04. Miongoni mwa baraka za usiku wa Qadar

Miongoni mwa baraka za usiku wa Qadar ni kwamba Allaah ameteremsha Qur-aan ndani yake. Amesema (Ta´ala):

إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ وَمَا أَدْرَاكَ مَا لَيْلَةُ الْقَدْرِ  لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْرٍتَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِم مِّن كُلِّ أَمْرٍ سَلَامٌ هِيَ حَتَّىٰ مَطْلَعِ الْفَجْرِ

“Hakika Sisi tumeiteremsha Qur-aan katika usiku wa Qadr. Na kipi kitakachokujulisha ni nini huo usiku wa Qadr? Usiku wa Qadr ni mbora kuliko miezi elfu: wanateremka humo Malaika na Roho kwa idhini ya Mola wao kwa kila jambo. Ni amani mpaka kuchomoza alfajiri!”[1]

Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah) amesema:

“Maneno Yake Allaah aliposema:

تَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِم

“Wanateremka humo Malaika na Roho kwa idhini ya Mola wao…. “

Malaika huteremka kwa wingi ndani ya usiku huu kutokana na wingi wa baraka zake. Malaika hushuka pamoja na kuteremka kwa baraka na rehema kama ambavo wanashuka wakati kunaposomwa Qur-aan, wanazunguka vikao ambavyo anatajwa Allaah na wanamuwekea mbawa zao mwanafunzi kwa ukweli kutokana na kumtukuza kwao.”[2]

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“… usiku wa Qadar.”

ima ikawa ni kwa njia ya kukiegemeza kitu katika sifa yake. Kwa msemo mwingine usiku wenye cheo, au ni kutokana na makadirio na uendeshaji. Kwa maana nyingine inakuwa na maana ya usiku ambao kunakadiriwa mambo yatakayopitika katika mwaka huo. Amesema (Ta´ala):

فِيهَا يُفْرَقُ كُلُّ أَمْرٍ حَكِيمٍ

“Humo hupambanuliwa kila jambo la hekima.”[3]

Qataadah amesema:

“Hupambanuliwa ndani yake jambo la mwaka mzima.”[4]

Ibn-ul-Qayyim amesema:

“Haya ndio maoni sahihi.”[5]

Kinachodhihiri ni kwamba hakuna kizuizi cha kuzingatia maana zote mbili.”[6] Allaah ndiye mjuzi zaidi.

Hakika huu ni usiku mtukufu ambao Allaah ameuchagua uwe mwanzo wa kuteremka kwa Qur-aan. Kwa hivyo ni lazima kwa muislamu kutambua nafasi yake, auhuishe kwa imani na kutaraji thawabu za Allaah. Aidha ni lazima akithirishe du´aa katika nyusiku ambazo kunatarajiwa ndani yake usiku wa Qadar. Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah) amesema:

“Inapendeza kuomba du´aa nyingi katika vipindi vyote na mtu azidishe du´aa ndani ya Ramadhaan, katika kumi lake la mwisho na afanye hivo zaidi katika zile siku zake za witiri. Inapendeza aombe du´aa ifuatayo kwa wingi:

اللَّهُمَّ إِنَّكَ عُفُوٌّ تُحِبُّ الْعَفْوَ فَاعْفُ عَنِّي

“Ee Allaah! Hakika Wewe ni Mwingi wa kusamehe na unapenda kusamehe. Hivyo basi, nisamehe.”

[1] 97:01-05

[2] Tafsiyr Ibn Kathiyr (08/465).

[3] 44:04

[4] at-Twabariy katika ”Tafsiyr” yake (25/65), al-Bayhaqiy katika ”Fadhwl-ul-Awqaat”, uk. 216 na cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh.

[5] Shifaa-ul-´Aliyl, uk. 42.

[6] Tafsiyr Ibn Kathiyr (08/472). Hadiyth iliyotajwa ameipokea at-Tirmidhiy (3513), an-Nasaa´iy katika “al-Kabiyr” (09/322), Ibn Maajah (3850) na Ahmad (42/236).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 62-63
  • Imechapishwa: 01/03/2023