21. Namna ya kuswali Tarawiyh kwa ufupi

Kwa jina la Allaah. Himdi zote njema anastahiki Allaah. Swalah na amani zimwendee Mtume wa Allaah, kizazi chake, Maswahabah zake na wale watakaofuata mwongozo wake.

Amma ba´d:

Nimefikiwa na khabari kwamba baadhi ya maimamu wa misikiti wanaswali katika Tarawiyh Rak´ah nne kwa pamoja kwa salamu moja, kisha Rak´ah nne nyenginezo kwa salamu moja. Kama ambavo nimefikiwa na khabari nyingine kwamba wako wengine wanaoswali Rak´ah nane kwa pamoja kwa salamu moja. Wanaona kuwa hayo ndio makusudio ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) pale aliposema katika Hadiyth Swahiyh:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiswali [Rak´ah] nne; usiulize juu ya uzuri wazo na urefu wazo, kisha akiswali [Rak´ah] nne; usiulize juu ya uzuri wazo na urefu wazo, kisha akiswali [Rak´ah] tatu.”[1]

Ufahamu huu ni kinyume na usawa na kinyume na Sunnah. Usawa ni kwamba makusudio yake ni kwamba alikuwa akiswali Rak´ah nne na akitoa salamu kila baada ya Tasliym mbili. Alichokusudia ni kuzisifu uzuri na urefu wake na si kwamba alikuwa anaziswali kwa salamu moja. Dalili ya hayo ni yale yaliyothibiti kutoka kwake yeye mwenyewe (Radhiya Allaahu ´anhaa) kwa al-Bukhaariy na Muslim ambao wamepokea kwamba ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa:

“Akiswali wakati wa usiku Rak´ah kumi ambapo akitoa salamu kila baada ya Rak´ah mbili kisha akiwitirisha kwa [Rak´ah] moja.”[2]

Hadiyth zake baadhi zinafasiri nyenginezo. Haijuzu kusafiri yale yaliyotajwa kwa njia ya ujumla kutoka katika Hadiyth yake kinyume na alivofasiri. Vilevile yanafahamisha hilo yale yaliyothibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Swalah ya usiku ni [Rak´ah] mbilimbili. Akichelea mmoja wenu kuingiwa na Subh basi ataswali Rak´ah moja anawitirisha kile alichoswali.”[3]

Maelezo haya kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) maana yake ni amri. Maana yake ni kwamba swalini usiku Rak´ah mbilimbili.

Kilichowekwa katika Shari´ah kwa muumini wa kiume na muumini wa kike ni kufungamana na yale yaliyowekwa wazi na Sunnah na atahadhari na yale yanayokwenda kinyume na hayo. Haifichiki ule wepesi unaopatikana kwa waswaliji na kutowatia uzito kwa kule kutoa salamu baada ya kila Rak´ah mbili ukiongezea na kwamba ni kuafikiana na Sunnah.

Lakini endapo mwanamme au mwanamke atataka kuswali Rak´ah tatu zote pamoja kwa salamu moja na kikao kimoja au Rak´ah tano zote pamoja kwa salamu moja hapana ubaya kufanya hivo. Kwa sababu imesihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba baadhi ya nyakati alikuwa akifanya hivo. Vivyo hivyo ni sawa endapo ataswali Witr kwa Rak´ah saba zote kwa pamoja kwa salamu moja.

Ni sawa pia iwapo ataswali Witr kwa Rak´ah saba pamoja ambapo akaketi katika ile Rak´ah ya sita na akasoma ile Tashahhud ya kwanza kisha akainuka kwenda katika Rak´ah ya saba. Kwa sababu imesihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwa alifanya yote mawili.

Vivyo hivyo ni sawa pia ikiwa ataswali Witr Rak´ah tisa pamoja ambapo akaketi katika ile Rak´ah ya nane na akasoma Tashahhud kisha akainuka katika Rak´ah ya tisa. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifanya hivo.

Lakini bora na kamilifu zaidi ni yeye kutoa salamu kila baada ya Rak´ah mbili kama tulivyotangulia kutaja. Haijuzu kuswali Witr kama Maghrib kwa njia ya kwamba akaketi katika ile Rak´ah ya pili baada ya kusoma Tashahhud ya kwanza kisha akasimama katika Rak´ah ya tatu. Kwani Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikataza kuifananisha Witr na Maghrib.

Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake.

[1] al-Bukhaariy (1147), Muslim (1219) na Ahmad (23307).

[2] Ahmad (24791), Muslim (1211) na Abu Daawuud (1334).

[3] al-Bukhaariy (991), Muslim (749), at-Tirmidhiy (461), an-Nasaa´iy (1694), Abu Daawuud (1421), Ibn Maajah (1175), Maalik (269) na ad-Daarimiy (1458).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Swalaat-it-Taraawiyh, uk. 21-23
  • Imechapishwa: 18/04/2022