20. Mambo ambayo mlinganizi anatakiwa kuyapa kipaumbele

Kunaingia katika hayo kulingania katika kuamini yale yote aliyoeleza Allaah na Mtume Wake katika yaliyoko na yatayokuweko katika mambo yanayohusu Aakhirah, mambo ya zama za mwisho kabla ya Qiyaamah na mengineyo.

Kunaingia katika hayo kulingania katika yale aliyowajibisha Allaah katika kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan, kuhiji Nyumba na mengineyo.  

Kunaingia katika hayo pia kulingania katika kupambana jihaad katika njia ya Allaah, kuamrisha mema, kukataza maovu na kutendea kazi yale aliyoyaweka Allaah katika Shari´ah katika twaharah, swalah, mambo ya miamala, ndoa, talaka, uhalifu, matumizi, vita, amani na kila kitu. Kwa sababu dini ya Allaah imeenea. Imekusanya manufaa ya waja duniani na Aakhirah. Imekusanya pia kila wanachohitajia watu katika mambo ya dini na dunia yao.

Mtu anatakiwa kulingania pia katika tabia njema na matendo mazuri na sambamba na hilo akemee tabia mbaya na matendo mabaya. Inahusiana na kufanya ´ibaadah na kuongoza. Kwa maana ya kwamba anakuwa mfanya ´ibaadah na mwenye kuongoza jeshi. Ni ´ibaadah na hukumu. Anakuwa mwenye kufanya ´ibaadah, anayeswali na anayefunga. Pia anakuwa mwenye kuhukumu kwa Shari´ah ya Allaah na mwenye kutekeleza hukumu Zake (´Azza wa Jall).

Vilevile anakuwa mwenye kufanya ´ibaadah na kupambana jihaad. Analingania katika dini ya Allaah na anapambana katika njia ya Allaah kwa yule anayetoka nje ya dini ya Allaah. Anakuwa mwenye kushika msahafu na upanga. Anaizingatia na kuitafakari Qur-aan na kutekeleza hukumu zake kwa nguvu ijapo kwa upanga haja ikipelekea kufanya hivo.

Vilevile anakuwa mwenye kufanya siasa na umoja. Analingania katika maadili mema na udugu wa kiimani, kufanya umoja kati ya waislamu na kuunganisha kati yao. Amesema (Jalla wa ´Alaa):

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا

”Na shikamaneni kwa kamba ya Allaah nyote pamoja wala msifarikiane.”[1]

Dini ya Allaah inalingania katika umoja na katika siasa njema na yenye hekima ambayo inakusanya na wala haifarikishi. Siasa ambayo inaunganisha na wala haifanyi watu kuwa mbali. Siasa ambayo inalingania kuwa na mioyo safi, kuheshimu udugu wa Kiislamu, kushirikiana juu ya wema na kumcha Allaah, kutoa nasaha kwa ajili ya Allaah.

Vilevile anatakiwa kulingania kutekeleza amana na kuhukumu kwa Shari´ah na kuacha kuhukumu kinyume na yale aliyoteremsha Allaah (´Azza wa Jall). Amesema (Subhaanah):

إِنَّ اللَّـهَ يَأْمُرُكُمْ أَن تُؤَدُّوا الْأَمَانَاتِ إِلَىٰ أَهْلِهَا وَإِذَا حَكَمْتُم بَيْنَ النَّاسِ أَن تَحْكُمُوا بِالْعَدْلِ

“Hakika Allaah anakuamrisheni kurudisha amana kwa wenyewe na pindi mtakapohukumu kati ya watu, basi mhukumu kwa uadilifu.”[2]

Vilevile ni siasa na uchumi. Kama ambavo ni siasa, ´ibaadah na jihaad.  Vivyo hivyo anatakiwa kulingania katika uchumi unaokubalika katika Shari´ah na wa wastani. Sio mbepari, mwenye kufanya ghushi na dhalimu ambaye hajali mambo ya haramu na anakusanya mali kwa kila njia. Haihusiani na uchumi wa kikomunisti unaomkana Muumba ambao hauheshimu mali za watu na wala hajali kuwashinikiza, kuwadhulumu na kuwafanyia uadui. Si haya wala yale. Bali anakuwa wastani kati ya uchumi mbili; wastani kati ya njia mbili na haki kati ya batili mbili.

Wamagharibi wametukuza mali na wakachupa mpaka katika kuipenda na kuikusanya kiasi cha kwamba wameikusanya kwa kila njia na wakafuata yale aliyoharamisha Allaah (´Azza wa Jall). Makafiri wa mashariki ambao ni wasovieti na wale waliowafuata hawakuheshimu pesa za watu. Bali wameichukua na kuihalalisha. Hawakujali waliyoyafanya katika jambo hilo. Walifanya watu kuwa kama waja, wakawatesa wananchi, wakamkufuru Allaah, wakazikanusha dini na wakasema hakuna mungu na maisha ni pesa. Hawakujali pesa hizi na wala hawakujali kuichuma kwa isiyokuwa njia yake. Vilevile hawakujali njia za kuangamiza, kutawala pesa za watu, kizuizi kati ya watu na yale ambayo Allaah amewaumba kwayo katika kuchuma, kunufaika na kufaidika na uwezo na akili zao na zile zana ambazo Allaah amewatunuku. Si haya wala yale.

[1] 03:103

[2] 04:58

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Da´wah ilaa Allaah wa Akhlaaq-id-Du´aah, uk. 31-34
  • Imechapishwa: 14/06/2023