21. Makatazo ya kujikakama na kuchupa mpaka

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

 Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَهْلَ الْكِتَابِ لِمَ تُحَآجُّونَ فِي إِبْرَاهِيمَ وَمَا أُنزِلَتِ التَّورَاةُ وَالإنجِيلُ إِلاَّ مِن بَعْدِهِ أَفَلاَ تَعْقِلُونَ هَاأَنتُمْ هَؤُلاء حَاجَجْتُمْ فِيمَا لَكُم بِهِ عِلمٌ فَلِمَ تُحَآجُّونَ فِيمَا لَيْسَ لَكُم بِهِ عِلْمٌ وَاللّهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لاَ تَعْلَمُونَ مَا كَانَ إِبْرَاهِيمُ يَهُودِيًّا وَلاَ نَصْرَانِيًّا وَلَكِن كَانَ حَنِيفًا مُّسْلِمًا وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ

“Enyi watu wa Kitabu! Kwanini mnahojiana kuhusu Ibraahiym na hali haikuteremshwa Tawraat na Injiyl isipokuwa baada yake? Je, hamtii akilini? Nyinyi ndio hawa mliohojiana katika yale ambayo mnayo elimu nayo, basi kwa nini [sasa] mnahojiana katika yale msiyokuwa na elimu nayo? Na Allaah anajua, na nyinyi hamjui. Hakuwa Ibraahiym myahudi wala mnaswara – lakini alikuwa ni mwenye imani iliyo safi na kutakasika na alikuwa ni muislamu; na hakuwa miongoni mwa washirikna.” (03:65-67)

وَمَن يَرْغَبُ عَن مِّلَّةِ إِبْرَاهِيمَ إِلَّا مَن سَفِهَ نَفْسَهُ ۚ وَلَقَدِ اصْطَفَيْنَاهُ فِي الدُّنْيَا ۖ وَإِنَّهُ فِي الْآخِرَةِ لَمِنَ الصَّالِحِينَ

“Na nani atakayejitenga na imani ya Ibraahiym isipokuwa anayeitia nafsi yake upumbavu? Na kwa hakika Tumemteua duniani, naye Aakhirah ni miongoni mwa waja wema.” (02:130)

Hadiyth kuhusu Khawaarij imeshatangulia. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kizazi cha baba fulani sio mawalii wangu. Si vyenginevyo mawalii wangu ni wale wachaMungu.”[1]

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Anas ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipata khabari kuwa kuna Maswahabah waliosema: “Mimi sintokula nyama.” Mwingine akasema: “Nitaswali tu na sintolala.” Mwingine akasema: “Mimi sintooa.” Mwingine akasema: “Nitafunga mwaka mzima.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Mimi ninaswali na kulala, ninafunga na kuacha, ninaoa wanawake na nala nyama. Atakayeipa mgongo Sunnah yangu basi huyo si katika mimi.”[2]

Tafakari ni ukali namna gani Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivyowakemea baadhi ya Maswahabah pindi walipotaka kuishi maisha ya kiutawa kwa ajili ya kumwabudu Allaah na akatamka maneno haya mazito na pia akaita matendo yao kuwa ni kuipa mgongo Sunnah yake. Unasemaje inapokuja katika Bid´ah nyinginezo? Unasemaje inapokuja kwa wengine wasiokuwa Maswahabah?

MAELEZO

Hapa kuna matahadharisho ya kujikalifisha na kujikakama na kwamba ni lazima kwa muumini kutahadhari hayo. Mara afunge, mara nyingine afungue, mara aswali, mara alale, ale nyama, alale juu ya kitanda na asijikalifishe. Kwa ajili hii Mtume wa Allaah Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Mimi ninaswali na kulala, ninafunga na kuacha, ninaoa wanawake na nala nyama. Atakayeipa mgongo Sunnah yangu basi huyo si katika mimi.”

Allaah amewawekea Shari´ah waja yale yasiyowatia uzito. Kwa hivyo haifai kuchupa mpaka na kujikalifisha. Katika Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuna yenye kutosheleza ilihali yeye ndiye mtukufu na mbora zaidi ya watu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] al-Bukhaariy (5990) na Muslim (215).

[2] al-Bukhaariy (5063) na Muslim (1401).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Fadhwl-il-Islaam, uk. 37-38
  • Imechapishwa: 04/11/2020