Swali 21: Ni ipi hukumu ya kupangusa juu ya kitata?

Jibu: Mosi tunapaswa kujua kitata ni kitu gani. Kitata ni aina fulani ya matibabu ambapo kiungo fulani cha mwili kilichovunjika kinafungwa banzi. Wanazuoni hukusudia kitu kinachohitajika kinachowekwa yale maeneo yanayotakiwa kuoshwa kama mfano wa plasta ambayo huwekwa ile sehemu ya kuvunjika au bendi inayowekwa kwenye kidonda au maeneo ya maumivu mgongoni au kwenginepo. Ni sahihi kupangusa juu yake badala ya mtu kuosha kiungo hicho. Kama yule mwenye kutawadha yuko na bendi anayoihitajia mkononi kwenye kidonda, basi inafaa kwake kupangusa juu yake badala ya kuosha kiungo hicho. Twahara hii inakuwa kamilifu. Hiyo ina maana kwamba twahara yake inabaki endapo mgonjwa huyu ataondosha plasta au bendi hiyo. Haichenguki kwa sababu imekamilika kwa njia inayokubalika katika Shari´ah. Hakuna dalili inayoonyesha kuwa kuondoshwa kwa plasta kunachengua wudhuu´ au twahara.

Kuna tofauti juu ya dalili zote zinazozungumzia kupangusa juu ya kitata. Kumepokelewa Hadiyth dhaifu juu yake. Baadhi ya wanazuoni wanaona kuwa zote zinapeana nguvu na kufanya ni dalili. Wanazuoni wengine wanaona kuwa ni dhaifu mno kiasi cha kwamba haziwezi kutegemewa. Wanazuoni hawa wa pili wametofautiana. Miongoni mwao wamesema kuwa hahitajii kusafisha yale maeneo ya banzi kwa sababu ameshindwa kufanya hivo. Wengine wamesema kuwa atafanya Tayammum na wala hatopangusa kiungo hicho.

Maoni yaliyo karibu zaidi na usawa (pasi na kujali zile Hadiyth zinazozungumzia mada hii) ni kwamba anatakiwa kupangusa juu yake. Ufutaji huu utamtosheleza kufanya Tayammum na hatohitajia kufanya hivo. Kutokana na haya nasema kuwa wakati donda linakuwa katika kiungo ambacho kinatakiwa kuoshwa kuna hali mbalimbali:

Hali ya kwanza: Liwe wazi na halidhuriwi na kuoshwa. Ni lazima kuosha kiungo hichi.

Hali ya pili: Liwe wazi na linadhuriwa na kuoshwa na si kupanguswa. Ni lazima kupangusa kiungo hichi na kisioshwe.

Hali ya tatu: Liwe wazi na linadhuriwa na kuoshwa na kupanguswa. Hapa anatakiwa kufanya Tayammum.

Hali ya nne: Limefunikwa kwa plasta au kitu kingine anachohitajia. Anatakiwa kupangusa kile kitu kilichofunika. Hapana haja ya kuosha wala kufanya Tayammum.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Buhuuth wa Fataawaa fiyl-Mas´h ´alaal-Khuffayn, katika Majmuu´-ul-Fataawaa (11/171-172)
  • Imechapishwa: 06/05/2021