakomunisti wakanamungu ambao wanahalalisha mali za watu na wakafuja heshima ya wenye nayo. Hawakujali na pia wakafanya wananchi kuwa watumwa, wakawatumia na wakahalalisha yale aliyoharamisha Allaah. Kwa hivyo unapaswa kuchuma mali na kuzitafuta kwa njia zilizowekwa katika Shari´ah. Wewe una haki zaidi ya mali na pato lako kwa njia iliyowekwa katika Shari´ah na Allaah na akaihalalisha.

[1] 04:29

[2] Muslim (2564).

[3] al-Bukhaariy (67) na Muslim (1218).

[4] al-Bukhaariy (1417) na Muslim (1042).

[5] Ahmad (04/141).

[6] al-Bukhaariy (2072).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Da´wah ilaa Allaah wa Akhlaaq-id-Du´aah, uk. 34-36
  • Imechapishwa: 14/06/2023