20. Sunnah ni lazima ifuatwe na Bid´ah ni lazima iepukwe

Sunnah na Bid´ah na hukumu ya kila kimoja

Sunnah kilugha ni njia. Sunnah maana yake kiistilahi ni yale aliyokuwa akifuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake katika ´Aqiydah au matendo.

Ni lazima kufuata Sunnah. Amesema (Ta´ala):

لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّـهَ كَثِيرًا

“Hakika mna kigezo chema kwa Mtume wa Allaah kwa yule mwenye kumtaraji Allaah na siku ya Mwisho na akamtaja Allaah kwa wingi.”[1]

 Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Jilazimieni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu na wenye kuongoza baada yangu. Ziumeni kwa magego yenu.”[2]

Bid´ah maana yake kilugha ni kitu chenye kuzuliwa. Bid´ah maana yake kiistilahi ni kile chenye kuzuliwa katika dini ambacho kinapingana na yale aliyokuwa akifuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake sawa katika mambo ya ´Aqiydah au matendo.

Bid´ah ni haramu. Amesema (Ta´ala):

وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا

”Yule atakayempinga Mtume baada ya kuwa imeshambainikia uongofu na akaifuata njia isiyokuwa ya waumini, Tutamgeuza alikogeukia na tutamuingiza Motoni – na ni uovu ulioje mahali pa kuishia!”[3]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Tahadharini na mambo yaliyozuliwa. Kwani hakika kila kilichozuliwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu.”[4]

[1] 33:21

[2] Abu Daawuud (4607), at-Tirmidiy (2678), Ahmad (4/126-127), ad-Daarimiy (1/44-45), Ibn Maajah (42-43), al-Haakim (1/95) na wengine. Imaam Ibn Hibbaan, Imaam al-Ajjurriy na Imaam al-Albaaniy (Rahimahumu Allaah) wamesema kuwa ni Swahiyh. Tazama “Swahiyh al-Jaamiy´ as-Swaghiyr” (2/344) ya Imaam al-Albaaniy (Rahimahu Allaah).

Faida!

Haafidhw Ibn Rajab amesema alipokuwa akitoa maelezo yake juu ya Hadiyth hii kuhusu mambo yaliyozuliwa na kuyahesabu:

“Kigumu zaidi kuliko hayo ni yale maneno yaliyozuliwa kuhusu dhati na sifa za Allaah ambayo yamenyamaziwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Maswahabah na wale waliowafuata kwa wema. Baadhi wamekanusha mengi katika yale yaliyotajwa ndani ya Qur-aan na Sunnah katika hayo na wakadai eti wamefanya hivo kwa ajili ya kumtakasa Allaah katika yale ambayo akili imepelekea kumtakasa nayo. Aidha wakadai kuwa yanayopelekea huko ni mambo yasiyowezekana kabisa kwa Allaah (´Azza wa Jall). Wengine hawakutosheka kuzithibitisha mpaka wakathibitisha yale wanayodhani kuwa yanamlazimu kwa nisba ya viumbe. Malazimisho haya – ni mamoja kwa njia ya kukanusha na kuthibitisha – ni mambo ambayo kile kizazi cha kwanza cha Ummah kilishika njia ya kuyanyamazia.” (Jaamiy´-ul-´Uluum wal-Hikam, uk. 365)

[3] 04:115

[4] Abu Daawuud (4607), at-Tirmidiy (2678), Ahmad (4/126-127), ad-Daarimiy (1/44-45), Ibn Maajah (42-43), al-Haakim (1/95) na wengine. Imaam Ibn Hibbaan, Imaam al-Ajjurriy na Imaam al-Albaaniy (Rahimahumu Allaah) wamesema kuwa ni Swahiyh. Tazama “Swahiyh al-Jaamiy´ as-Swaghiyr” (2/344) ya Imaam al-Albaaniy (Rahimahu Allaah).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 40
  • Imechapishwa: 14/10/2022