21. Ibn Mas´uud akihimiza Sunnah na akitahadharisha Bid´ah

Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Fuateni na wala msizue, kwani hakika mmetoshelezwa.”[1]

´Umar bin ´Abdil-´Aziyz (Radhiya Allaahu ´anh) amesema maneno yakiwa na maana ifuatayo:

“Simama pale ambapo walisimama watu, kwa hakika walisimama juu ya elimu na ujuzi. Wao katika kitu kizuri, walikuwa ni wenye nguvu na fadhilah kubwa kwa kukifanya hadharani. Ikiwa mtasema: “Kimezuka baada yao, basi hakikuzushwa na yeyote isipokuwa yule anayekwenda kinyume na uongofu wao na kuipa mgongo Sunnah yao. Walionyesha yenye kukidhi na kuzungumza kwa yanayotosheleza. Yaliyo juu ya hayo, ni kujichosha bure na khasara, na yaliyo chini ya hayo ni mapungufu. Kuna watu waliopunguza waliyokuwemo, yakawafanya kuzembea, wakati wengine wakavuka mipaka waliyokuwemo, yakawafanya kuchupa mpaka. Baina ya hao wawili ndio wako juu ya uongofu uliyonyooka.”[2]

Imaam Abu ´Amr al-Awzaa´iy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Lazimiana na Aathaar za waliotangulia, hata kama watu watakukataa, na jihadhari na maoni ya watu, hata kama watakupambia kwa maneno.”[3]

MAELEZO

Aathaar zilizopokelewa juu ya kuhimiza Sunnah na kutahadharisha Bid´ah

2 – Miongoni mwa maneno ya Maswahabah amesema Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ni Swahabah mtukufu aliyekufa mwaka wa 32 akiwa na miaka sitini na kitu:

“Fuata… “

Lazimiana na Aathaar za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pasi na kuzidisha wala kupunguza.

“… na wala msizue.”

Msizue Bid´ah ndani ya dini.

“… kwani hakika mmetoshelezwa.”

Wamekutoshelezeni wale wa awali waliokutangulieni juu ya mambo muhimu katika dini kwa vile Allaah ameikamilisha dini kupitia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akateremsha maneno Yake:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ

“Leo Nimekukamilishieni dini yenu.”[4]

Kwa hiyo haihitaji kukamilishwa.

[1] ad-Daarimiy (211), at-Twabaraaniy katika ”al-Kabiyr (9/168), al-Laalikaa´iy katika “Sharh Usuul-ilI´tiqaad Ah-is-Sunnah wal-Jamaa´ah” (104), al-Marwaziy katika “as-Sunnah” (23), Ibn Wadhdhwaah katika “al-Bid´ah wan-Nahiy ´anhaa” (10), al-Haythamiy katika “al-Majmah” (1/181). Imaam al-Haythamiy (Rahimahu Allaah) amesema: “Wapokezi wake ni waaminifu.”

[2] Abu Nu´aym (5/338-339) na wengine.

[3] al-Khatwiyb al-Baghdaadiy katika ”Sharaf Asw-haab-il-Hadiyth” uk. 7, al-Ajjurriy katika “ash-Shari´ah”, uk. 58, Ibn ´Abdil-Barr katika Bayaan Fadhwl-il-´Ilm” (2/114) na wengine. Imaam al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) amesema kuwa ni Swahiyh katika “Mukhtaswar-ul-´Uluww”, uk. 138. 22 Tazama “Siyar A´laam-in-Nubalaa” (11/314) ya Imaam adh-Dhahabiy (Rahimahu Allaah) na “al-Bidaayah wan-Nihaayah” (1/335) ya Imaam Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah).

[4] 05:03

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 40-43
  • Imechapishwa: 14/10/2022