21. Je, ni haramu kuvaa nguo zinazovuka kongo mbili za miguu ikiwa ni pasi na kiburi au hapana?

Swali 21: Je, ni haramu kuvaa nguo zinazovuka kongo mbili za miguu ikiwa ni pasi na kiburi au hapana?

Jibu: Wanamme kuvaa nguo inayovuka tindi mbili za miguu ni haramu. Ni mamoja mtu amefanya hivo kwa kiburi au bila kiburi. Lakini ikiwa kumeambatana na kiburi basi adhabu yake ni kubwa na mbaya zaidi kutokana na Hadiyth ya Abu Dharr iliyothibiti katika “as-Swahiyh” ya Muslim ambaye amesimulia ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu aina tatu hatowasemeza Allaah siku ya Qiyaamah, hatowatakasa na watakuwa na adhabu kali.” Abu Dharr akasema: “Ni kina nani, ee Mtume wa Allaah, wamekula patupu na wamekhasirika?” Akasema: “Mwanaume mwenye kuvaa nguo ndefu yenye kuvuka kongo mbili za miguu, mzee mzinifu, mtu fakiri mwenye kiburi na mtu ambaye kamfanya Allaah ndio bidhaa yake; hanunui isipokuwa kwa kuapa na wala hauzi isipokuwa kwa kuapa.”[1]

Hadiyth hii ni yenye kuenea, lakini hata hivyo inafanywa maalum kwa Hadiyth ya Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah hatomtazama ambaye anaburuza nguo yake kwa kiburi.”[2]

Kwa hivyo ueneaji katika Hadiyth ya Abu Dharr unafanywa maalum kwa Hadiyth ya Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa). Ikishakuwa anafanya hivo kwa kiburi basi Allaah hatomtazama, hatomtakasa na pia atakuwa na dhabu kali. Adhabu hii ni kubwa zaidi kuliko adhabu atayopata yule ambaye anaburuza nguo yake chini ya kongo mbili za miguu pasi na kiburi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu ya mtu huyo:

“Kile kilicho chini ya kongo mbili za miguu katika kikoi ni Motoni.”[3]

Pindi ilipokuwa adhabu mbili zinatofautiana, basi kunazuilika maandiko yaliyoachiwa kuyafasiri yaliyofungwa. Kwa sababu ili maandiko yaliyoachiwa kuyafasiri yaliyofungwa ni sharti maandiko hayo mawili yawe na hukumu moja. Lakini ikiwa hukumu inatofautiana, basi andiko moja haliwezi kufungamanishwa na jengine. Kwa ajili hiyo Aayah inayozungumzia Tayammum ambapo Allaah (Ta´ala) amesema:

وَإِن كُنتُمْ جُنُبًا فَاطَّهَّرُوا ۚ وَإِن كُنتُم مَّرْضَىٰ أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ أَوْ جَاءَ أَحَدٌ مِّنكُم مِّنَ الْغَائِطِ أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ فَلَمْ تَجِدُوا مَاءً فَتَيَمَّمُوا صَعِيدًا طَيِّبًا فَامْسَحُوا بِوُجُوهِكُمْ وَأَيْدِيكُم مِّنْهُ

“Mkiwa na janaba, basi jitwaharisheni na mkiwa wagonjwa au mko safarini au mmoja wenu akija kutoka msalani au mmewagusa wanawake kisha hamkupata maji, basi fanyeni Tayammum kwa ardhi kwa juu panguseni kwayo nyuso zenu na mikono yenu.”[4]

hatukuifungamanisha na Aayah ya wudhuu´ inayosema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا قُمْتُمْ إِلَى الصَّلَاةِ فَاغْسِلُوا وُجُوهَكُمْ وَأَيْدِيَكُمْ إِلَى الْمَرَافِقِ

“Enyi mlioamini!  Mnaposimama kwa ajili ya swalah, basi osheni nyuso zenu na mikono yenu mpaka kwenye visugudi.”[5]

Kwa ajili hiyo Tayammum haitambai kwenda mpaka kwenye visugudi. Kinachofahamisha hayo ni yale aliyopokea Maalik na wengineo kutoka katika Hadiyth ya Abu Sa´iyd al-Khudriy ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kuwa kikoi cha muumini ni mpaka kwenye nusu ya muundi wake, kwamba kile kilicho chini ya kongo mbili za miguu katika kikoi ni Motoni na kwamba Allaah hatomtazama ambaye anaburuza nguo yake kwa kiburi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akataja mifano miwili katika Hadiyth moja na akabainisha kutofautiana kwa hukumu zake kwa kutofautiana kwa adhabu zao. Ni wenye kutofautiana katika kitendo na pia ni wenye kutofautiana katika hukumu na adhabu. Kutokana na haya yanabainika makosa ya wale ambao wamefungamanisha maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kile kilicho chini ya kongo mbili za miguu katika kikoi ni Motoni.”

kwa maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah hatomtazama ambaye anaburuza nguo yake kwa kiburi.”

Licha ya haya wapo watu pindi wanapokatazwa kuvaa nguo inayovuka kongo mbili za miguu wanasema kuwa wao hawavai kwa kiburi. Tunawaambia kuna sampuli mbili za nguo inayovuka kongo mbili za miguu. Aina ya kwanza ya adhabu ni mtu kuadhibiwa yale maeneo aliyotenda dhambi peke yake, nacho ni kile kilicho chini ya mafundo mawili ya miguu pasi na kiburi. Huyu ataadhibiwa na Allaah ikiwa ni pamoja na kutomtazama na kutomtakasa. Lakini yule anayeburuza nguo zake kwa kiburi Allaah atamuadhibu kwa kutomsemeza, hatomtazama wala hatomtakasa siku ya Qiyaamah na atakuwa na adhabu kali. Hivi ndivo tunavyomwambia.

Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake.

[1] Muslim, Abu Daawuud, an-Nasaa´iy na Ibn Maajah.

[2] al-Bukhaariy.

[3] al-Bukhaariy na Ahmad.

[4] 05:06

[5] 05:06

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: As-ilah Muhimmah, uk. 28-30
  • Imechapishwa: 01/03/2023